Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia na mimi fursa angalau nitoe na mimi mchango wangu katika hii sekta muhimu ya kilimo na pia niwasemee wananchi wenzangu wa Jimbo la Singida Kaskazini ambao kwa asilimia kubwa wanategemea kilimo katika maisha yao ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kutoa pongezi na shukrani nyingi sana kwa Waziri wa Kilimo pamoja na Mheshimiwa Rais kwa kutoa angalau bajeti ya shilingi bilioni 751 kwa ajili ya kilimo. Hii ni hatua kubwa lakini hatua ya pili ni utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pia shukrani na pongezi kwa Mheshimiwa Waziri kwa hatua yake ya kufika Jimboni kwangu Singida Kaskazini. Mheshimiwa Waziri alifika katika bonde kubwa na zuri sana la umwagiliaji pale Msange, akaenda Mughamu na akatuahidi kwamba sasa tutakwenda kupona kwa kutuletea mradi mkubwa wa umwagiliaji katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, project ile tayari imeshafika hatua kubwa ya feasibility study survey na bwawa pamoja na eneo lenyewe la mradi liko tayari kwa maana ya mashamba, kikubwa sasa tunachosubiri ni fedha kwa ajili ya kuweka miundombinu ile kazi iweze kuanza. Ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri aendelee kulimulikia macho kwa karibu sana eneo lile ili kuwakomboa ndugu zako wale wa Singida Kaskazini ambao walifurahi sana siku ile ulipokuja wakaona kabisa kwamba upele sasa umepata mkunaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo na pamoja na ujio wa Mheshimiwa Waziri alienda kwenye maeneo machache sana mawili tu ya umwagiliaji katika Jimbo la Singida Kaskazini, lakini yako maeneo mengine ambayo tungependa sana afike ili aje aone na kutupa moyo aweze kuwahamasisha Wanasingida Kaskazini kwa kilimo cha umwagiliaji. Kuna maeneo kama vile Mtambuko mabwawa makubwa yana maji muda wote wa mwaka, lakini hayatumiki ipasavyo kwa ajili ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Bwawa la Masoweda, Kisisi kuna Mikuyu na Endeshi, maeneo haya ninaomba sana nimuombe Waziri pamoja na Wizara kwa ujumla wayamulike eneo la Mkoa wa Singida kwa kiwango kikubwa ni kame, lakini tumepata baraka hii ya water bodies ambazo yapo muda wote. Niombe sana maeneo haya yatazamwe ili yaweze kuwasaidia na kuwakomboa wananchi wetu ambao kwa kiwango kikubwa wanategemea kilimo, lakini kilimo chenyewe siyo cha uhakika kwa sababu wanategemea mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo niipongeze tena Wizara na hasa Mheshimiwa Waziri kwa kutuletea mbegu hizi za kisasa za alizeti. Tunaipongeza sana Serikali na ni hatua nzuri lakini kwa upande wa Mkoa wa Singida mbegu hizi hazijafanya vizuri sana kwa sababu ya mvua. Mbegu zimekuwa za bei nzuri lakini sasa mvua imetuangusha ndiyo maana nasisitiza kwenye eneo la umwagiliaji ili hizi mbegu ambazo tumepewa kutoka shilingi 35,000 kwa kilo sasa hivi ni shilingi 3,500 lakini hazijaweza kutusaidia sana kwa sababu ya kukosekana mvua ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nisisitize kwenye hizi mbegu ufanyike utafiti sasa tupate mbegu zinazohimili ukame, zinazochukua muda mfupi na zinazotoa mazao mengi ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia pembejeo zingine, tumepata mbegu nashukuru na naendelea kuomba huu mpango uendelee na uboreshwe. Lakini kwenye eneo la pembejeo ninaomba sasa tujielekeze kwenye mbolea. Mbolea hivi sasa mathalani Urea mfuko mmoja ambao ulikuwa unauzwa shilingi 60,000 leo unauzwa shilingi 110,000; DAP ambayo ilikuwa inauzwa shilingi 75,000 leo inauzwa shilingi 110,000 ni gharama kubwa sana kwa mkulima hii. Haiwezi kumsaidia na hatuwezi kuwakomboa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali iweke ruzuku kwenye mbolea na pembejeo zingine za kilimo, madawa mengine, viuatilifu lakini pia hata matrekta leo tumeona jeshi la kilimo hapa Bungeni wamepewa pikipiki, wamepewa mpaka vishikwambi, lakini mkulima anatumia jembe la mkono. Haiendani, tunataka hivi vitu viende sambamba tumboreshee mazingira mtendaji kwa maana ya mtumishi, msimamizi lakini hata mkulima naye pia tumtazame, tumboreshee mazingira yake ya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, sana, sana tuhakikishe tunaondoka kwenye jembe la mkono, jembe la asili ambalo halijatupa tija tangu tumepata Uhuru tunalima na jembe la mkono mpaka leo tunalalamika njaa, tunalalamika hatutoshelezi kwenye uzalishaji ni kwa sababu hatujawekeza ipasavyo kwa mkulima. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekuacha, lakini malizia.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, niombe sana kwenye eneo la upungufu wa watumishi hasa Maafisa Kilimo katika Jimbo langu la Singida Kaskazini tunavyo vijiji 84, kata 21 lakini tuna Maafisa Ugani na Kilimo ni 13 tu. Kwa hiyo, niombe sana vijiji vingi havina Watendaji, havina Maafisa Ugani hawa, wataalam kwa hiyo, wakulima wanajilimia hawana mwongozo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya kusema hayo, ninayo mengi na nitayawasilisha mengine kwa maandishi. Niombe sana Wizara hii next time iongezewe muda. Muda wa dakika tano hizi hatuwezi kuishauri Serikari ipasavyo, tutaishia kupitiapitia tu juu juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninashukuru sana na ninaunga mkono na ahsante sana. (Makofi)