Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyoko mezani ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kwa ajili ya Taifa letu na katika kila hatua anayoendanayo katika muda wa uongozi wake amekuwa akiwaletea matumaini makubwa Watanzania. Ushahidi mkubwa ni huu wa juzi tu pale alipoamua kusikiliza cha wafanyakazi na kuweza kupandisha mishahara kwa asilimia 23. 3, ambayo ni kubwa sana nchi, zote za Afrika hazijafanya hivyo, ni Tanzania peke yake. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. Tumepokea hotuba yake, tumepokea mipango ya Wizara yake. Kwa hakika Mheshimiwa Bashe unatuheshimisha sana kama Taifa, unafanya kazi nzuri sana. Kama kijana wa Kitanzania unaonekana wazi wazi wewe ni mzalendo wa kweli, na kwa hakika Mheshimiwa Rais hakukukosea na kukuweka kwenye Wizara hii. Hongera sana, tunaomba tukuhakishie kwamba Wabunge tutaendelea kukuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa ndugu yangu Mheshimiwa Antony Mavunde, Naibu Waziri, nawe unafanya vizuri, unamsaidia sana Mheshimiwa Waziri na timu yenu ni timu ambayo inaonekana wazi kwamba inaenda kufunga magoli ambayo ni magoli ya kukiboresha kilimo cha Tanzania. Nimpongeze sana Katibu Mkuu kaka yangu Massawe Pamoja na Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa namna mlivyojipanga vizuri katika kukileta kilimo kiwe ni kilimo cha manufaa kwa ajili ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo nimefurahi kuona kwamba hata bajeti, kama ambavyo nimepongeza Mheshimiwa Rais, ni utashi wa hali ya juu sana kwamba kutoka bajeti ya bilioni 234 kwenda mpaka bilioni 751 si jambo dogo. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, lakini hii ni mipango ambayo Wizara ikiongozwa na Waziri wameweza kumpelekea maoni na mapendekezo yao. Nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri, huu mwendo mzuri. Wabunge tumekuwa tukilalamika hapa kwamba bajeti ni ndogo, lakini kwa bajeti hii, ingawa ni ndogo lakini inaweza kuwa nafasi nzuri ya kuanzia katika kuboresha kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nitakuwa na maeneo machache kuchangia leo. Nitachangia leo, nitachangia kuhusiana na kilimo cha umwagiliaji, suala la mbegu na nitamalizia ushirika kama muda utanitosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa eneo la umwagiliaji. Nimefurahi sana kwamba katika bajeti hii tunayoenda kuiangalia hapa tumeona ambavyo tumevuka vizuri. Bilioni 51 zitaenda kuleta mapinduzi makubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu nilikuwa naomba, kama ambavyo ulishasema huko nyuma, kwamba tutajitahidi kuhakikisha kwamba Tume ya Umwagiliaji inakwenda kwenye halmashauri zetu. Kule ndiko kwenye mahitaji, na nivizuri wakiwa Jirani kwa sababu wataweza kusimamia kwa karibu sana. Ni kweli kwamba tumekuwa na maafisa kilimo lakini yeye ana-deal na mambo ya ugani na mambo mengine, lakini suala la umwagiliaji ni component inayoonekana kama Wizara ya maji hivi. Lakini kwa sababu Tume ya Umwagiliaji iko mezani kwako ukiweza kuweka wawakilishi ambao watakuwepo muda wote, wanaamka na kulala pale pale, watasaidia sana kuhuisha kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niseme tu, kwa bajeti ambayo tumeiona hapa tukijipanga vizuri tunaweza tukaibadilisha sana kilimo chetu kwa sababu kilimo cha kutegemea mvua kwa kweli tumeona kimekuwa hakina tija tena. Ninyi wenyewe ni mashahidi, mwaka huu tulijitahidi kupeleka mbegu, na nipongeze sana kwenye eneo hili; mmepeleka mbegu za kutosha mfano za alizeti kule Singida Mkoa wa Dodoma pamoja na Mkoa wa Simiyu, lakini mvua zimekuwa chache; maana yake jitihada zetu zimekwenda kugonga mwamba. Lakini tungekuwa na maji ya kutosha, tungekuwa na skimu za umwagiliaji wa kutosha leo hii ile mbegu ambayo tumeipanda kule isingepotea, maana kuna baadhi ya maeneo hakuna tena matumaini ya kuvuna alizeti ambayo tumeipanda kwa bei nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee kabisa kwangu mimi kwenye eneo la kwangu pale Jimbo la Singida Mashariki niliongelea Habari ya skimu ya umwagiliaji wa Mang’onyi. Nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwamba mmekubali kunipelekea milioni 700 ambayo itaenda kuisaidia sana skimu ile ili ianze kufanya kazi. Wananchi wa Mang’onyi wanatusubiri kwa hamu. Lakini kama haitoshi kwenye ule mgodi wa madini ambao unaenda kufunguliwa hivi karibuni wako tayari kununua mboga mboga kutoka kwenye mashamba ya wakulima wale. Maana yake ni kwamba, soko litakuwepo na hiyo skimu italipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama haitoshi niombe sana tuongeze suala mabwawa katika maeneo mbalimbali katika jimbo langu, tukiweza kuweka mabwawa yatawasaidia wakulima kuendelea kufanya kilimo cha umwagiliaji. Naomba, kama Kata za Mkiwa, Kikio, Isuna, Mang’onyi, Misuwaha paoja na Ndung’unyi tukipata mabwawa yatatusaidia sana kuboresha kilimo chetu ambacho ni kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mbegu ni roho ya kilimo. Tukiwa na mbegu nzuri zitasaidia kuleta mazao mengi, uzalishaji wa mazao ukiwa mwingi maana yake hata mnyororo wa thamani utakuwa umepatikana. Kwa kwa hiyo niombe sana; kuna suala ambalo tumelizungumza hapo nyuma, tuwe na mbegu zetu za asili na tuzilinde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anajua namna ambavyo GMO tumekuwa tukitumia sasa hivi; lakini kuna mahali ambapo tukitegemea tutakuwa ni watumwa wa mbegu za nje siku moja tutajikuta hatuna mbegu zetu, na hivyo hatutakuwa salama. Hata hivyo tunao wenzetu wa ASA ambao ndiyo wakala wa mbegu nchini...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa; hitimisha hoja yako basi, naona muda wako umekwisha.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: …Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ninaomba sana mbegu zipewe kipaumbele ili ziwasaidie wakulima kupata tija na ninaamini kabisa uzalishaji utaongezeka na lengo la wizara itatimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.