Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hotuba iliyowasilishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kazi kubwa anayoifanya akishirikiana na viongozi wakuu kwa maana watendaji wakuu wa Wizara hizo pamoja na changamoto mbalimbali ambazo wanakabiliana nazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeanza na suala zima la magereza. Tumesema kwamba Serikali yetu tunataka nchi hii safari hii iwe nchi ya viwanda; ukiangalia kwenye taarifa ya Kamati imetoa ushauri kwa kuishauri Serikali kwamba tuiwezeshe magereza ili iweze kufanya kazi yake vizuri. Ninavyokumbuka, nilipokuwa nikikua, magereza wamekuwa wakilima mashamba kwa mfano yale magereza ya kilimo walikuwa wakilima mashamba na kuweza kutosheleza mazao ya chakula na ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kinachotakiwa hapa ni kurejesha ule utaratibu wa zamani ili magereza waweze kupatiwa zana za kufanyia kazi, waweze kupatiwa mtaji, kwa ajili ya uzalishaji. Magereza wakizalisha mazao ya kutosha inaweza ikapatikana malighafi ya kupeleka kwenye viwanda ambavyo tunasema tunataka tuwe na viwanda ili kusudi viweze kulishwa na malighafi itakayokuwa imezalishwa na magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii inawezekana kwa magereza kwa sababu wenzetu tayari wana rasilimali watu, tukiwawezesha magereza tukawapa mtaji wa kutosha hakuna kitakachoshindikana. Magereza zamani walikuwa wanafuga mifugo kwa maana ya ng’ombe wa maziwa. Nakumbuka nilipokuwa pale Mafinga yalikuwa yanatoka maziwa kwenye gereza la Isupilo, yanaletwa huku ukiuliza yametoka wapi, wanasema maziwa yanatoka Gereza la Isupilo. Kwa hiyo, kama tutataka kuanzisha viwanda vya maziwa, magereza hawa tukiwawezesha watafuga vizuri na viwanda hivyo vitaweza kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali yangu ili tuweze kuufufua huu uchumi tunaouzungumza wa kutaka tuwe na viwanda tuweze kuwawezesha magereza kwa kuwapa mtaji na hatimaye kuwawezesha kwa zana za kufanyia kazi ili kusudi wao wenyewe waweze kuzalisha kwa maana ya kulisha magereza yao, kuachana na kuendelea kuitegemea Serikali. Wakati huo huo ziada itapatikana kwa ajili ya kuuza na hatimaye kuweza kupata fedha ambazo zitapatikana kama sehemu ya maduhuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Kamishna Mkuu wa Magereza kule kwangu Korogwe kwenye gereza moja la Kwa Mngumi ameanza kufufua mabwawa 30 ya ufugaji wa samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabwawa yale ni makubwa na ameshaanza kupanda samaki mle ndani, lakini anachohitaji hapo kuna changamoto, nimwombe Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi aweze kutembelea lile gereza ili aende akaone yale mabwawa ambayo ameyaanzisha huyu Kamishna Mkuu wa magereza ili aweze kuona ni namna gani ambavyo anaweza kuwasaidia ili kusudi waweze kufanikisha kukamilisha ule mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kama walivyosema wenzangu suala la maslahi ya askari. Lipo tatizo pamoja na kwamba tunasema bajeti inakuwa ndogo, lakini inakuwa ndogo kwa hawa askari wa ngazi ya chini tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, askari wa ngazi ya chini wanapata shida, wanakwenda likizo bila malipo ya likizo yao, hata wakirudi kutoka likizo wakiomba fedha hizo kulipwa hawalipwi. Niiombe Serikali katika bajeti ile ambayo inatengwa kwa ajili ya Wizara hii ni vizuri tukawapa fedha zote ili kusudi waweze kulipa madeni wanayodaiwa na askari wa ngazi za chini walipwe madai yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo lingine ambalo askari wa ngazi ya chini wanapata shida, suala la upandishwaji wa vyeo, wana utaratibu wa kila baada ya miaka mitatu askari wa ngazi ya chini anatakiwa kupandishwa cheo, lakini hawapandishi kwa wakati na hata wakipandishwa hawalipwi mshahara kulingana na cheo alichopandishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana tusiwafishe moyo vijana hawa askari wa ngazi ya chini hawa mishahara yao ni midogo, wanapandishwa vyeo halafu hawalipwi kulingana na vyeo walivyopewa, wapewe kulingana na vyeo vyao walivyopewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la kufiwa, askari wa ngazi ya chini akifiwa nitaomba Waziri anipe majibu anapo-wind up hivi ni kweli kwamba akiwa na baba yake mzazi, mama yake mzazi anakaa naye pale nyumbani na tuseme bahati nzuri huyu askari yeye kwao labda ni Musoma amefiwa na baba yake alikuwa akimlea hapo nyumbani alikuwa anaugua, askari yule hawezi kusafirisha na mzazi wake yule kupelekwa nyumbani, askari yule anahangaika anatafufa fedha za kusafirisha mwili ule hivi ni kweli?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu askari si mtumishi wa Serikali inakuaje watumishi wa Serikali wengine wazazi wao wakifariki wanasafirishwa iweje askari polisi anafanyiwa kitu cha namna hiyo? Nitaomba majibu kama ni kweli, utaratibu ni huo naomba utaratibu huo ubadilishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za Polisi, wenzangu wamezungumza sana, nimefanya ziara yangu nilitembelea taasisi ikiwemo Polisi, Magereza kama walivyosema wenzangu inasikitisha. Askari wa Korogwe Mjini wana nyumba chumba kimoja na sebule, ana watoto watano, wa kike wawili, wa kiume watatu, wote wana umri mkubwa hebu niambieni sasa maadili yako wapi hapo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, nimeona hapa mnazungumzia suala zima la Serikali kupitia mkopo wa China, sasa nimwombe Waziri atakapokuja ku-wind up aniambie huu ni mkopo ambao umeshapatikana au wanakusudia kupewa hizi fedha, naomba waje waniambie. Kama mkopo huu umepatikana, niwaombe askari wa Korogwe wawemo katika mpango wa nyumba hizi 4,136. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nichukue nafasi tena kumpongeza Waziri kwa kuwasilisha taarifa yake vizuri na haya mengine ni mapito, yeye apige mwendo, mti wenye matunda mazuri siku zote huwa unapigwa mawe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.