Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia kwenye sekta hii ya Wizara ya Kilimo. Kwanza kabisa naunga Taarifa yote ya Kamati ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa mambo yote anayoyafanya. Na tatu, nataka kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Hussein Bashe, pamoja na Naibu Waziri, Makatibu wote pamoja na wafanyakazi wote wa sekta ya Wizara ya Kilimo. Pia, bila kuwasahau kamati yangu nzima, wajumbe wote wa Kamati ya Kilimo kwa kazi nzuri waliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuwapongeza wakulima wote wa Tanzania kwa kazi wanayoifanya ya kutupatia chakula tunachokula kila siku. Kwa kusema hayo ninasema kuwa maendeleo ya uchumi tukubali kuwa yanatokana na sekta za uzalishaji ikiwemo sekta ya kilimo. Kwa pamoja tukishikamana na kilimo tukakipa kipaumbele namba moja naamini umasikini utapungua kama hautakwisha kwa watu wote hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa bajeti. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kukiona kilimo na kukipa kipaumbele kwa kuwaongezea Wizara fedha kutoka bilioni 274 mpaka bilioni 751. Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana kwa kuliona hili na Mwenyezi Mungu azidi kukubariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhumuni ya Kamati na madhumuni ya Serikali, hasa Wizara ni kukibadilisha kilimo kikawa kilimo cha mageuzi chenye tija na chenye biashara. Kilimo ni ajira, kinaleta chakula, ni lishe. Kilimo ni kila kitu. Huwezi kukaa bila ya kula ukadhani kuwa utaishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kusema mambo muhimu yanayopaswa kufanyika kwenye kilimo, nikianza na utafiti. Mheshimiwa Waziri naomba; hela zimetengwa za utafiti, Waziri mmepewa hela nyingi, hizo hela kuna vituo mbalimbali vya utafiti ambavyo tunaviita TARI pamoja na vyuo vingine vikuu kikiwepo Chuo Kikuu cha Sokoine na pia Chuo Kikuu cha Nelson Mandela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa TARI ihakikishwe kuwa ni fedha kiasi gani inapelekwa kwenye kila kituo cha utafiti. Tafiti mbalimbali zimefanyika, na tafiti hizo ziwwafikie wakulima. Kuna tafiti rafiki ambazo ziko kwenye kituo cha Kibaha ambako wanafanya tafiti za biological control ambazo bado hazijawafikia wananchi. ninaomba hizo ziweze kuwafikia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaweza kuongea ni kwenye huduma za ugani. Huduma za ugani nakuhakikishia haiajawahi kutokea. Maafisa Ugani walikuwa hapa, naamini wengine bado wako hap ana wengine wananisikia. Ninachokiomba maafisa ugani fanyeni kazi. Mmepewa vitendeakazi, mmepewa pikipiki, kila mmoja atapata pikipiki yake, pikipiki 7,000 zimetolewa, visikwambi vimetolewa, extension kit imetolewa, pia mmepewa na vi-sample vya kufanyia sampling na ubora wa udongo kila Halmashauri. Kwa hiyo, nawaomba ninyi maafisa ugani fanyeni kazi tuweze kuona matokeo ya kilimo, kilimo kiweze kubadilika na kilimo kiweze kuwa cha tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa huduma za ugani ni mambo mengi yametolewa haijawahi kutokea, hawajawahi kupata vifaa kama hivyo. Kwa hiyo, waweze kuwafikia wakulima, siyo kukaa nyumbani bila kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni umwagiliaji. Wewe mwenyewe ni shahidi, watu wote ni mashahidi. Mnaona kuwa kwa upande wa tabia-nchi hasa kwa sasahivi, kama ninavyosema, unaona kuwa hakuna mvua, lakini kusema ukweli watu wengi wamelima na haya mazao ya mafuta ya alizeti mnayoyasema pamoja na mawese yamelimwa, lakini ni ukame. Dawa yenyewe ni umwagiliaji, lakini kusema ukweli mpaka sasahivi sehemu tunayoimwagilia ni sehemu ndogo. Sehemu inayofaa kumwagiliwa ni kubwa ambayo sasa hivi tunamwagilia asilimia 2.5 tu ndiyo inayomwagiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hamjui hela zimeongezwa za umwagiliaji, lakini ni asilimia 2.5 tu ndiyo inayomwagiliwa. Naamini kuwa mmejikita kweli, pesa zimetolewa, kwahiyo simamieni umwagiliaji. Ili tufanikishe kilimo chetu lazima umwagiliaji upewe kipaumbele kwa hiyo, angalieni umwagiliaji kusudi tuweze kumwagilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye mbegu. Kwenye mbegu, mbegu zinazalishwa na mbegu zinazalishwa na ASA…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Ishengoma, mda wako naona kama umeisha.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kidogo. Niongezee dakika moja. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, haya nakuongeza dakika moja basi ili uweze kumalizia. (Makofi)

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa upande wa mbegu, uzalishaji wa mbegu ambao unafanya kusambazwa na ASA, na hasa sanasana tumeona wamesambaza mbegu za alizeti pamoja na mbegu za mahindi. Naomba wakulima tutumie hizi mvua chache ambazo zitakuwa zinanyesha, lakini sanasana kumkomboa mkulima ni kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana tena sana tuzingatie kilimo, kwa pamoja naamini tutatok. Hakuna kitu chochote kitatutoa kwenye umasikini bila ya kuangalia kilimo. Kwa hiyo, kilimo kipewe kipaumbele kusudi kiweze kututoa na sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siachi kuongelea Morogoro. Kwenye mabonde mengine ya Morogoro, mkoa ambao unazalisha chakula kwa wingi, yapewe kipaumbele. Ingawaje Serikali naiona kwenye umwagiliaji, lakini kwenye mabonde yote ambayo yako Mkoa wa Morogoro yaweze kuzalisha kwa wingi yaweze kuulisha Mkoa wetu wa Morogoro pamoja na mikoa mingine Tanzania kwa ujumla nan chi nyingine zinazofuata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaunga mkono hoja, ahsante sana nawashukuru. (Makofi)