Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia matukio makubwa ambayo siyo ya kawaida; Vituo vya Polisi kutekwa nyara, bunduki kuporwa, mauaji na uporaji wa mabenki na wenzetu Askari wanajitahidi kuhakikisha kwamba wanadhibiti hali hiyo. Ninayo maeneo machache ya kuchangia, lakini moja ni suala la watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyoona kwenye hotuba zilizotangulia ni kwamba ratio ya Askari ni mmoja kwa 1,071 nchini kwetu hapa, lakini katika nchi zilizoendelea ni mmoja kwa 450. Sasa ni muhimu tukahakikisha kwamba tunafanya jitihada za makusudi kuajiri askari zaidi. Tumeona kwamba kuna wanaoajiriwa, lakini uwepo mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba pengo hilo linazibwa ili kuweza kuwa na usalama wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Jeshi la Polisi limekuwa linafanya kazi, lakini limekuwa na uhaba wa magari. Uhaba wa magari ni tatizo; matukio yanapotokea hawawezi kwenda kwa wakati kwa sababu magari hayapo na machache yaliyopo mengine ni chakavu. Kwa hiyo, ni muhimu ukatengenezwa mapango mkakati kuhakikisha kwamba Polisi wetu wanapata magari ya kutosha na yawepo maeneo yote hasa ya Vijijini kwa sababu matukio hayapo mijini tu na vijijini yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia liko tatizo la mafuta; Polisi wetu wamefikia hatua sasa ya kuwa ombaomba. Wanaomba mafuta kwa wafadhili mbalimbali, lakini wanapoomba mafuta, wanaomba kwa mhalifu mtarajiwa. Kwa hiyo, mhalifu mtarajiwa atakapofanya uhalifu, Polisi wanakosa nguvu ya kwenda kumkamata kwa sababu anakuwa ni mshirika kwenye utendaji kazi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wamezungumza suala la BRN (Big Results Now). Suala linalojitokeza hapa ni kwamba mpango umeandaliwa vizuri na ulikuwa uanzie Dar es Salaam, lakini mpango wenyewe haujatengewa fedha za kutosha na hiyo ilikuwa ni pilot study ambayo baadaye ingesambaa kwenye mikoa mingine. Sasa ni muhimu ikaangaliwa namna mradi huu ufanyike na tuweze kuupima ndani ya mwaka huu mmoja na tuone kwamba tutasonga vipi mbele, lakini intent ya mradi huu ilikuwa kudhibiti vitendo vya uhalifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Askari wetu pia wana matatizo ya sare. Askari anatakiwa awe na zaidi ya pair mbili; lakini inapoonekana Askari anakuwa na pair moja tu, tunakoelekea huko Askari watakuwa wanavaa nguo za kiraia kama hatutakuwa makini. Kwa hiyo, ni jambo muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la makazi, limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge waliopita, lakini tukiweka mkakati wa makusudi kwa mwaka huu na kwa miaka inayokuja katika kipindi hiki cha utawala wa Serikali, miaka mitano ya utawala uliopo madarakani, tuna hakika kabisa suala hili litapata ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo habari ya Magereza. Hapa nataka kugusia suala la msongamano. Msongamano huu, kuna namna mbalimbali ambazo zimeshazungumzwa, adhabu mbadala; wengine wafungwe uraiani wafanye kazi za kijamii. Hilo ni jambo jema, lakini inaonekana utekelezaji wake umekuwa ni wa kusuasua sana. Hii ni kwa sababu sheria hizo zilishapita miaka mingi iliyopita, lakini bado hazitekelezwi. Kwa hiyo, nashauri mamlaka zinazohusika zitekeleze kikamilifu ikiwemo ujenzi wa Magereza mapya hasa katika Wilaya mpya ikiwemo Wilaya ya Mkalama. Hilo ni jambo la muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie suala lingine nyeti; mimi niko kwenye Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama; tulitembelea kwenye Gereza la Isanga, kuna eneo ambako wako kuna watu waliohukumiwa hukumu ya kifo. Watu hao na wenyewe wanasongamana; na kwa sababu wamesongamana na utekelezaji wa adhabu hiyo unachukuwa muda mrefu, watu wameshakaa muda mrefu sana kwenye eneo hilo. Kwa hiyo, ni vyema basi kukawepo na tafakari mpya, labda wabadilishiwe kifungo kiwe kifungo cha maisha, lakini waweze kufanya na kazi nyingine na waondoe msongamano huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo, wako watu ambao rufaa zao hazijasikilizwa, wana haki ya kukata rufaa, lakini ma-file yao yako kwenye kanda nyingine. Kwa hiyo, wamekaa hawajui ma-file yao yatakuja lini na wameshakaa kwa muda mrefu. Nashauri zichukuliwe hatua za makusudi kabisa, ma-file hayo ya wananchi yaletwe, rufaa zao zisikilizwe na hukumu itolewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa bado niko kwenye Idara ya Magereza, kumekuwa na changamoto kubwa kwa Askari Magereza kwa sababu dawa haziko za kutosha. Ina maana wafungwa wakiugua Askari Magereza sasa wanachukuwa majukumu la kusaidia kutoa pesa zao mifukoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mahabusu wanapopelekwa kwenye kesi zao Mahakamani, imefikia mahali ambako wanapakiwa kwenye magari ya uraiani; na wenyewe wanatakiwa wawe na magari maalum. Mambo hayo yanatakiwa yaangaliwe kwa ukaribu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa bado katika Jeshi la Magereza, kuna miradi mbalimbali kama vile miradi ya mifugo na miradi mizuri, tunasema tunataka nchi hii iwe nchi ya viwanda ikiwemo viwanda vya nyama. Tunaamini kabisa miradi hii ikiwekewa mitaji ya kutosha wanaweza wakatoa mchango katika kupeleka malighafi kwenye viwanda vya nyama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Jeshi la Magereza linakabiliwa na uvamizi kwenye maeneo yake. Kwa hiyo, tunaomba Wizara iangalie suala hili, viwanja vyote vya Magereza viweze kupimwa na wawe na hatimiliki ili migogoro na wananchi iweze kumalizika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, pamoja na mambo yote niliyozungumza, lakini liko jambo moja ambalo naomba Wizara hii kwa kushirikiana na Wizara ya Sheria na Katiba ilifanyie kazi. Lenyewe linahusu mfungwa mmoja ambaye ni binti, yuko Gereza la Isanga hapa, yule amekatwa vidole viwili; kidole cha mkononi na cha mguuni na yuko Magereza. Sasa huo ni unyanyasaji na ukiukaji wa haki za binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba suala hilo Mawaziri husika walichukuwe, walifanyie kazi na walete taarifa. Binti yule ameshakaa muda kidogo kule ndani; akiendelea kukaa ndani ya Magereza na huku amedhulumiwa kiasi hicho, maana yake ni kwamba haki itakuwa haijatendeka. Ni vyema suala hilo lichukuliwe na lifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono na nafikiri ushauri nilioutoa unaweza ukafanyiwa kazi na Wizara. Ahsante.