Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Nakushukuru sana kwa kunifanya mchangiaji wa kwanza kwa hotuba hii muhimu sana ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kimaumbile nilivyoumbwa, siwezi kunyamaza. Nikitendewa jambo jema, nitasema, tena nitasema kwa sauti kali; lakini likitendwa jambo baya, nasema tena nasema kwa ukali zaidi. Sasa naomba nizungumze kwa sauti nzuri, sauti ya unyenyekevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan. Nasema hivyo kwa sababu nimetumwa na wananchi walionichagua. Jimbo langu lilikuwa limejifunga, walioko milimani hawafiki tambarare, na walioko tambarare hawafiki mjini kwa sababu nilikuwa sina barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeanza kuongoza jimbo hili mwaka 2005. Miaka yote nilikuwa napewa pesa Shilingi milioni 350 na majedwali yote ninayo ya kuanzia mwaka 2005, Shilingi milioni 350 za kutengeneza barabara za TARURA. Tangu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameingia madarakani tarehe 19 mwezi wa Tatu mwaka 2021 mpaka leo, Jimbo la Same Mashariki limepewa fedha za kutengeneza barabara za TARURA Shilingi 5,200,000,000/=. Hili jambo siyo la kawaida. Wananchi wa Same Mashariki wanamshukuru sana Rais aliyeko madarakani, mpaka wananiuliza, hivi hizi pesa zilikuwa wapi miaka yote? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wangu asilimia 100 ni wakulima, na mkulima anahitaji barabara apeleke mazao yake kwenye masoko makubwa. Jimbo lilijifunga, walanguzi ndio wanaoweza kufika milimani kuchukua tangawizi kwa bei wanayoitaka wao; lakini sasa hivi wananchi wangu wanapeleka kwa magari, hawana wasiwasi, njaa jimboni kwangu imepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi tarehe 01/03/2023 walifanya sherehe kubwa kwangu ya kumshukuru Rais. Leo hii wamenituma kwa Waziri Mkuu, wameniambia tunakutuma kwa Waziri Mkuu na yeye ukamtume akamwambie Rais tunampenda sana, tunamshukuru sana, Mungu ambariki. Hapo nimesema kwa sababu nimefurahi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naingia jambo la pili. Serikali ya Chama cha Mapinduzi nawashukuru. Mimi natokea Mkoa wa Kilimanjaro. Mkoa wa Kilimanjaro elimu ilianza siku nyingi sana, shule zimeanza siku nyingi sana kwa sababu kuna waeneza dini, wamisionari walianza kuingia kwetu mwaka elfu moja mia nane themanini na kitu hivi. Walipoeneza dini wakajenga Shule. Baadae Serikali ikataifisha zile shule, ikajenga pamoja na wananchi. Hata hivyo, Shule zile zimechakaa sana, shule zile za msingi zimechoka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kuna waeneza dini, wamisionari walianza kuingia kwetu mwaka elfu moja mia nane themanini na hivi. Walipoeneza dini wakajenga Shule baadae Serikali ikataifisha zile Shule ikajenga pamoja na Wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, shule zile zimechakaa sana, Shule zile za msingi zimechoka sana, naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita. Nimeona na nimeletewa ripoti hapa ya pesa za boost za kwenda kuboresha na kujenga Shule za Msingi za Mkoa wa Kilimanjaro, nimepokea za kwangu, Charles angalia utaona za kwako huko. Kila Halmashauri ya Mkoa wa Kilimanjaro tunamshukuru Mungu tumepokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali naomba niwambie kitu kimoja Serikali ya Chama cha Mapinduzi, hizi Shule zitajengwa, hizi Shule zitaboreshwa, nitoe mfano; huu mwaka uliokwisha 2022 Serikali ilinipendelea iliniletea Milioni 100 za kujenga upya Shule ya Msingi inayoitwa Kihurio Kata ya Kihurio. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ile Shule ilijengwa, aliisimamia Mkurugenzi Vizuri sana na shule ile ikawa mpya. Madarasa tisa yalipokwisha sasa nakwenda kuona shule, Madawati! Ile shule iliyokuwa imechoka Madawati yalikuwa ni Magogo, yalikuwa ni madawati yaliyochoka, nimeshindwa kuingiza hayo magogo kwenye shule mpya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwenyewe kama Mbunge nimetengeneza madawati ya madarasa tisa kwa sababu nimeona niisaidie Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, imenipa Milioni 100 na mimi Mbunge niliyechaguliwa na wananchi nikafanya kidogo, nikafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiambie TAMISEMI, tumewashukuru mlivyotuletea hii pesa, tunaomba mpange vizuri mlete pesa za Madawati. Nina uhakika sio kwangu tu

kwa sababu ninaangalia mitandao ninaona ni sehemu nyingi sana. Sasa hilo limekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge mnisikilize kidogo, sasa naomba niongee na watanzania, naomba niongee kwa unyenyekevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nje watanzania wamekasirika sana lakini naomba niwambie watanzania kitu kimoja, Rais amechukizwa sana. Vilevile watanzania naomba niwambie jambo la tatu, Waheshimiwa Wabunge wote hapa ndani wamechukizwa waliposikia Rais akikabidhiwa ile ripoti ya CAG tarehe 29/3/2023 kila mtu alichukizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwambie Watanzania kitu kimoja, hizi shughuli kubwa kama hizi sisi Wabunge tunazifanya kwa utaratibu. Wananchi nje wanaona kama wabunge mbona hawasemi? Tunakwenda kwa utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba uniruhusu suala la CAG liko hapa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Suala la CAG sisi Wabunge tunakwenda nalo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 143(4) naomba uniruhusu kunukuu; “Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atawasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa kwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hii. Baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa hiyo na itabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku 7 tangu siku ile kilipoanza kikao hicho kuketi. Iwapo Rais hatachukua hatua za kuwasilisha taarifa hiyo kwenye Bunge basi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu atawasilisha taarifa hiyo kwa Spika wa Bunge au Naibu Spika ikiwa kiti cha Spika ki wazi wakati huo au ikiwa kwa sababu yoyote Spika hawezi kutekeleza shughuli za kazi yake ambaye atawasilisha taarifa hiyo kwenye Bunge” mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Spika wa Bunge anapokea taarifa ya CAG kesho, ikiwa na maana nataka kuwambia Watanzania taarifa hiyo haijaingia hapa Bungeni. Watanzania wajue kitu kimoja ambacho na sisi Wabunge tunakijua, Rais Samia Suluhu Hassan anahangaika mno kutafuta pesa kwa ajili ya maendeleo ya watanzania. Hawezi kukubali watu…

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni taarifa? Haya nakaa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba si tu kwamba hayajafika Bungeni lakini kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Ukaguzi Kifungu cha 39(1) baada ya kuja Bungeni taarifa ya CAG ndiyo itakuwa public document na hata sisi Waheshimiwa Wabunge ndiyo tutaweza kuisoma in details taarifa yote na kila kitu kilichosemwa na CAG.

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeipokea na kijana ameidadavua ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni lazima watanzania labda hawaelewi. Wakilalamika kwamba Wabunge hawasemi ni vema tuwambie kwamba tunafuata taratibu. Taratibu zitakpofika watanzania wawe na uhakika hakuna atakayepona. Rais hatakubali, Wabunge hatutakubali, sisi hatutakubali ambaye kweli tutakuwa tumehakikisha amechezea pesa za watanzania akaendelea kuzunguka kwenye nchi hii hapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba na ninawaomba Watanzania kwa unyenyekevu waturuhusu sisi tunaowawakilisha tufuate utaratibu tusifanye kazi kinyume na utaratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo naomba kuunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)