Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye sekta hii muhimu ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya na uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, nina uzoefu wa miaka sita, sasa tunakwenda saba; kwenye Wizara hii ya Kilimo kila Waziri anayekuja amekuwa na maneno matamu sana ya kutupa matumaini makubwa wakulima wa nchi hii. Sijawahi kuwa na shida na matumaini ya maneno matamu ya kumtoa nyoka pangoni. Shida yangu kubwa Mheshimiwa Bashe ambalo mpaka sasa kwa hotuba yako tamu uliyoitoa leo kulihutubia Taifa hili: Je, haya uliyotunenea mbele ya Bunge hili, Mheshimiwa Mwijage amesema umelihutubia Taifa; ndiyo na kweli umelihutubia Taifa, yatakwenda kutekelezeka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya unayoyasema, yasemwa miaka nenda, miaka rudi, lakini hatujawaji kuona utekelezaji wake. Suala la bajeti tulisema sana, lakini mkawa mnaongezewa, mnaongezewa, mnaongezewa. Shida siyo kuongezewa bajeti kwenye vitabu, shida ni utolewaji wa fedha kwenda kwenye utekelezaji wa miradi. Wakati mwingine nikikuangalia nakuonea huruma kama vile unaanza kuzeeka kabla ya umri wako, lakini ndiyo hivyo tena tumekupa majukumu, kubali kuzeeka. Utalitendea haki Taifa hili kama haya uliyoyanena leo kulihutubia Taifa hili, utakwenda kuyasimamia kwa dhati ya moyo wako wakulima wa nchi hii wakaona uwepo wako kwenye hii Wizara. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba maneno yake ni mazuri na tunaona njia na nuru ya bajeti yake, lakini Mheshimiwa Waziri huwezi ukawa na miujiza yoyote yakutekeleza haya kama hutakuwa na wasaidizi wa kutosha kwenye Wizara yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee tu mfano upungufu wa watumishi kwenye Chuo Kikuu cha Sokoine. Chuo hiki ndicho kinachotuzalishia wataalam; na watalaam hao ndio tunawategemea watoke chuoni waende field kwa wananchi wetu kule kusaidia kilimo bora, kilimo chenye tija kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhitaji wa watumishi Chuo Kikuu ni 2,076; tulionao ni 1,253. Tuna upungufu wa zaidi ya watumishi 800. Bila ya hawa kuwepo, haya yote aliyoyaeleza Mheshimiwa Waziri itakuwa ni kazi bure. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Bashe, tunakuomba usimame kwenye ajira zinazokuja hizo zilizotangazwa na naiomba Serikali, kipaumbele iwe ni sekta ya kilimo tupate watumishi wa kutosha waende wakatusaidie kwenye suala zima la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la pili ambalo natamani kulisema leo, ni suala zima la ushirika. Wote tunaamini kwenye suala zima la ushirika, lakini nina changamoto moja. Moja ameisema kaka yangu Mheshimiwa wa Jimbo la Kishapu kuhusu upungufu wa watumishi, lakini pamoja na upungufu wa watumishi wa Ushirika, halikadhalika watumishi waliopo baadhi yao sio waadilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna madhaifu makubwa sana ya watumishi wa Kitengo cha Ushirika kutokuwa waadilifu, lakini kwenye ushirika huko huko watumishi wetu, Maafisa Ushirika, wao ndio wanajifanya wamiliki wa ule ushirika ilhali wamiliki wa ushirika ni wananchi wenyewe walioamua kujiunga kwenye ushirika, lakini wao ndio wamekuwa ma-top wa ule ushirika kiasi kwamba kupelekea watu na Watanzania kuuchukia ushirika kwa sababu ya watumishi wasiokuwa waadilifu kwenye sekta ya ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Namwomba Mheshimiwa Waziri, watumishi wote wa sekta yako ya ushirika ambao sio waadilifu, suluhisho lisiwe kumtoa Chemba kumpeka Hombolo, suluhisho ni apaki gari lake pembeni hili atupishe tuweze kufanya kazi ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilitembelea Mikoa ya Kusini kwa ajili ya kwenda kuona namna gani ushirika unafanya kazi. Tumekuta watu kule wako vizuri na mfumo wao uko vizuri; na leo kwa mara ya kwanza nakuwa muumini wa Stakabadhi Ghalani ambayo niliipinga kikao kilichopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipofika kule nikakuta watu hawa kwenye ushirika wao wanafanya mazao yao vizuri, wanauza mazao yao vizuri, na kiasi kwamba inapelekea kwenda kuwa na vitega uchumi ambavyo vina fedha nyingi sana. Ila changamoto iliyopo, watu hawa unakuta wanamiliki mradi wa Shilingi bilioni 1.5 lakini watu hawa wanakwenda kukopa fedha kwa ajili ya kumpeleka mtoto wake shule, analipa riba ya asilimia 24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri, naomba ushirika uende ukawafundishe wananchi wetu ambao wako tayari kujiunga na ushirika namna ya kujiwekea akiba kwenye vyama vyao badala ya kwenda kukopa benki, waepukane na kodi ya asilimia 24 waweze kuchukuwa fedha yao ile iliyoko pale waweze kukidhi mahitaji yao wakiwa wamevuna mazao yao na wanasubiri msimu wao wa bei kupanda ili waweze kuvuna mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba pia nizungumzie suala zima la kodi kwenye zana za kilimo. Tuna changamoto kubwa sana kwenye zana zetu za kilimo na hili limesemwa hapa. Tuna mfuko wa pembejeo ambao sasa unaenda kuzama baharini. Sasa hebu fikiria, leo mwananchi wa kawaida, wa Itololo kule ambaye ana eka zake tano au kumi, anatamani kutoka kwenye kilimo cha jembe la mkono angalau akanunue power tiller ama hata trekta, lakini ukienda kuuliza bei ya power tiller ni shilingi milioni kumi na kitu, shilingi milioni saba, na kadhalika; ukigusa trekta, shilingi milioni 45, shilingi milioni 60, shilingi milioni 30. Ni mwananchi gani wa nchi hii jamani anayeweza kumiliki trekta kwa bei hizo?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuondokana na kilimo kisichokuwa na tija na tuwasadie wakulima wetu, tunaiomba na Serikali kwa ujumla, zana za kilimo.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: … wananchi waweze kumiliki matrekta na kuleta tija kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)