Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha mchana huu kusimama ndani ya Bunge lako hili Tukufu ili kujadilia bajeti hii ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitatoa shukrani kwa hawa wafuatao. Naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya wizara hii, Naibu wake, Katibu Mkuu, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na watumishi wote wa Wizara ya Kilimo ambao kwa njia moja au nyingine wameshiriki katika maandalizi ya bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Jimbo la Nanyumbu, jimbo ambalo ndilo ambalo linazalisha sana korosho, tunazalisha sana ufuta na tumeanza kujikita katika kilimo cha alizeti. Sasa kwa leo naomba nijielekeze kilimo cha korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitamshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan ambaye kwa miaka miwili mfululizo ameweza kutupatia pembejeo bure. Hili jambo kwakweli nila kushukuru sana, kwa sababu moja ya changamoto ya wakulima ni upatikanaji wa pembejeo; lakini si pembejeo bure kwa mara ya kwanza pembejeo zimefika kwa wakati ndani ya wilaya yetu. Hili ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tarehe 17 mwezi wa tano, Mkuu wetu wa Mkoa, ndugu yangu Kaguti amekuwa akishikiri katika kuhakikisha pembejeo zinasambazwa kwenda katika wilaya zetu. Kwa hiyo, mimi natoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Waziri na uongozi mzima wa mkoa kwa jitihada wanazofanya katika kuhakikisha kwamba kilimo chetu cha korosho kinakwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewahi kuzungumza ndani ya Bunge lako kwamba pembejeo peke yake haitoshi, wananchi wetu wanahitaji fedha kwaajili ya palizi, kupulizia mikorosho, kuokota korosho na hatimaye kukusanya hizo korosho na kuzirudisha nyumbani. Lakini, wananchi hawana fedha. Kwa hiyo, tunatarajia benki zetu zi-support nguvu za wananchi, na nguvu za mama yetu. Hata hivyo, benki zetu zinatuangusha. Tarehe 28 mwezi wa nne MAMCU walifanya Mkutano Mkuu pale Masasi na Benki zote zilikuja pale, Mkuu wa Mkoa aliwaita akawahimiza kutoa mikopo kwa vyama vya msingi. Mimi nina vyama 37, lakini mpaka nianvyozungumza hakuna hata chama kimoja kimepata mkopo kwaajili ya zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakata kuinua zao la korosho, tutainuaje zao la korosho kama hatuwapatii mikopo wakulima wetu? Juzi hapa nimemsikia Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu Mkenda, anasema Benki ya NMB imetoa bilioni mbili kwaajili ya mikopo kwa vijana wetu. Sasa, sasa hizi benki zinashindwaje kutoa mikopo kwa wakulima ili waweze kuinua zao letu la korosho? Kwa hiyo, ninakuomba sana kesho Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa anieleze na anishawishi; ni jitihada gani amezichukua kuzishawishi hizi benki ili ziweze kuwakopesha wakulima wetu; vinginevyo tunatwanga maji kwenye kinu. Hatuwezi kuinua zao la korosho kwa kutumia nguvu ya mwananchi kupata msaada kutoka kwenye benki zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu uadilifu kwa wataalamu wetu, hasa wafanyakazi wa ushirika. Tunawafanyakazi ambao si waadilifu, Ndani ya Jimbo langu msimu huu uliopita zaidi ya shilingi milioni 60 hazikuweza kulipwa kwa wakulima na chanzo kikubwa ni watumishi wa Idara ile ya Ushirika. Jambo hili Mheshimiwa Waziri analifahamu sana, kwamba tunao watumishi pale si ambao si waadilifu lakini wanaachiwa. Tunakuja kuwaeleza jamani huyu mtumishi si mwadilifu lakini wanasema huyu ndiye anafanya kazi. Sasa, kama anafanya kazi basi mumchukue nyinyi kwa sababu kule kwa wananchi amesababisha matatizo makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hakuna kitu ambacho kinaudhi kama mkulima amelima korosho, amepeleka godown halafu asipate fedha. Halafu mfanyakazi wa ushirika ambaye ndiye Internal Auditor katika AMCOS anasema kwamba AMCOS zote hazina matatizo, lakini kumbe kuna matatizo kibao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri, hawa watumishi ambao tunakuja kukuletea malalamiko uchukue hatua immediately. Haiwezekani wakulima wanapata tabu, na tukienda sisi Wabunge tunalalamikiwa kama vile sisi ndio tumesababisha matatizo hayo kumbe ni watumishi wenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ninayoiona kwa hawa wafanyakazi wa ushirika wanawatu wawili wanaowajibika kwao kuna Mkurugenzi wa Halmashauri halafu kuna Mrajisi wa Vyama. Sasa naomba sana Serikali iamue hawa watumishi wapelekwe eneo moja. Na mimi ningeomba hawa watumishi wa ushirika wote waende kwa Mrajisi ili waweze kuwajibika moja kwa moja; vinginevyo wale watumishi kule wanakuwa kama miungu watu. Wao badala ya kuvisimamia hizi AMCOS wao ndiyo wanakuwa wenye AMCOS. Wananchi ambao ndio wenye AMCOS wanaweka pembeni wao ndio wanakuwa miungu watu. Sasa hili jambo kweli halikubaliki, hatukubali kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kesho Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aeleze ni jitihada gani amezifanya kwa hawa watumishi ambao wamesababisha hasara kubwa ndani ya wilaya yangu, wamesababisha kadhia kubwa ndani ya wilaya yangu na bado wapo ndani ya wilaya yangu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache naomba kuunga mkono hoja, nategemea majibu mazuri sana kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kesho. Ahsante sana. (Makofi)