Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kuniruhusu na mimi niweze kuchangia. Kwanza nianze sana kwa Kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya nchi hii. Vilevile nimpongeze pia Waziri Mkuu na msaidizi wake Makamu wa Rais kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya kuunga mkono jitihada za Rais Mama Samia Suluhu Hassan. Vilevile niwapongeze Mawaziri wote kwa namna ambavyo wanavyojituma kuunga mkono jitihada za Rais za kutuletea maendeleo katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema wenzangu na mimi niungane. Ukweli utabaki kuwa kweli, kuna methali inasema Mnyonge mnyongeni haki yake mpe. Hapa hakuna mnyonge mnyongeni habari ya mnyonge mnyongeni haipo. Mama Dkt. Samia anafanya kazi kubwa, kazi nzuri ya maendeleo katika Halmashauri zetu na nchi hii haijapata kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Miradi iliyoko huko kwenye Halmashauri zetu Mabi, na Mabii, na Mabii ni nyingi kwa hiyo tunampongeza sana. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, fedha zinazokwenda huko ni nyingi na wanaosimamia pia katika Shughuli hizi ni pamoja na Waheshimiwa Madiwani wetu. Naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu ni lazima tuhakikishe ili wakasimamie vizuri na wenyewe waongezewe posho ili wakasimamie vizuri shughuli za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukulie kwenye jimbo langu la Makambako, ukienda upande wa Maji, miradi iliyofanyika katika jimbo langu ni mingi ya hela nyingi za mabii na Mabii. Vilevile tuna miradi ile ya miji 28 hivi sasa mkandarasi yuko site anaendelea na shughuli za miradi ya maji vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaimani atakapomaliza hivi 2025 Mkandarasi huyu tatizo la maji katika Mji wetu wa Makambako litakuwa limeisha kabisa kwa asilimia zaidi ya100. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye Afya, shughuli nyingi nzuri zimefanyika sana katika jimbo letu la Makambako lakini katika nchi nzima. Vilevile ukienda katika upande wa barabara; barabara nyingi zinatengenezwa vizuri hususani pale mjini tuna barabara zinatengenezwa za lami, kuna barabara za Changarawe na Vumbi zinaendelea kutengenezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu TARURA waongenzewe bajeti ili waweze kufanya kazi nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukinda kwenye elimu, vilevile kwa miaka nenda inapofika Januari, wananchi wetu huwa wanapata tabu kwa namna ambavyo tunakuwa tunawachangisha ili madarasa yaweze kujengwa. Kwenye Halmashauri yetu na nchi nzima tumepata fedha nyingi madarasa yamejengwa na Shughuli zinaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi upande wa elimu, kuna Shule kongwe za msingi ikiwepo Shule ya Mwembe Togwa, Shule ya Mashujaa, shule hizi sasa zinahitaji zipate hela kwa ajili ya ukarabati na kujenga madarasa mengine mapya.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto; pamoja na kazi nzuri mbalimbali ambazo zimefanywa tuna changamoto. Tuna tatizo la fidia eneo la Polisi ambalo Mheshimiwa Rais alipokuja Mwezi Agosti, 2022 wananchi wale wanapata tabu fidia ya Shilingi Milioni 235, wanashindwa sasa waende wapi kwa sababu hawaruhusiwi kuongeza kitu chochote. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ihakikishe fedha hizi zinatolewa kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais ili wananchi hawa waweze kulipwa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye fidia kuna eneo ambalo walipewa fidia zaidi ya shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kujenga Soko la Kimataifa, kuna wananchi 18 walibaki hawakulipwa. Tunaiomba Serikali ihakikishe wananchi hawa wanalipwa fidia zao, stahiki zao ili kero hii iweze kuondoka. Hata hivyo, Mheshimiwa Rais alipokuja aliagiza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye fidia kuna tatizo la umeme wa upepo Watu wa muogemo wa upepo walikuja wawekezaji pale na walikuwa tayari kulipa fidia tatizo lipo kwenye wizara ya nishati. Niombe sana Mheshimiwa Naibu Waziri tuhakikishe kwamba hii fidia inalipwa ili wananchi waweze kuishi kwa amani. Nimekuwa nikilizungumza mara nyingi sana jambo hili, na naomba sasa lipate baraka za wananchi hawa kwa kulipwa fidia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile kuna suala la vifaa tiba. Kwenye halmashauri zetu au kwenye wilaya zetu kwenye hospitali za wilaya tumepata vifaa tiba ambavyo hatujawahi kupata. Tumepata mpaka vifaa ambavyo vinashitua moyo, ambavyo vilikuwa vinapatikana KCMC au Muhimbili. Leo sasa makambako vimekuwepo vifaa hivyo. Kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. Vifaa ambavyo vilikuwa vinapatikana Ulaya tu leo viko Makambako, vinapatikana; kwa hiyo tunaipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri ambayo tumekuwa tukiifanya (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu lingine, kuna barabara ya kutoka Kigoma kwenda Lupembe. Barabara hii tanga 2015 iko kwenye ilani, 2020 iko kwenye ilani. Ombi langu barabara sasa itengewe fedha kwa ajilli ya kutengeneza na wananchi wa lupembe wana imani kubwa kwa sababu rais wetu akiwa Makamu wa Rais aliwaahidi, na sasa tunaomba barabara hii iweze kutengenezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, si kwa umuhimu, ameteuliwa kijana anayeshughulikia mambo ya dawa za kulevya; tunampongeza sana mama kwa kumteua kijana huyo. Ni imani yetu kwamba vijana wetu watapona; akasimamie vizuri suala la madawa ya kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, la mwisho, na Waheshimiwa Wabunge wenzangu hili la mwisho kabisa. Rais Mama Samia yaani hata unapotembea kwenye jimbo lako unatembea unaringa, unajidai kwa sababu mabilioni na mabilioni yamekwenda huko. Na imani yangu, kutokana na mabilioni yaliyokwenda huko Wabunge wote mtarudi na Mama Samia atapata kura nyingi haijapata kutokea kwa sababu ya kazi anazozifanya ni nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na wewe kwenye jimbo lako yamefanyika kule. Yaani ukipita huku mara upande juu mara ushuke chini na kadhalika na kadhalika, kazi iliyofanyika Dar es salaam ni nzuri, kwa hiyo na wewe tunakuombea, utarudi. vievile Mbeya kwa Spika haijawahi kutokea, ule msongamano wa Mbeya sasa wamepata by-pass ya kupunguza msongamano. Kwa hiyo tunakuombea na wewe Spika na utarudi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo haya nichukue nafasi kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia; lakini kwa kweli mama tunampongeza sana kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya. (Makofi)