Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika bajeti ya Kilimo, pia nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kututunuku uhai na nishukuru Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuunga mkono jitihada za Bunge la 12 ambalo limejipa agenda ya kufanya mapinduzi ya kweli ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ya Shilingi Bilioni 751 ambayo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 200 ni kiashiria kwamba Rais wetu ana imani kubwa na Bunge hili na yupo pamoja nasi na kwasababu tumejipa agenda ya kufanya mapinduzi ya kilimo basi huu ni uungwaji mkono wa aina yake, nami naomba nitumie nafasi hii kumshukuru Rais wetu kwa imani hii ambayo anatuonesha na ushirikiano ambao anatupa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangu walikuwa wanauliza kwamba ndiyo watumishi wameongezewa mshahara kwa asilimia 23.3 sisi wakulima tumepata nini? Jibu wamepata leo kwenye bajeti hii ya Wizara ya Kilimo, kwamba Serikali yetu inapeleka Bilioni 751 kwa ajili yao na fedha hizi zinaenda kuleta mabadiliko ya kweli katika uchumi wao. Ninampongeza Rais wetu na nimpongeze pia kwa suala la kuongeza mshahara kwa watumishi hasa hawa wa kilimo ambao ninaamini ongezeko la mshahara huu unaenda kuwapa incentive ya kwenda kuji-engage kikamilifu katika kufanya mapinduzi ya kilimo hasa katika maeneo ya pembezoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze na utafiti, kwenye bajeti ya kilimo Waziri wetu Profesa Mkenda alizungumza kwamba ametenga Bilioni Mbili kwa watafiti wetu ambao wanakwenda ku-publish kwenye journals za kueleweka. Kwenye tafiti za kilimo bado tupo nyuma sana na ndiyo maana mwaka jana tulitenga Bilioni Tano na mwaka huu tumetenga Bilioni Tano kwa ajili ya kuaziga viuatilifu nje. Fedha hizi kama tungekuwa tumewekeza walau Bilioni Moja au Mbili kwa ajili ya utafiti wa viuatilifu naamini kabisa tusingefikia mahali ambapo tunatenga zaidi ya Bilioni Tano kwa ajili ya kuagiza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo tunahitaji kupata mbegu bora, jana tulizungumzia kwa hisia kuhusiana na afya ya akili lakini unapozungumzia kilimo afya ya udongo ndiyo kila kitu, lakini kuna tafiti ngapi ambazo zimejikita kuangalia afya ya udogo katika maeneo mbalimbali? Hiyo ni changamoto ambayo naomba Wizara ya Kilimo ichukue kwa uzito wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katikati ya miaka ya 70 kuna nchi ndogo kule Amerika ya Kusini ilitusaidi yenyewe ikiwa katikati ya vikwazo na hali ngumu ya kiuchumi, ilitujengea shule Nne kule Kibiti, Ruvu, Ifakara na Kilosa. Shule hizi zilikuwa za kilimo na zilijengwa kama msaada wakati Serikali hiyo ikiwa katika hali ngumu sana ya kiuchumi. Shule hizi sijaona kama kuna mpango unaoeleweka katika miaka ya karibuni kurudisha hadhi yake ya kuzalisha Wataalam wa Kilimo katika elimu ya sekondari. Ninaomba Mheshimiwa Waziri wakati unafanya majumuisho ujikite katika kutuambia nini mpango wa Wizara yako kushirikiana na Wizara ya Kilimo na TAMISEMI katika kurudisha hadhi ya shule hizi za sekondari ambazo zilijikita kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo tuna kitu kinaitwa skills development levy ambayo ni asilimia Nne inatoka katika private secto,r fedha hizi lengo lake ni kujenga uwezo kwa vijana wetu, lakini sioni matumizi yake fedha hizi katika ujenzi wa skills katika vyuo vya kati. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo muangalie namna bora ya kushirikiana na Wizara ya Elimu kuangalia vyuo vyetu vya VETA kuzalisha wataalam wa kati kwenye kada ya kilimo, pamoja na kuimarisha vyuo vyetu vya kilimo kwenye tafiti na vitu vingine. Kubwa kuliko yote ni taasisi zetu za TARI na ASA hali yake ni ngumu na kwasababu tunaagiza mbegu kwa kiasi kikubwa tunao wajibu wa moja kwa moja kuziwezesha taasisi katika hizi ku-develop ama kufanya tafiti za mbegu ili tupunguze utegemezi wa mbegu kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna jambo ambalo tumejifunza kwenye vita hii ya Ukraine ni kwamba kujitegemea ni muhimu hasa katika sekta ya kilimo pia kama kuna jambo ambalo tumejifunza hawa watu ndiyo wazalishaji wakubwa wa mafuta na ngano. Sasa Serikali tumejipanga vipi kutumia fursa hii, kwasababu kule kuna wawekezaji ambao uzalishaji wao umekuwa destructed na hii vita. Tuwakaribishe kama wawekezaji huku, wanayo knowledge, wanazo skills na wanayo mitaji. Tumejipanga vipi kuhakikisha kwamba kwa sababu soko la Ulaya katika maeneo hayo limevurugika, tuwavutie huku waje ku-boost sekta ya kilimo katika maeneo yetu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo wakati nikiwa mdogo pale Halmashauri ya Mji wa Morogoro magari yote yalikuwa yanaandikwa Ofisi ya Mkurugenzi except gari moja tu ambalo lilikuwa linabeba takataka lile halikuandikwa kabisa, halina maandishi yoyote ambayo yanaeleza gari linamilikiwa na nani. Waswahili wanasema ukitaka kumuua mbwa mpe jina baya ukimwita queen au prince huwezi kumuua, ukimuita snake ama cobra utamuua tu bila shaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika sekta ya mbogamboga ambayo ni maarufu wanaita mali kuoza, sekta hii ni muhimu sana kwasababu imeajiri vijana wengi, akina mama wengi lakini haipewi msukumo. Ndio maana unasikia bodi ya Mkonge, Bodi ya Kahawa lakini huwezi kusikia Bodi ya Mbogamboga, Bodi ya Matunda, huwezi kusikia kwa sababu imeshaitwa mali kuoza, lakini hilo ndilo eneo ambalo linaajiri vijana wetu wengi, katika mazao ambayo tunasafirisha sana nje ni mbogamboga na matunda, lakini huwezi kuona msukumo wa dhahiri ambao umejikita katika kuonesha kwamba tunaenda kuchukulia sekta hii katika uzito wake.

Hilo ndiyo eneo ambalo linaajiri vijana wetu wengi na katika mazao ambayo tunasafirisha sana nje ni mbogamboga na matunda, lakini huwezi kuona msukumo wa dhahiri ambao umejikita katika kuonyesha kwamba tunaenda kuzichukulia sekta hii katika uzito wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana TAHA kwa sababu imelibeba sana zao la matunda na mbogamboga lakini pamoja na yote hayo, tunahitaji Serikali kuwezesha sekta hizi hasa kwa kuondoa kodi kwenye cold storage na facilities ili mkulima mdogo aweze kuhifadhi matunda yake ambayo yanaitwa mali kuoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, bajeti yetu inapaswa kujikita sana katika umwagiliaji. Tuna hekta zaidi ya milioni 29 ambazo zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini mpaka sasa eneo ambalo tunamwagilia ni ekari 727,280 sawa na asilimia 2.5. Huu ni utani, huu ni mzaha. Katika nchi ambayo tumejizatiti katika kuleta mapinduzi ya kilimo, hatuwezi tukawa na hekta zaidi ya milioni 29 ambazo zinafaa kwa umwagaliaji, tunaenda kukomea kwenye hekta 700,000 ambayo ni asilimia 2.5. Lazima tuonyeshe seriousness kwenye hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anapofanya majumuisho atuambie nini mpango mkakati wa Serikali yetu katika kuhakikisha kwamba tunaenda kuboresha kilimo chetu hasa katika eneo la umwagiliaji? Katika hili napendekeza kuangalia nafuu ya kodi kwenye pampu ndogo ndogo kuwawezesha wakulima wetu katika maeneo ya vijijini kwa ajili ya kulima, lakini pia kutoa nafuu ya kodi kwenye mitambo ya kuchimba visima pamoja na uchimbaji wa mabwawa. Ukiweka kodi pale unaweza ukapunguza thamani kwa kutoa asilimia 30 mpaka 40, na hii inaweza ikaboresha suala zima la utengenezaji wa miundombinu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, uvunaji wa maji ya mvua. Tunatumia fedha nyingi kuboresha barabara zetu na miundombinu yetu, vile vile fedha ambazo tunatumia kukarabati miundombinu ambayo imeondolewa na mafuriko zinaweza zikawa nyingi ukilinganisha na fedha ambazo tungewekeza kujenga mabwawa ya kuvunia maji kwa ajili ya kulinda miundombinu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka Dar es Salaam mpaka hapa, utakuta mashimo mengi sana kwenye SGR. Yale mashimo yanafaa kutengeneza mabwawa ambayo yanaweza yakatunza maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, naomba kutoa rai kwa Wizara ya Kilimo kuyaangalia mabwawa haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.