Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii. Kama walivyosema wenzangu waliotangulia bado nampongeza Mheshimiwa Waziri Bashe, kwa kuwa amekuwa mwepesi, tunapompelekea matatizo yetu kutusaidia hususani sisi watu wa Nyanda za Juu Kusini ambapo ndiyo tunalima sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imezungumza habari ya pembejeo na hasa tukienda kwenye eneo la mbolea; kwa muda mrefu imekuwa bei pamoja na kwamba wameizungumzia, wananchi wamepata shida sana, sana katika ulimaji msimu huu wa kilimo. Tunafahamu kabisa na Mheshimiwa Waziri amesema kwamba dunia imepandisha bei, lakini mwisho wa siku Watanzania wana Serikali yao ambayo wanaitegemea na tunajua kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo kama ambavyo tulikuwa tukisema miaka mingi, watanzania hao wanahitaji chakula. Sasa Serikali kuchelewa kutoa maamuzi ya kuwasaidia wakulima na hasa kuweka ruzuku kwenye mbolea, nafikiri wamefanya kosa kubwa sana la kutufanya tusiwe na chakula kipindi kinachokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia mbolea kupanda bei, DAP ilikuwa shilingi 66,000; Urea ilikuwa Sh.53,000, mbolea hizi zilifika mpaka bei ya shilingi 150,000 kwa mfuko wa kilo 50. Sasa kuna haja ya Mheshimiwa Waziri kuona matatizo yanapotokea kuwa na first truck ya kuamua kuweza kusaidia Watanzania. Kwa kukaa kimya mpaka leo bajeti imekuja na Waziri anatamka na hatujui utekelezaji wake utachukua muda gani, kwa kweli hatujawatendea haki wakulima wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amezungumza kwenye hotuba na naweza kumwamini kwa sababu naamini anaweza kufanya kazi...

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kumpa mzungumzaji taarifa kwamba, pamoja na kwamba mbolea ilikuwa bei ya juu, lakini bado upatikanaji wake ulikuwa ni changamoto kwa wakulima wetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakagenda unaipokea taarifa?

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea. Tunaamini kwa uchapa kazi wa Mheshimiwa Bashe, bajeti hii ameipata moja kwa moja akiwa Waziri, kwa hiyo, alichokisema hapo kwamba anaenda kuhakikisha mbolea inashuka bei, lakini si tu, hivyo inapatikana kwa wakati ili wakulima wasiingie kwenye matatizo. Tunaomba Mheshimiwa Waziri alitekeleze hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la chai. Zao la chai ni zao kubwa sana katika nchi yetu ya Tanzania. Mikoa inayolima chai au sehemu zinazolima chai, Lushoto, ukienda Muheza, Njombe na Rungwe kwetu tunalima sana chai. Nimekuwa nikisema mara nyingi hapa Bungeni na nikiongea na Mheshimiwa Bashe juu ya zao hili. Zao hili kwa ripoti ya Bodi ya Chai yenyewe, inasema uzalishaji wa chai umepungua kwa asilimia nne katika mwaka uliopita. Kwa nini zao hili linapungua kwa wakulima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao hii linapungua kwa sababu bei yake haipandi na bahati mbaya sana Bodi ya Chai kama wapo hapa wananisikiliza wanapendelea maeneo kwa maeneo. Nchi ni moja lakini chai inauzwa bei tofauti tofauti. Ukienda Rungwe chai haizidi Sh.230, lakini ukienda Njombe unakuta chai kilo moja ni Sh.500. Nchi moja, wakulima hao hao, Rais wao mmoja, lakini bado tumewagawa kwenye bei. Sijaelewa ni vigezo gani Bodi ya Chai inatumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, Bodi ya Chai haisimamii haki ya wakulima, kuna makampuni yanayonunua chai mbichi, lakini wakulima kwa muda mrefu hawalipwi madeni yao bila sababu yoyote. Sisi tunaamini Bodi ya Chai ndiyo msimamizi wa wakulima wasiokuwa na sauti, lakini bodi hii imeungana na wanunuzi, imeungana na makampuni na kuwaacha wakulima wakihangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la pembejeo kwa wakulima wa chai. Makampuni haya yanatoa mikopo ya mbolea kwa bei ambayo si nzuri. Mtu anapewa mfuko wa mbolea kwa bei iliyo juu, akija kuuza chai anakuja kukatwa, mwisho wa siku mkulima anabaki na fedha ndogo sana. Naomba Mheshimiwa Waziri alisimamie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii chai nimeizungumzia muda mrefu na naomba sana, sana kwa maelezo ya CAG, ukaguzi uliofanyika mwaka huu Machi, 2022, makampuni sitaki kuyataja hapa, yamekopa wakulima toka 2018 mpaka leo hii hawajawalipa madeni yao. Naamini Mheshimiwa Bashe anayamudu makampuni haya, naomba ayasimamie ili wawalipe wakulima stahiki zao, kwa sababu wamefanya kazi kwa jasho na sasa wanahitaji kutumia fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Benki ya Kilimo; benki hii ipo kwa ajili ya wakulima, lakini kwa mfano, kwa wakulima wadogo wadogo, kuna mfuko ambao ulitolewa pesa zaidi ya bilioni 7.0 kwa ajili ya kuwakopesha wakulima wadogo wadogo, lakini pesa hii kwa mujibu wa CAG kwenye ripoti ya Machi, 2022, walichukua pesa hiyo wakabadilisha matumizi badala ya kuwakopesha wakulima wadogo wadogo. Pesa hiyo ikaenda kufanya kazi nyingine bila kuwasaidia hao wanaohitaji msaada wa kukopa. Naomba hilo pia Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha anipe maelezo tuweze kuelewa ilikuwaje, kwa sababu mwisho wa siku wakulima wakubwa wanafaidika na walio wengi ambao ni wadogo hawapati chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba Benki ya Kilimo lengo lake ni kusaidia Watanzania, tunaomba isimamie lile kusudio ambalo imepewa na Serikali. Pia kuna Mfuko wa Pembejeo, Mfuko huu unaenda kufilisika kwa sababu zaidi ya bilioni 27 ambazo zilitolewa, bilioni 20 zimekopwa na hazijarudi. Sasa tunawezaje kusaidia Watanzania kama kuna fedha zinatolewa halafu hazirudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mheshimiwa Waziri ametoa kwenye hotuba yake akisema, anataka watu wanaouza pembejeo mbolea waungane. Naamini katika mipango mizuri aliyonayo Mheshimiwa Waziri au iliyonayo Serikali yake, lakini mwisho wa siku utekelezaji haupo. Kupanga ni kitu kingine na kutekeleza ni kitu kingine. Kwa hiyo, Mfuko huu zaidi ya asilimia 72 pesa bado ziko mikononi mwa watu, hazijarudi wakati sisi tunategemea pesa hizi ziweze kusaidia wale wengine ambao bado hawajakopa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalima parachichi kama alivyosema Mheshimiwa Waziri na watu wamejitokeza kulima parachichi kweli kweli, lakini kwenye export ya parachichi tunashindwa kujenga kiwanda cha kutengeneza box la kuhifadhia parachichi mpaka twende Kenya tukanunue. Nafikiri hatujitendei haki kama Watanzania kwa sababu kujenga kiwanda cha kutengeneza box hapa, tutatoa ajira kwa vijana na tutapunguza gharama ya ku-export parachichi, badala ya kwenda kuagiza Kenya, order inachukua mpaka siku nne mpaka siku saba, mtu aipate kutoka Kenya, ije Rungwe iende Makete, tunakuwa hatuwatendei haki Wtanzania. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)