Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii. Napenda kuanza kwa kumshukuru kwa dhati kabisa Mheshimiwa Waziri na Wizara ya Kilimo kwa kutambua umuhimu wa lishe. Kwa mara ya kwanza kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo jambo la lishe limetambuliwa na limetajwa kwa kina. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo, hivi karibuni Wizara ya Kilimo imezindua Kampeni ya Kitaifa ya Lishe na huo ni mwendelezo wa kutekeleza ahadi ya Ilani ya Chama vha Mapinduzi ambapo jukumu la kutokomeza masuala ya udumavu na aina zote za utapiamlo yamewekwa chini ya Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana pia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka uzito mkubwa katika suala zima la tafiti na uzalishaji wa mbegu ili kuongeza tija ya kilimo. Nami mchango wangu kwa siku ya leo utajikita katika eneo la mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri wa Kilimo amesema, “hivi sasa tunazalisha mbegu kwa asilimia 26 tu ya mahitaji yetu.” Kwa maana hiyo, bado uzalishaji wa mbegu uko chini na hatujitoshelezi. Kwa hiyo, lazima tuweke jitihada za makusudi kabisa ili kuongeza uzalishaji wa mbegu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake ameelezea mipango ya kina ya Serikali katika kufanya tafiti na pia kuimarisha mbegu za msingi pamoja na mbegu za awali. Naomba nitumie fursa hii kuikumbusha Wizara Kilimo, hatuwezi kuongeza tija ya mbegu zetu kama hatukuwa tunajumuisha mbegu za asili. Kwa mantiki hiyo, namshukuru pia Mheshimiwa Waziri ametoa ahadi hapa kwamba ifikapo 2025 mbegu za asili zitakuwa zinauzwa madukani kama ilivyo mbegu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tufikie hapo, yapo mambo ya msingi lazima yaanze kufanyika hivi sasa. Kwa hiyo, napenda kupendekeza mambo manne yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, tukija kwenye suala la kiusalama, tumeona vita ya Ukraine na Urusi, jinsi ambavyo nchi inaweza ikaamua kutokuuzia kile ambacho inazalisha. Kwa hiyo, nasi tukiendelea kutegemea mbegu za nje kwa zaidi ya asilimia 70, ipo siku tutakuwa hatarini kutopata mbegu yoyote, hivyo kujikuta tuna njaa. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri ahakikishe ya kwamba suala la uzalishaji wa mbegu ndani ya nchi analitia uzito mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, Sheria ya Mbegu ya Mwaka 2003 haitambui mbegu za asili. Sasa tutafikaje 2025 kuzizalisha ziuzwe madukani ikiwa Sheria ya Mbegu ya Mwaka 2003 haitambui mbegu za asili? Kwa hiyo, naomba sheria hii ya mbegu ya mwaka 2003 ifanyiwe mapitio ili sheria hii izitambue na iweze kuzilinda mbegu zetu za asili kama ambavyo wanafanya nchi za wenzetu India, Ufilipino, Malaysia, Ethiopia na Zimbambwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa tatu, ni lazima sasa Wizara ichukue jitihada za makusudi kabisa za kuboresha Kituo cha Tafiti cha Kutumia Vinasaba vya Mbegu ili kwanza kuimarisha uzalishaji wa mbegu zetu na pia sisi kama Taifa tunaweza tukaingia kwenye soko la vinasaba vya mbegu duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwisho, ni lazima tuanzishe benki ya mbegu za asili ambazo zitasimamiwa na jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naungana na wenzangu kuwapongeza sana Waziri Mheshimiwa Bashe pamoja na Mheshimiwa Anthony Mavunde. Mheshimiwa Bashe ni kaka yangu, ni kati ya mentors wangu, lakini atakapohitimisha, asiponipa maelezo ya uhakika ya kujitosheleza kwamba Wizara hii inakwenda kufanya nini ili kuzitambua na kuzilinda mbegu za asili, basi nitaondoka na Shilingi yake na ataifuata Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana. (Makofi)