Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia; na niseme tu ninayofuraha kubwa sana kuanza kuchangia kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwa champion namba moja wa masuala ya lishe katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe tu ni wiki mbili zimepita tumeona Mheshimiwa Rais ameenda kuzindua jukwaa la mfumo wa chakula Barani Afrika, Dar es salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu leo utajikita sana kwenye suala la lishe kwa sababu ni kitu ambacho kama taifa tunapitia changamoto kubwa sana. Na kama tunavyoona, hali ya udumavu kwa nchi yetu tuna asilimia 30, kitu ambacho kama taifa tunatakiwa kujitathmini na kuangalia ni jitihada gani za msingi tunazoziweka ili kuhakikisha hali ya lishe nchini inaimarika.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nimeongelea suala tu la udumavu kwamba ni asilimia 30, lakini tuna kitu kinaitwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo hayo yanaenda kwa asilimia 45. Kwa hiyo unaweza ukajumlisha asilimia 30 na asilimia 45 unaweza ukaona kwamba ni kwa kiwango gani nchi yetu ina hali mbaya ya lishe. Kwa hiyo naomba tu niweke msisitizo kwamba kama Taifa ipo jitihada ya kufanya kuhakikisha suala la lishe linapewa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea suala la lishe tunaona mikoa inayozalisha chakula ndiyo mikoa ambayo inateseka na hali ya lishe duni. Ukiangalia Mikoa kama ya Iringa, Njombe, Rukwa na mikoa mingine kama Songwe, Morogoro, Mbeya unaona bado hali hali duni ya lishe iko juu. Tunapoongelea udumavu kwenye mikoa yote hii iko juu ya ile cut-off point ya hali ya udumavu kwa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninazidi kusisitiza tu kwamba kama taifa tuone umuhimu wa kupambana na suala la lishe ili tuweze kuondoa hizo changamoto za utapiamlo. Tunapoongela lishe ndicho kitu kinachogusa kuanzia wakati wa mimba mpaka mtu anakuja anazeeka. Katika suala la lishe tunaangalia kuanzia chakula kinapozalishwa, kinapovunwa shambani, kinavyochakatwa mpaka kinavyokuja kwenye utumiaji ule wa mwisho; lakini pia bila kusahau zile hatua za uchakataji wa hiki chakula ili kiweze kuhifadhika kwa matumizi ya baadaye. Kwa hiyo kuna mambo mengi ambayo kama taifa tunatakiwa tuzingatie kwenye suala la lishe ili tuweze kuwa na Taifa ambalo litakuwa na afya nzuri na litakuwa na tija kwenye mchakato mzima wa maendeleo ya kiuchumi wa taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo langu kubwa katika kuongea haya yote ninayoyaongea ni kwamba mpaka saa hizi Sera ya Lishe ya Taifa inayotumika ni ya mwaka 1992. Ni miaka 30 nyuma tangu hiyo sera ianzishwe mpaka leo sioni jitihada ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuja na Sera ya Taifa ya Lishe ambayo itaenda kusaidia kupunguza changamoto zote za masuala ya lishe yanayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona taifa limekuwa linapitia hatua mbalimbali za masuala ya lishe, tunaona kwamba kama Taifa wameweza kuajiri maafisa lishe, walau angalau sasa kila halmashauri ina afisa lishe mmoja, ambao nao si toshelevu. Lakini tunaona kumekuwa na uanzishwaji wa kamati za lishe kwenye halmashauri zetu, na ni kuanzia ngazi ya taifa tumekuwa na nutritiol steering committee pamoja na ngazi ya mkoa na wilaya, na wamekuwa na harakati za kuhakikisha zinaenda mpaka kwenye ngazi ya kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kabisa kumekuwa na utengenezaji wa mikakati ya lishe. Tumeona mkakati wa MNAP1, MNAP2 lakini mambo hayo yote yanafanyika kindi ambacho hatuna sera ambayo inaweza ikasimamia haya mambo yote; yaani sera inayoenda na wakati ya kuweza kuyasimamia haya mambo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeona kabisa Mheshimiwa Rais aliweza kusaini mikataba ya lishe na wakuu wa mikoa; na hii mikataba ya lishe imeenda mpaka ngazi ya chini kabisa kwenye kata, watu wamesaini mikataba ya lishe; lakini inasainiwa kutoka kwenye msimamo upi wa kisera?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapokuwa nayaona hayo ninazidi kuona umuhimu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuona umuhimu wa kufanya uwepo wa sera ambayo inaenda na wakati ya masuala ya lishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa sera ya lishe ulikuwepo na umeanza tangu 2017 ni miaka mitano zaidi saizi mpaka saizi hatuoni matokeo ya sera ya lishe. Ninapokuwa nayajadili haya natamani kuona Waziri Mkuu atapokuwa ana-wind-up mwishoni atuambie ni wapi ambapo hii sera ya masuala ya lishe imeweza kukwama? Kwa sababu tumeona kumekuwa na uzalishaji wa vyakula saizi tuna vitu vinaitwa GMO.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vitu ambavyo vina-impact kwenye chakula na afya za Watanzania, lakini tunaona kabisa kumekuwa na kemikali mbalimbali ambazo zinaingizwa nchini kwa ajili ya processing za vyakula mbalimbali. Kuna udhibiti gani, lakini tumeona athari ambazo zimetokea pale ambapo TFDA iliweza kuvunjwa ikapelekwa ikapelekwa TBS. Tumeona ni wapi ambapo tumekuwa tukifeli kama Taifa. Kwa hiyo kuna mambo mengi katika masuala ya chakula ambayo yamekuwa yakiendelea ambayo yanahatarisha usalama wa chakula chetu, kitu ambacho kingekuwa na sera nzuri inayoenda na wakati ingekuwa rahisi kwa wasimamizi au waratibu wetu wa masuala ya lishe kuweza kuzingatia vigezo ambavyo viko kwenye hiyo sera. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea suala la chakula ni suala la Kitaifa, lakini ni la Kimataifa na ndio maana utakuta wakati mwingine hata bidhaa zetu zinazuiliwa kwenda Mataifa mengine. Mfano mzuri ni lile suala la mahindi yale yalikuwa yanaenda Kenya, masuala ya sumu kuvu, unaona kabisa usimamizi wa namna ya utunzaji wa vyakula vyetu ina maana hauko smart mpaka mahindi yanazuiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama tutakuja na sera nzuri, sera ambayo inaenda na wakati, ina maana hata wajasiriamali wetu, wakulima wetu wataweza kuzalisha vyakula vitakavyokuwa na ubora na mwisho wa siku sisi kama Taifa tutakuwa tuna uhakika wa chakula kilichobora, lakini pia sisi kama Taifa tutakuwa na uwezo wa ku-supply vyakula vyenye viwango vya Kimataifa. (Makofi)

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MBUNGE FULANI: Endelea ni kengele ya kwanza.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilifikiri muda umekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niseme tu, Ofisi ya Waziri Mkuu ije na kauli ya kusema ni wapi mchakato wa masuala ya Sera ya Lishe umekwamia. Kwa sababu haiwezekani jambo moja miaka mitano linaendelea kutokutekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho ningependa kukiongelea, na-declare interest kwamba mimi ni mkazi wa Mji wa Tunduma na Mji wa Tunduma kama Taifa huwa siku zote naendelea kusisitiza kwamba ni mji wenye tija na ni mji ambao kama Taifa kweli litaamua kuwekeza ni kitu ambacho wanaweza wakapata fedha nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mipango mingi ambayo inatekelezwa upande wa Dar es Salaam bila kuzingatia destination ya ile mizigo au shughuli zile zinazofanyika Dar es Salaam kwamba zina impact ipi kwa Mji wa Tunduma. Natamani kuona kwamba mipango yao Ofisi ya Waziri Mkuu, sera zao wanazoziunda katika kuhakikisha wanakuza uchumi wa nchi hii, wawe wanafanya kwa kuzingatia na Mji wa Tunduma au Mkoa wa Songwe kwa ujumla; la si hivyo tutakuwa tunawekeza sehemu moja, tunaboresha eneo la Dar es Salaam pekee yake, lakini eneo ambalo mizigo hii inaenda kama Tunduma unakuta halipewi kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niseme tu hali ya Tunduma kwa maana kwamba kwa kuweza kusaidia mchakato mzima wa ukuaji wa maendeleo ya nchi hii kwa kulinganisha na Dar es Salaam, haina mazingira mazuri. Naamini kabisa kama kweli asilimia 70, kwa sababu takwimu zilizopo ni asilimia 70 ya mizigo inayotoka Dar es Salaam inapita custom ya Tunduma. Waone jitihada ya kuwekeza kule, nakumbuka ni juzi tu hapa Mheshimiwa Stella alikuwa anauliza suala la dry port, yakajibiwa majibu kirahisirahisi tu. Majibu ambayo hayakuonesha kwamba Serikali inayo dhamira ya kuhakikisha kwamba kwanza inalinda barabara zetu ambazo zinajengwa kwa gharama kubwa, lakini pia kuona umuhimu wa kuongeza soko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kukiwa na dry port Tunduma, wafanyabiashara wa nchi zingine za SADC wanaweza kuona wepesi wa kuja kuchukua mizigo yao pale au kuagiza kupitia bandari yetu kwa sababu huduma inakuwa imesogezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niseme tu na niombe kwamba Wizara hii ya masuala ya mipango izingatie pia Mji wa Tunduma katika mipango yake, ahsante. (Makofi)