Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri George Simbachawene na Mheshimiwa Angellah Kairuki, Naibu Waziri, Mheshimiwa Jafo pamoja na Viongozi wote walioko kwenye Wizara zao. Nawapongeza kwa hotuba zao nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu suala la afya, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kutembelea hospitali ya Muhimbili, baada ya yeye kutembelea Muhimbili huduma zimeboreka, hakukuwa na kipimo cha MRI, MSD imeanzisha duka pale Muhimbili, wananchi wanapata huduma ya kupata dawa kwa bei rahisi. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie Mkoa wetu wa Kigoma. Serikali kwa kushirikiana na wananchi walijenga vituo vya afya, wakajenga zahanati, hii ni katika nchi nzima, lakini zahanati pamoja na vituo vya afya vilivyojengwa havina watumishi. Watumishi limekuwa ni tatizo, dawa limekuwa ni tatizo, vifaa tiba limekuwa ni tatizo. Kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Kigoma, Mkoa wa Kigoma una Wilaya saba, Mkoa wa Kigoma umekumbwa na wimbi kubwa la Wakimbizi. Wakimbizi wanatibiwa kambini lakini wakati mwingine wanaletwa kwenye hospitali za wilaya. Mkoa wa Kigoma hauna Daktari Bingwa, Hospitali ya Maweni Daktari Bingwa ni mmoja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu fikiria, wananchi wa Wilaya zote saba wanapewa rufaa, wanapelekwa kwenye hospitali ya Maweni ambayo ndiyo hospitali ya Mkoa, lakini Daktari Bingwa ni mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuletewe Madaktari katika Mkoa wa Kigoma. Najua Muhimbili wapo Madaktari wa kutosha lakini huku Mikoa ya pembezoni Madaktari hawatoshi. Kwa kuuangalia Mkoa wa Kigoma naomba upewe kipaumbele kutokana na wimbi kubwa la Wakimbizi kutoka DRC na Burundi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Kasulu lipo vile vile tatizo la upungufu wa Watumishi, hatuna ultra sound, wanawake wanateseka, wanapata shida wanapokwenda kuambiwa wapimwe, wanakuta ultra sound hamna, hawawezi kujua mtoto amelalaje tumboni, kwa hiyo wanalazimika kwenda katika hospitali za kulipia. Naomba tuletewe ultra sound kuwaondolea adha wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Wauguzi ni wachache, utamkuta Muuguzi mmoja pengine yupo kwenye wodi ya akinamama, akinamama wanaotaka kujifungua wako nane ama kumi, Wauguzi wapo wawili, wanawake wanaohitaji kujifungua wako kumi, hebu angalia tofauti iliyopo, watu wawili kuhudumia watu kumi! Matokeo yake wanawake wanapoteza maisha na wakati mwingine watoto wanazaliwa wakiwa wamekufa? Naomba tuongezewe Waganga pamoja na Wahudumu wa Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia suala la maji. Nimewahi kusema Tanzania tumejaliwa kuwa na vyanzo vingi vya maji; maziwa, mito mikubwa na midogo lakini maji yamekuwa ni tatizo kubwa linalowakumba wanawake. Naomba Serikali itenge pesa kwa ajili ya kufikisha maji vijijini ili kuwaondolea adha wanawake ambao wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu. Utamkuta mwanamke muda mwingi anatumia kwenda kutafuta maji, anashindwa kufanya shughuli za uzalishaji mali. Kwa hiyo, naomba Serikali itenge pesa, ipeleke pesa ili maji yaweze kufikishwa vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wa Kasulu lipo tatizo la mabomba kutoa maji machafu, Serikali imekuwa ikitenga pesa kupeleka Kasulu kwa ajili ya kuanzisha miradi iliyokwishaanzishwa katika Wilaya ya Kasulu. Naomba kupitia bajeti hii mtupelekee pesa ili miradi iliyoanzishwa iweze kukamilika. Mtupelekee pesa kwa ajili ya Mji wa Kasulu ambao maji yanatoka machafu bombani ili maji yaweze kutibiwa, kwa sababu maji yakiwa siyo salama ni hatari kwa maisha ya binadamu. Ipo miradi ya Kasangezi, Ahsante Nyerere, Heluwishingo na Nyarugusu pamoja na Nyumbigwa naomba pesa zipelekwe ili miradi hiyo iweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Walimu walipwe stahiki zao kwa sababu ni kilio cha muda mrefu. Walimu wanateseka sana wakati mwingine Mwalimu anahamishwa kutoka kituo hiki kupelekwa kituo kingine lakini halipwi pesa ya uhamisho. Siyo hivyo tu Walimu wanapata shida, hela za matibabu hawapewi, sisi tunapata pesa ya matibabu lakini Mwalimu hapewi pesa ya matibabu, hivi kwa nini Mwalimu anatengwa? Wakati mwingine anaweza kwenda akapewa hata sh. 20,000 au sh. 40,000. Hivi kweli mtu unampa sh. 20,000 au sh. 40,000, shika hizi kwanza zikusaidie halafu nyingine utadai! Naomba watendewe haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia wastaafu nao; naomba wanapostaafu pesa zao ziwafikie mara moja, wengine wamekuwa wakistaafu wakiwa wamerekebishiwa mishahara, lakini Serikali inashindwa kurekebisha mishahara yao kulingana na jinsi walivyopanda madaraja, matokeo yake wanastaafu wakiwa na mishahara ile ambayo walikuwa nayo huko nyuma. Ile ambayo wamepandishwa madaraja na wamekiri kupanda daraja inachelewa kufanyiwa marekebisho, matokeo yake wanapata pensheni ambayo hailingani na mishahara yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuja na wazo la kukarabati shule za sekondari ambazo ni kongwe, kwa mfano, Tabora Boys, Tabora Girls, Pugu na kadhalika. Naomba Serikali itenge pesa na Kigoma Sekondari nayo iweze kukarabatiwa, hii ni shule kongwe, naomba Serikali iweze kuikumbuka Sekondari ya Kigoma ambayo ndiyo amesoma Mheshimiwa Zitto, amesoma Kigwangallah, na wengine wengi. Naomba shule hiyo ikumbukwe, ni shule kongwe nayo ipelekewe pesa kwa ajili ya ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo kuhusu milioni 50. Naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutenga shilingi milioni 50. Imekuwepo mikakati mingi kwa muda mrefu ya kutenga pesa kwa ajili ya kuwapelekea vijana na wanawake, lakini mipango hiyo imekuwa haitekelezeki, zilipelekwa pesa kidogo kidogo kupitia SIDO, kupitia SELF…..
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.