Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, nami nichangie hotuba ya Waziri wa Maji. Awali ya yote niwashukuru wananchi wa Jimbo la Ngorongoro kwa kunichagua kwa kura nyingi sana.

Mheshimiwa Spika, nami niungane kuwapongeza timu nzima ya Wizara ya maji kuanzia Waziri Mwenyewe, Makatibu Wakuu, na Naibu Makatibu Wakuu, lakini pia nimpongeze Eng. Andrew ambaye ni meneja wa RUWASA Wilaya ya Ngorongoro. Pamoja na mazingira ya Wilaya yetu na kutokuwa na vitendea kazi kwasababu hawana gari kwa sasa kwasababu gari yao waliyokuwa wanaitumia ni mbovu; na unavyojua Wilaya yetu ya Ngorongoro ukitoka Kata moja kwenda Kata nyingine unatumia zaidi ya kilometa 70 hadi
100. Kwa hiyo ni lazima tuwatafutie vitendea kazi ili waweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti iliyopita mwaka 2021/2022 Wilaya yetu ya Ngorongoro tulitengewa bajeti ya Shilingi bilioni 7.1 lakini mpaka ninavyozungumza tumepokea Shilingi 1,200,000,000 tu kwa ajili ya miradi ya maji. Sasa tumebakiza mwezi mmoja kwa ajili ya kukamilisha mwaka wa fedha.

Mheshimiwa Spika, tushukuru kwamba tumepata kiasi hicho, lakini kiuhalisia tukijaribu kuangalia, kwasababu tuna miradi 13 inayoendelea mpaka sasa hivi; lakini fedha zilizotengwa pia kwa mwaka 2022/2023 zimetengwa Shilingi bilioni 1.9; na kabla hatujamaliza mwaka huu bado tunadai zaidi ya Shilingi bilioni sita na fedha ambazo hazijaenda kwa ajili ya miradi ya maji inayoendelea kule Wilaya ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Spika, je, tunategemea nini? Kwasababu leo tunawadai Shilingi bilioni sita ya bajeti iliyopita maana yake sasa miradi inayoendelea pale kwenye Wilaya ya Ngorongoro ni miradi ambayo tutaenda kuiona kama ni White Elephant Projects. Kwasababu kama hatupeleki fedha kila siku labda tunapeleka kwa mradi wa Shilingi milioni 300 tunapeleka Shilingi milioni 50 itawezesha wananchi kupata maji? Na ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi inasema kwamba ifikapo mwaka 2025 vijijini tuwe na asilimia 85 ya watu wanaopata maji na mjini ni 95. Kwa mtindo huu wa kuweka bajeti halafu tunapeleka a little amount of money tutatekeleza kweli miradi hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini suala lingine, ukijaribu kuangalia miradi mingi ambayo imetekelezwa; Mheshimiwa Aweso nikukumbushe tu na nikupongeze pia, kwamba umeweza kufika kwenye mradi wa vijiji nane ambao ni mradi maarufu sasa hivi Ngorongoro. Mradi huo umeanza tangu mwaka 2018 lakini mpaka leo bado tunajenga chanzo tu. Niombe tu, kwamba tutenge fedha za kutosha ili tuweze kumaliza mradi huo wa vijiji nane ambao ni maarufu kwa jina la mradi wa Mageri.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali, kama kweli tunataka kuwasaidia wananchi, akina mama kwenye vijiji na kwenye vitongoji kwenye kata za Enguserosambu, Tinaga, Digodigo na kata nyingine zilizopo karibu kwa ajili ya mradi huo akina mama wanateseka kwenda kuchota maji mtoni kila siku, wanateseka kufuata maji usiku na mchana; kama kweli tunawapenda wananchi wetu na ni kweli kwamba tunataka nao waondokane na umaskini tuwaletee maji ili muda wanaotumia kwenda kuchota maji mtoni watumie kwa ajili ya shughuli nyingine za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini suala lingine ambalo linatokea, sisi wafugaji tunahitaji maji kwa ajili ya binadamu pamoja na mifugo. Kwenye Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi inasema kwamba tutajenga mabwawa kwa kila Wilaya, lakini Wilaya yetu ya Ngorongoro hakuna hata bwawa moja, ukienda pia Longido hakuna hata bwawa moja. Tunahitaji kujenga mabwawa kwa ajili ya mifugo ambayo kwa sisi tunaweza kutumia yale mabwawa kwa ajili ya mifugo pamoja na binadamu. Sisi wakati wa mvua tunaweza tukapata maji, kuna maeneo mengi. Kwa mfano Kata za Malambo, Oloipiri pamoja na Maalon hawana maji; na kata nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi Wilaya yetu tuna vijiji 65 lakini vijiji ambavyo vinapata maji angalau ni 34, vijiji 28 vinapata maji ambayo si toshelezi na vijiji zaidi ya 13 havina maji kabisa. Kwa hiyo niiombe Wizara tuangalie namna ya kuwasaidia wale wananchi nao waweze kupata maji ya kunywa.

Mheshimiwa Spika, lakini suala lingine, kule Loliondo wananchi wanapata maji Unit moja kwa shilingi 2,500, hicho ni kiasi kikubwa sana. Mama zetu na watu wengine wameamua kurudi kwenda kuchota maji mtoni kwasababu hawawezi kumudu gharama ya maji. Wakati mwingine wanasema wasimamizi wanaweka bei ambazo wananchi hawajui. Kwa hiyo tuombe, kama ikiwezekana wizara ijipange zilete zile pre-paid meters ambazo zitawasaidia Watanzania kuibiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini suala lingine mimi niombe na nisisitize sana. Fedha hizi ambazo zilitengwa kwa bajeti ya mwaka 2021/2022, nikuombe sana uweze kuangalia angalau hata tupate fedha kwaajili ya miradi inayoondelea. (Makofi)