Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa nami niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kwanza kabisa kabla sijachangia nitoe masikitiko yangu kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano ambayo kwa kweli inajisifu kwamba ni Serikali ya Hapa Kazi Tu. Imezuia television isionyeshwe lakini yet tuko ndani tumejifungia sisi wenyewe, bado mnazuia taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani isisomwe. Inaonesha ni jinsi gani hamjiamini, hamjajipanga na hamjajua ni nini mnataka mlifanyie Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi; kuna mambo makuu mengi sana ya kuyazungumzia na kwa sababu ni dakika kumi, naomba nianze na Jeshi la Magereza. Ni dhahiri kwamba kwenye Jeshi letu la Magereza sheria ambazo zinatumika sasa hivi ni zile ambazo zilikuwa zikitumika wakati wa ukoloni; ni sheria ambazo zimepitwa na wakati. Leo unaweza ukakuta Askari Magereza kwa bahati mbaya, mahabusu au mfungwa ametoroka, atapewa adhabu labda ndani ya miaka mitatu tuseme, ambayo adhabu moja ya mfungwa kutoroka anatakiwa akatwe mshahara wake, nusu ya mshahara au robo ya mshahara, anatakiwa ashushwe cheo, anatakiwa asiende masomoni kujiendeleza na hata ikitokea huyo aliyekimbia amekamtwa, bado huyu Askari Magereza atatakiwa atumikie hiyo adhabu kwa miaka yote ambayo amepangiwa. Hii ni dhuluma na haikubaliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo mzima wa uendeshaji wa Jeshi la Magereza kiukweli unatakiwa ufumuliwe upya. Tunahitaji kufumuliwa upya kama walivyofanya kwenye idara nyingine. Kuna malalamiko mengi sana ambayo yamekuwa yakiendelea. Hata bila kufumba macho, ni dhahiri kwamba Commissioner General wa Prison amekuwa akilalamikiwa sana. Naomba kabisa mchunguze hayo malalamiko ambayo yako dhidi yake, myafanyie kazi. Kwa sababu tumekuwa tukizungumza, mnapuuzia, baada ya muda ukija kuchunguzwa, ripoti ya CAG inatoa yale ambayo tunayalalamikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi wote wa Umma tumekuwa tukijaza hizi fomu za maadili, mwachunguze mali wanazomiliki, mishahara wanayopewa ina-reflect uhalisia wa mali ambazo wanamiliki? Kuna ufisadi mkubwa sana ambao unaendelea kwa Viongozi Wakuu wa haya Majeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, makazi ya Askari ni duni sana. Mwaka 2015 wakati wa bajeti nilizungumza hapa na mkasema kwamba mlikuwa mmetenga kujenga zaidi ya makazi 9,000. Leo tunavyozungumza, Waziri umekuja unatuambia mnajenga makazi 4,000. Tunapenda kujua yale ya mwaka 2015, hayo makazi 9,000, yamejengwa kwa kiasi kipi? Leo ninavyozungumza, kule Tarime Askari Magereza makazi wanayoishi hata ukienda kumweka sungura, atalalamika kwa nini anaishi kwenye ile nyumba. Leo unamweka binadamu, tena Maaskari Magereza ambao wana familia, kinyumba ambacho kilijengwa mwaka 1942, enzi za ukoloni mpaka leo hujaboresha na zaidi kipindi hicho walikuwa wakikaa Askari Magereza wachache, leo wanakaa wengi kwenye kijumba hicho kimoja, wana familia na mnajua kuna mambo mengine ya staha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unakuta saa nyingine Askari Magereza wanawajibika kujijengea wenyewe vijumba. Tunaomba mnapokuwa mnasema nyumba 4,000, basi wajalini wale ndugu zetu ambao wanafanya kazi kwenye mazingira magumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Serikali hii ya Hapa Kazi Tu inakwepa kuzungumzia Lugumi ya Jeshi la Polisi, lakini inasemekana kuna Lugumi nyingine kwenye Jeshi la Magereza. Inasemekana kwamba kuna fedha zilitolewa kwa ajili ya mfumo wa utambuzi wa ndugu zetu ambao wapo Magereza; wafungwa na mahabusu, wanaojulikana kama OMS (Offender Management System), ilitolewa ili hizi system ziweze kufungwa kwenye Magereza yote nchini, lakini inasemekana hadi leo hakuna system ambayo imefungwa kwenye hayo Magereza. Nataka kujua kama ni kweli, hizo fedha zimekwenda wapi? Au hii ndiyo ile dhana ya kuendeleza Lugumi ndani ya Jeshi la Polisi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, inasemekana pia kuna fedha zilitolewa kwa ajili ya kununua magari ndani ya Jeshi la Magereza ya kuwabeba mahabusu kutoka Gerezani kwenda Mahakamani na pia wale ambao unakuta wana-escort. Mheshimiwa Waziri amesema hapa kwamba watajitahidi kutenga fedha na kuna baadhi ya wilaya mmenunua, lakini inasemekana kwamba kuna fedha zilitengwa. Sasa nataka nijue, kama hizo fedha zilitengwa na mzabuni alikuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, zimeweza kununua hayo magari mangapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli zilitolewa, maana yake inasemekana zilitengeneza magari mabovu ambayo sasa hivi hayafanyi kazi na tunaendelea kuona kwamba Askari Polisi ndio wanasindikiza watu kwenda Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho ni cha fedheha, ni uniform. Uniform mara ya mwisho kutolewa kwa hawa Maaskari Magereza, ambao nimefanya nao mazungumzo, ilikuwa ni 2009, mpaka leo hamjaweza kuwapa uniform.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hawa Maaskari Magereza, labda hata na wa Jeshi la Polisi, ukiwatazama na wengine wamekuja hapa Bungeni, wana uniform tofauti. Viatu vyao vinatofautiana, maana yake wanajinunulia, uniform zao ziko tofauti. Halafu Serikali ambayo inawatumia hawa ndugu zetu, tena vilivyo katika kuwakandamiza wapinzani, mnashindwa hata kuhakikisha kwamba mnawastahi na mavazi yao, angalau waonekane ni watanashati, mnawadhalilisha! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza, kama mmeshindwa kuleta uniform kwa hawa Askari, kwenye mshahara wao waongezeeni fedha za posho ya kununua uniform zao ambazo wataweza kununua uniform zenye kiwango cha juu. Maana inasemekana kuna mtu mmempa tenda ya ku-supply uniform; na ni mke wa kigogo wa Jeshi la Magereza. Anafanya kazi BOT, uniform zenyewe anazoleta ni za kiwango cha chini, yet hawa Maaskari wetu wanakwenda kununua vile vitambaa, wakifua siku mbili havina kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza bado, hii Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba chombo hiki muhimu kwa mustakabali wa maisha ya Watanzania inawaboreshea makazi yao? Inawapa mazingira mazuri ya kufanya kazi? Siyo tu mnawatumia halafu mnawaacha wanaishi kama watumwa kwenye nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni ucheleweshaji wa malipo; mafao ya Askari wastaafu na Mheshimiwa Waziri nimekupa copy. Kuna baba, ni Askari mstaafu sasa hivi ana miaka 70, tena bila huruma, ametumikia Jeshi kwa zaidi ya miaka 32; kuanzia mwaka 1962 mpaka 1995, anaitwa Simon Mirumbe. Amekuwa akihangaikia mafao yake kuanzia 1995 mpaka leo 2016, mnamzungusha tu. Mmemtumia lakini mnashindwa kumpa mafao yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike wakati Serikali ya Chama cha Mapinduzi itambue umuhimu wa Jeshi hili la Polisi, msiwatumie tu, bali muwajali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni msongamano wa mahabusu kwenye Magereza yetu. Leo ukienda Tarime, lile Gereza limejengwa 1942, uwezo wake ulikuwa ni kubeba wafungwa na mahabusu 209, lakini kuna siku unakuta wapo zaidi ya 500 mle ndani. Miundombinu ni mibovu, choo hakitamaniki, watu wanabanana, magodoro yenyewe ni aah! Tumekuwa tukishauri humu ndani; kuna kesi nyingine hazihitaji hata kumpeleka mtu kwenye Gereza, lakini unakuta mnalundika. Leo ukienda Tarime, kufuatia uchaguzi wa Oktoba, kuna kesi za kisiasa watu wako mle zaidi ya mia, wakati mnajua kabisa ile ni hatarishi kwa afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, nataka kujua; na Mheshimiwa Ummy kama angekuwepo; unakuta mwanamke labda amekamatwa kwa bahati mbaya akiwa mjamzito, anapelekwa mahabusu Gerezani, inatokea anajifungua, yule mtoto aliyezaliwa naye anakuwa ni mfungwa au mahabusu kwenye lile Gereza. Nataka nijue Serikali mnajipanga vipi angalau miezi sita huyu mama muweze kum-excuse atoke Gerezani, aweze kumzaa mtoto wake ili mtoto asiathirike kwa yale… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Aah, mmenibania eeh! (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante.