Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Mama yetu mpendwa, mama msikivu na mwenye huruma Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa uongozi makini na uwazi wenye kujali maslahi ya wananchi, nampongeza sana.

Pia nampongeza sana Waziri wa Maji Mheshimiwa Juma Aweso, Naibu Waziri Engineer Maryprisca Mahundi na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha Watanzania wanapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi na mafanikio yaliyopatika katika utekelezaji wa miradi ya maji katika mkoa wangu wa Singida bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama katika mkoa wangu wa Singida hususan maeneo ya vijijini na hii ni kwa sababu wananchi wengi wanatumia visima virefu na vifupi katika kupata maji kwa matumizi yao ya kila siku.

Mheshimiwa Spika, jiografia ya mkoa wa Singida ni kame hivyo ni lazima kuwa na chanzo cha uhakika wa maji ambacho kitawezesha wananchi wa mkoa wa Singida na viunga vyake kupata maji safi na salama wakati wote kwa uhakika, hivyo naiomba Serikali iangalie Mkoa wa Singida kwa jicho la kipekee katika suala zima la upatikanaji wa maji.

Mheshimiwa Spika, nipongeze sana mkakati wa Serikali wa kutoa maji kutoa chanzo cha Ziwa Victoria ambao kwa sasa maji hayo yamefika Wilaya yangu ya Iramba katika Mji wa Shelui, naishukuru Serikali na kuipongeza sana lakini niiombe Serikali iyafikishe maji hayo Makao Makuu ya Wilaya ya Iramba, Mji wa Kiomboi ambao una changamoto kubwa ya upatikanaji wa vyanzo vya maji endapo maji hayo yatafika Kiomboi itakuwa ni faraja kubwa kwa wananchi wa Vijiji vya Urughu, Mntenkente na Kizaga, lakini maji hayo pia yafike hadi Wilaya nyingine za Singida zikiwemo za Singida Vijijini, Mkalama, Ikungi, Singida Mjini na Manyoni ili ziweze kupata maji ya uhakika.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia ni mradi wa visima ishirini kwa Wilaya ya Ikungi ambavyo kwa sasa vimekamilika lakini visima hivi havina miundombinu. Ombi langu kwa Wizara kwa kuwa visima hivi vimechimbwa kwenye vijiji na vijiji hivyo vina vitongoji ambavyo vipo mbali na sehemu kisima kilipochimbwa uwepo wa visima hivyo hautakuwa na maana endapo visima hivyo havitawekewa miundombinu.

Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kuwapongeza sana watendaji wa RUWASA ambao wamekuwa wakifanya kazi nzuri katika mkoa wangu wa Singida. Nawapongeza sana lakini pamoja na pongezi hizo RUWASA Mkoa wa Singida inakabiliwa na uhaba mkubwa wa watumishi, kuna uhaba wa watumishi 42 pamoja na vitendea kazi, magari yaliyopo katika Wilaya zangu zote ni mabovu, ni gari moja tu ambalo ni zima. Je, kutakuwepo vipi na ufanisi wa utekelezaji endapo vitendea kazi muhimu kama magari hakuna? Hakutakuwa na ufanisi.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali ituongezee wataalam na vitendea kazi vya kutosha ili kazi za utekelezaji wa miradi ya maji hususan maeneo ya pembezoni ufanyike kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya yangu ya Mkalama ipo miradi ambayo utekelezaji wake ulianza mwaka 2014 lakini miradi hii mpaka leo hii haijakamilika na miradi ambayo imetumia fedha nyingi za walipakodi. Miradi hii ni mradi wa Gumanga wa vijiji vitano, mradi wa maji wa Nyaha ambao umetumia shilingi milioni 900 lakini nao haujakamilika, hapa niishauri Serikali nikiamini Serikali yangu ni sikivu, iundwe kamati kutoka Wizarani ili kubaini ni kwa nini miradi hii mpaka sasa haijakamilika? Pia ili kubaini nini changamoto ya kutokukamilika kwa miradi hiyo wakati wananchi wanaendelea kuteseka kwa kukosa huduma ya maji?

Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa kuendelea kutenga fedha katika Mradi wa Maji Kintinku - Lusilile wa vijiji kumi na moja na kwa kuwa mradi huu ni wa muda mrefu na wananchi wamesubiri kwa muda mrefu kupata huduma hii muhimu ya maji na kwa kuwa maeneo ya kata ya Kintinku, Maweni na Makutopora maji yake ni ya magadi na hayafai kabisa kwa matumizi ya binadamu na kwa kuwa wananchi hutembea zaidi ya kilometa tano kufuata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, niiombe na kushauri Serikali itenge fedha za kutosha katika mradi huo ili umalizike na wananchi wafurahie uwepo wa Serikali yao ya Awamu ya Sita ambayo ni sikivu sana!

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi na naunga mkono hoja.