Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nipate kuchangia katika bajeti hii muhimu ya kilimo. Kwanza nianze kwa kumnukuu mnenaji mmoja maarufu duniani anaitwa John C. Maxwell anasema, “everything rises and falls depending on the leadership.” Kila kitu kinaweza kupanda au kushuka kinategemeana na uongozi. Nchi inaweza kuzama, kampuni inaweza kuzama, Wizara inaweza kuzama kutegemeana na uongozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza Waziri akitoa hotuba zake kuanzia tarehe 4 siku ile wakati anagawa zile pikipiki, alitoa hotuba moja jiwe sana ambayo ilikuwa kwa kweli ni mwongozo. Kama akiweza kuisimamia, ile ni operating model yake ambayo akiitekeleza nchi hii itakwenda kubadilika. sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru sana Rais, kwa kweli nimekuwa nikiwasikia hawa wenzetu wanaitwa wachache wanasema kwamba political will; maana wakizungua mambo yao wanasema, “political will” kwamba tumemwona Rais ana political will kwenye upande wa kilimo. Hivyo nina uhakika kwamba nchi hii kwenye kilimo itakwenda kubadilika kwanza kugawa zile pikipiki karibu 7,000 na sasa kupandisha bajeti kutoka Shilingi bilioni 294 kwenda Shilingi bilioni 754. Hiyo ni political will.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wenzangu ambao walikuwa wanazungumza kwamba ni maneno; haya sasa siyo maneno tena, kwa sababu tayari jambo limeshakuwa kwenye bajeti na bajeti zimeshatoka. Kwa hiyo, tunashukuru. Pia mwaka jana nilichangia kwa habari ya ruzuku na ninamshukuru sana Rais, pamoja na Waziri kwa sababu ya ruzuku ambayo wanakwenda kuweka sasa kwenye mbolea pamoja na mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii inaonesha namna gani tutakwenda ku-transform kilimo cha nchi hii. Kwa hiyo, kwa kweli niseme Mungu awabariki sana na sisi kama watumishi wenu na wafuasi wenu tutaendelea kuhakikisha kwamba tunafanya kazi ili tuwatie moyo katika kutekeleza majukumu yenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumezungumzia habari ya umwagiliaji, nakushukuru Mheshimiwa Waziri kwamba sasa tunakwenda kubadilisha kilimo chetu kwenye umwagiliaji. Bilioni hizo ambazo zimewekwa kwenye kilimo, sasa naomba hata Jimbo la Kalenga lipate kufaidika pamoja na umwagiliaji huu. Kwenye Jimbo la Kalenga tuna scheme zipatazo 19 ndogo ndogo na za kati. Sasa changamoto nyingi tulizonazo kwenye hizi skimu, nyingi ni za kizamani na kienyeji. Kwa hiyo, unakuta kwamba zinahitaji kutengeneza mabanio tu kidogo ambayo ni bajeti ndogo ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kueleza skimu zote hapa. Kwa mfano, kuna Skimu ya Weru iliyoko Kata ya Ulanda, wanasema hii ina ukosefu wa banio, kwani iliyopo ni ya kienyeji fedha za kutengeneza banio na kugawa mifereji; kitu kama hicho, ziko kama 19. Kwa hiyo, utatusaidia na sisi tupate bajeti, siyo kubwa, angalau tutengeneze hizi banio ndogo ndogo hata kwenye huu umwagiliaji mdogo mdogo tuweze ku-maximize tuweze kupata mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna skimu nyingine nilikuwa ianze, tulishafanya usanifu katika Kijiji cha Magubike Kata ya Nzi. Shilingi milioni 40 zilishatumika kufanya usanifu, lakini hatukuendelea. Hili tutaliangalia, nafikiri document ninayo hapa, nitakuja tuzungumze kirefu na Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji hapo ili tuone tunakwendaje juu ya hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye vyama vya ushirika, ushirika ni nguzo muhimu sana kwenye ukuaji wa uchumi unaokua kwa wakulima. Hata Mwalimu Nyerere wakati fulani alisema, katika mambo ambayo alishawahi kusikitika sana, alisema alisikitika kuuacha ushirika. Tumeona hata wawekezaji wakubwa ambao ninao kule kwenye Jimbo la Kalenga, ambao walikuja katika kulima tumbaku miaka hiyo, walitokea katika ushirika. Kwa hiyo, ushirika ni nguzo muhimu na inaweza kusaidia nchi hii ikaweza kukua kwa sababu watu wakilima katika ushirika ni rahisi sana kuweza kuratibu hata shughuli zao za kilimo lakini shughuli za kimasoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye ushirika kumekuwa na changamoto kubwa. Moja ya changamoto ambazo naziona pia kwenye ushirika ni ukosefu wa vifaa. Kwa mfano, hawana magari. Ni ngumu sana kuweza kufanya uratibu (coordination) wa shughuli za kilimo kama hawana vifaa. Kwa hiyo, Serikali ione namna gani itafanya kuimarisha ushirika kuhakikisha kwamba inawapa vitendea kazi, hasa magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Afisa Ushirika wengi wako chini ya Halmashauri. Sasa napendekeza hawa Maafisa Ushirika wahame kwenye Halmashauri, wawe chini ya Wizara ya Kilimo ili sasa Waziri wa Kilimo awe na nguvu ya kuweza kuwaamuru. Tuliona kwenye ardhi, Waziri wa Ardhi wa wakati huo alihamisha Maafisa Ardhi wakaenda kwenye Wizara ya Kilimo na tumeona ufanisi. Kwa hiyo, na kwenye ushirika tufanye hivyo hivyo, vinginevyo line of reporting zinakuwa nyingi. Kwa hiyo, hakuna mtu mwenye nguvu wa kuweza kuwasimamia. Hili tuliangalie sana ili kama tunataka tukuze kilimo chetu kiweze kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanzisha Kituo cha Afya ya Mimea pale Arusha. Tunaishukuru Serikali, sasa tunaweza kutoa ithibati; tumepata ithibati ambayo inaturuhusu sisi tuuze mazao yetu kwenye nchi zinazotuzunguka. Sasa changamoto ambayo naiona pale ni kwamba tuna mashine ambazo tulipewa za msaada, mashine moja moja; sasa Serikali ione umuhimu wa kuhakikisha kwamba tunanunua mashine nyingine ili sasa kama hii inaharibika, basi tunakuwa na mashine nyingine za kuweza kuendelea kukagua mazao yetu na kuendelea kuyapa ubora unaotakiwa ili tuweze kuuza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ambalo nimeliona, hatuna wataalam. Mara nyingi mitambo ikiharibika tunaleta wataalam kutoka nje na gharama za kuwalipa hawa ni kubwa sana. Kwa hiyo, Serikali ione umuhimu wa kupeleka vijana wetu wakajifundishe huko nje ili waje wahudumie hizi mashine zetu, tusiingize hizi gharama za kuleta wataalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye suala lingine ni kwenye maghala. Nilishalizungumza suala la maghala kwenye viwanda, lakini huku nitalizungumza katika mtizamo mwingine. Maghala yatatusaidia sana. Kwanza tumekuwa na tatizo la sumukuvu kubwa sana katika nchi hii na ukiangalia mazao yanavyohifadhiwa katika maeneo yetu mara nyingi wanamwaga chini ardhini, lakini tutakapokuwa na maghala mpaka kwenye vijiji kama Waziri alivyozungumza, yatasaidia sana kwanza kutunza ubora, na pia kudhibiti upotevu wa mazao. Tuna asilimia karibu 30 mpaka 40 ya mazao yetu yanayopotea. Kwa hiyo, tukiwa na haya maghala itasaidia sana kuratibu na pia kuwa na mazao yenye ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwenye hili atafute pesa, aidha anakopa; hapo ni mahali pazuri pa kuanzia. Hapo utatengeneza alama, utawasaidia Watanzania kupata masoko na utaweza kuratibu mazao yanayozalishwa katika nchi hii na kuwatafutia masoko.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naona kengele imeshagongwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)