Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hoja iliyoko mbele yetu. Niungane na wenzangu kwanza kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kutujalia uzima. Vilevile niwashukuru wananchi wa Jimbo la Nkasi Kusini kwa kunirejesha tena kwenye nafasi hii. Nawaahidi nitawatumikia kwa heshima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wenzangu wote wanaounga mkono hoja hii. Katika kuchangia, naomba nianze na kuiangalia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Katika ukurasa wake wa 16, alijaribu kubainisha maeneo ambayo yakishughulikiwa yanaweza kuwa na mchango mkubwa sana katika kuinua uchumi wa nchi hii.
Vilevile alielezea namna ambavyo sekta mbalimbali zinavyochangia katika uchumi wa Taifa na kutoa ajira. Sekta hizo ni kilimo, uvuvi na ufugaji bila kusahau wachimbaji wadogowadogo. Tunafahamu kwamba kilimo kinachangia kuwapatia ajira Watanzania kwa zaidi ya asilimia 75. Vilevile kwenye GDP kilimo kina mchango wa zaidi ya asilimia 25 na kinasaidia kutuingizia fedha za kigeni kwa zaidi ya asilimia 30. Kwa hiyo, kwa wachumi na maafisa wetu wanaopanga mipango, hapa ndiyo mahali ambapo pangezingatiwa tungeweza kuubeba mzigo mkubwa na kuhakikisha kwamba tunaboresha uchumi wa nchi yetu ambao umezorota kwa kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia napenda kuangalia katika suala zima la kilimo. Ninavyoona mimi kilimo hatukiendeshi vizuri licha ya sera nzuri ambazo tumeziweka kwenye kilimo za kuchangia pembejeo mbalimbali, lakini bado kumekuwa na uchakachuaji ambao umesababisha matarajio kutofikiwa. Inaonekana hakuna anayesimamia kilimo kwa karibu. Nashukuru kupata Waziri wetu, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, naomba ajielekeze kwenye kilimo. Ametueleza kwenye historia yake kwamba ametoka kijijini na amekuwa mtoto wa mkulima sasa adha zile alizozipata na aka-fluke kwa kubahatisha mpaka kufikia hapo alipo leo, ndiyo zimewabana Watanzania wengi. Akikaa vizuri kushughulikia kilimo, anaweza akawatoa watu wa aina yake wengi ambao wamekosa fursa kwa sababu kilimo hakishughulikiwi na watu wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie sekta hii, wakulima, wafugaji na wavuvi, hawapati incentive zinazotakiwa kutoka Serikalini. Ruzuku inayotengwa kwa wakulima haziwafikii wakulima, kuna watu wako katikati hapa wanachakachua na inaonekana ni kama tunawashindwa. Nawashangaa Wizara hii ambayo imesheheni wasomi mnashindwaje kutatua changamoto hizi ambazo zinatusumbua kila mwaka? Katika miaka kadhaa tunahangaika jinsi gani ruzuku itawafikia wakulima, mbolea zinachakachuliwa, fedha zinatengwa na tumeona takwimu hapa lakini hatuoni tija, ni jambo la kushangaa. Naomba tuielekeze Serikali yetu ihakikishe wakulima wanatazamwa kwa macho mawili na changamoto zinazowahusu zishughulikiwe vizuri kwa sababu zinabeba Watanzania wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wakulima wamegawanyika, tunaposema wakulima wako wavuvi pia. Katika Jimbo langu vijiji zaidi ya 30 viko mwambao wa Ziwa Tanganyika. Hawa ndiyo wamesahaulika kabisa, hawajasaidiwa chochote, Serikali haijaonyesha juhudi kuwasaidia wavuvi. Wavuvi wanaishi tofauti na mazingira yao, mazingira yanaonyesha kuna utajiri mkubwa lakini maisha yao bado ni hafifu sana. Maeneo mengi ya wavuvi utakuta ni watu ambao wanatumikia watu wengine licha ya kwamba rasilimali zinazowazunguka zinaonyesha utajiri mkubwa lakini wameshindwa kwa sababu hawajasaidiwa inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yetu isaidie kwa kuwapa vifaa vya kisasa vya uvuvi na ikiwezekana kuwapelekea vitu ambavyo vinaweza kuwa vichocheo vya uwekezaji na kichocheo kimojawapo ni umeme. Suala la umeme lingefanyiwa utaratibu tukapata umeme wa kutosheleza katika maeneo ya Ziwa Tanganyikia maana yake tungeweza kuwavutia wawekezaji katika sekta hii. Ule ukibarua wanaofanya sasa hivi wa kupeleka samaki na dagaa nje ya nchi kwenda kuuza wangeweza kuwekeza hapahapa na tungeweza kuwa tumewasaidia vizuri kuliko ilivyo sasa. Naomba suala hilo liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ambayo napenda kuchangia ni suala hili hili la umeme lakini nazungumzia kupatiwa umeme mkubwa zaidi kuliko uliopo sasa. Katika bajeti ya mwaka jana kulikuwa na utaratibu wa kusafirisha umeme kwenye Gridi ya Taifa kutoka Nyakanazi kuleta Kigoma, Mpanda na Sumbawanga. Lengo kubwa lilikuwa ni kuunganisha Mikoa hii na umeme mkubwa zaidi kwa kujua kwamba ni mikoa ambayo kwa kweli ni tajiri na ina bahati nzuri ya kilimo na ingeweza kusaidia pia ku-attract wawekezaji ambao wangeweza kutusaidia.
Kwa hiyo, nia hii naomba iendelee, tusiiachie maana katika mipango hii iliyowekwa sasa hivi sijaona kama kuna mwendelezo huu. Kwa hiyo, naiomba Serikali ione wazo hili linapewa kipaumbele na tunaenda nalo ili kuwasaidia wananchi wa maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la msingi na la mwisho ni barabara. Katika kuunganisha mikoa yetu, ipo miradi ya barabara inayosuasua. Barabara ya kutoka Sumbawanga kwenda Mpanda ni barabara ya muda mrefu na hatuwezi kuzungumzia masuala ya uchumi kuwasaidia wananchi kama hatuwezi kuboresha miundombinu hii kwa kasi inayotakiwa, sasa hivi ujenzi wake unasuasua sana. Nashauri Serikali kuongeza kasi katika ujenzi wa barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali isisahau barabara zinazoenda kwa wakulima. Katika Jimbo langu kuna barabara ambazo zinaelekea kwenye vijiji vya Katani na Myiula. Vijiji hivi vinazalisha kwa wingi lakini inafika wakati barabara zinajifunga. Kwa hiyo, juhudi ambayo wananchi walikuwa wamewekeza kwenye kilimo inakosa faida kwa sababu hawafikiwi na masoko na wala huduma muhimu kama za pembejeo kwa sababu barabara zimefunga. Kwa hiyo, muone uwezekano wa kuongeza fedha ili kushughulikia barabara zinazoenda kwenye maeneo ya uzalishaji kama maeneo ya Myiula, Chonga, Charatila ambayo katika Jimbo langu ni muhimu sana kwa uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ni muhimu kulizungumzia ni suala la maji. Maji katika maeneo yetu yamekuwa ni tatizo na hapa tumekuwa tukizungumza juu ya miradi mbalimbali ya maji ikiwepo mradi wa King‟ombe. Mradi wa King‟ombe ulitengewa zaidi ya shilingi 500,000,000 kwa kijiji kimoja lakini mpaka fedha hizo zimekwisha kijiji hicho hakijapata maji. Jambo hili tumelizungumza kwenye Bunge lililopita, Mheshimiwa Keissy amezungumza sana hapa, hakuna anayesikia suala hili. Mpaka mwisho tunakuwa na wasiwasi pengine hawa watu tunaowaambia ni sehemu ya tatizo.
Naomba mliangalie suala hili. Ukienda King‟ombe kama kiongozi na mdau wa kisiasa watakufukuza, hata wakati mwingine wanawafukuza watalaam kwa sababu wanaona fedha nyingi zimeingia lakini hazina tija, hawapati maji jambo ambalo ni hatari sana. Kuna wizi mkubwa umefanyika lakini hakuna mtu anayefuatilia jambo hili. Naiomba Serikali ijaribu kufuatilia...
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.