Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara nyeti ya Kilimo na pia nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kabisa naungana na wote waliotoa sifa nyingi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Wizara nzima kwa kazi kubwa wanayoifanya. Bahati nzuri mimi Mheshimiwa Hussein Bashe namfahamu kabla hajawa Mbunge, kabla hajawa Waziri na namfahamu jinsi alivyo mahiri kwa jambo lolote ambalo anakusudia kulisimamia. Kwa hiyo naendelea kuwatia moyo ili kazi iweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya yote tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameona umuhimu mkubwa wa kuongeza nguvu kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo. Ukurasa wa 71 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia kilimo cha umwagiliaji na ukiangalia bajeti nzima hii kuna mambo matatu ambayo naweza nikasema yamepewa nguvu kubwa sana kwenye bajeti hii. Kwanza, ni kilimo cha umwagiliaji; Pili, ni mkakati wa kupambana na tatizo la upungufu wa mafuta nchini kwa kuongeza nguvu katika kutoa mbegu, na Tatu ni kuongeza nguvu katika huduma za ugani yaani kwa kuwaongezea nguvu wataalam kwenye masuala ya utafiti na masuala ya kuwawezesha wataalam. Napongeza sana hatua hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye ukurasa huu amezungumzia mradi wa umwagiliaji wa Bonde la Mto Luiche lililoko katika Jimbo langu la Kigoma Mjini. Huu mradi umeshafanyiwa upembuzi yakinifu kwa asilimia 100 na sasa unakwenda kwenye hatua ya utekelezaji. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, wananchi wangu wamekaa kwa muda mrefu tangu waliposikia mradi huu umepata ufadhili kutoka Kuwait Fund, wanasubiri kwa muda mrefu lakini wanaona kama unasuasua. Nimwombe kama alivyoahidi kuhakikisha kwamba mwakani hatua zote zinakamilika na mradi ule unapata mkandarasi. Mradi huu utakwenda kunufaisha wananchi wa maeneo ya Mgumile, Totwe, Nyaruboza, Kabogo, Kangona na Kafumbatwa. Hawa wananchi wote wa maeneo haya wanasubiri kwa hamu siku nyingi mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nilizungumzie ni kilimo cha michikichi. Tuna upungufu wa tani kama 400,000 za mafuta ambazo tunataka tuzizalishe humu nchini. Eneo moja ambalo Serikali imelenga la kuzalisha ni kwenye kilimo cha michikichi na kilimo cha michikichi asili yake hasa ni Kigoma, hata hao ma-giant wa kuzalisha michikichi huko Malyasia tunaambiwa mbegu wameitoa Kigoma. Sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri, Waziri Mkuu ameweka juhudi kubwa sana kwa niaba ya Serikali, amekuwa akifuatilia sana, lakini kilimo hiki cha kuwapa wananchi miche ya kulima heka moja au heka mbili hakiwezi kututoa hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, Serikali lazima iwekeze katika jambo hili ili kuokoa pesa za kigeni tunazozitoa kwa ajii ya mafuta. Imewekeza katika mbegu tunashukuru na watu wa TARI wamefanya kazi nzuri ya utafiti wa mbegu na watu wa ASA wamefanyakazi nzuri sana nawapongeza ya kuzalisha mbegu. Hata hivyo, nasema twende mbele zaidi, tufike mahali tuwakopeshe wananchi, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza ilikuwa imeanza mpango mzuri kabisa, inasema inaandaa maeneo, inapanda miche kama ni heka tano au heka kumi, halafu inamkabidhi mwananchi kuendeleza lakini alipie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali iamue kwa makusudi kabisa kuingia katika kilimo kikubwa kitakachotutoa kwenye tatizo hili. wananchi wale wakikopeshwa, wakaandaliwa mashamba, wakakabidhiwa wayatunze, naamini kabisa tutatoka kwenye tatizo la mafuta tulilonalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla niseme, juhudi za Wizara wananchi wanazikubali, lakini tukiongeza kasi hapo tutalitoa Taifa letu katika matatizo ya mafuta, Kigoma peke yake inaweza ikakidhi mahitaji ya mafuta haya iwapo michikichi itapandwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)