Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumpongeza Rais wetu mama yetu mpenzi, kwa jinsi ambavyo anatekeleza ahadi yake ya kumtua mama ndoo kichwani kwa vitendo. Tumeshuhudia jinsi ambavyo ametoa fedha kwa asilimia 95 kwa Wizara hii. Ni pongezi kubwa sana tunamshukuru mama Mwenyezi Mungu aendelee kumbariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na wenzangu kuwapongeza Wizara, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri lakini na Katibu Mkuu Engineer Sanga. Kwa kweli Wizara hii imekuwa faraja kwetu. Tunapokwenda pale hata kama hujapewa fedha lakini unaondoka umecheka ni wakarimu ni Rahim wanatujibu vizuri wanatusikiliza; kwa kweli endeleeni kupiga kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza sana Engineer Mwenda wa Mkoa wa Kigoma kwa ushirikiano anaotupa pamoja na watendaji wake wote; Engineer Aida, Engineer Almasi wanafanya vizuri sana pale katika Jimbo la Muhambwe kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuishukuru Serikali kwa miradi ya maji vijijini ambayo imetekelezwa katika Jimbo la Muhambwe. Tumeupokea mradi wa maji katika Kijiji cha Mkarazi wenye thamani ya bilioni 1.2. Tumeupokea mradi wa maji katika Kijiji cha Mkabuye wenye thamani ya bilioni 1.4. Tumepata maji katika Kijiji cha Buyezi wenye thamani ya milioni 230. Isitoshe tumepata pesa kutokana na pesa za UVIKO, milioni 500 ambazo zimekwenda kutekeleza maji katika Kijiji cha Mshwagule. Tumepata pia milioni 500 ambazo zimetekeleza mradi wa maji katika Kijiji cha Samvura, Kata ya Mnyambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo bado nina vijiji 11 mbavyo havina maji. Hivi ni vijiji vya Kumkuyu, Rubunga, Kukinama, Magarama, Kigina, Nyaruranga pamoja na Kasana. Nimepitia bajeti hii tunayokwenda kuipitisha sasa na mimi nitakwenda kuipitisha kwa kiwango cha hali ya juu, nitaiunga mkono kwa sababu, nimeona nimetengewa maji katika vijiji vitatu, Mikonko, Magarama na Lukaya ambayo itagharimu takribani bilioni 1.7. Naishukuru sana Serikali kwa kuendelea kulijali Jimbo la Muhambwe. Naishukuru sana Serikali kwa kuendelea kumtua mama ndoo kichwani kwa vitendo katika Jimbo hili la Muhambwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo niishauri Serikali. Miradi hii ya vijijini scope yake imekuwa ndogo; kwa maana kwamba tunapata yale maji na tunapata yale magati, lakini watumiaji wale wa magati wanakuwa wengi na bado hatujawa na mtandao katika vijiji vyote. Hii inasababisha miradi hii kuharibika kwa haraka hasa uchakavu wa mabomba. Sasa, niiombe Serikali katika miradi hii ya vijijini tujitahidi kusambaza maji vijijini ili tufikie lengo la mwanamke asitembee zaidi ya mita 200 kufuata maji, ili kupunguza uharibifu wa haya mabomba, lakini pia kupunguza mwendo mrefu wa mama kwenda kwenye kituo cha kuchotea maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile niishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kutuletea wataalam katika hivi vituo. Wote ni mashahidi, changamoto ya maji vijijini ni kuwa na jumuiya za watumia maji hazina wataalam. Kwa hiyo, kwa kitendo hiki cha kutuletea wataalam kwenye jumuiya za watumia maji inatupa uhakika kwamba maji yapatikana. Kwa mfano kule kwangu Kumuhasha tunakaribu miezi sita hatupati maji kwa sababu tu hatuna mtaalamu mahali pale. Kule Malolegwa hatupati maji kwa sababu hatuna mtaalamu. Kwa hiyo, kwa kuja na suluhisho la kuwa na wataalamu kwa jumuiya za watumia maji tutakuwa na uhakika wa kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunayo Mamlaka ya Maji Mjini; niendelee kuishukuru Serikali kwa jinsi ambavyo imetusaidia. Ni mwaka mmoja sasa tulikuwa na asilimia 27 ya huduma za maji. Unaweza ukaona jinsi gani ilikuwa ni changamoto maji Kibondo Mjini nah ii ilikuwa ndio fimbo ya kumchapia Mbunge, hatuna maji. Nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa jinsi ambavyo imetusaidia, imetupatia milioni 595 tumejenga chujio pale mto wa Mgoboka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo, imetupatia tena milioni 590 ambazo tumekwenda kununua pump na mabomba kwa ajili ya kuongeza mtandao wa maji Kibondo Mjini. Tunakwenda kuongeza mtandao wa maji kwa kilometa 11.9 ambazo zitatupa faida kwa watumiaji 550. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hivyo tu, tulukuwa na deni kubwa sana la umeme kwenye vyanzo vya maji, milioni 283. Serikali imetusaidia imetulipia deni na sasa tumebaki na milioni 104 ambazo tunaamini Serikali hii ni sikivu, Serikali yetu ya mama yetu Samia Suluhu Hassan, itakwenda kutusaidia kumalizia hizo milioni 104. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeshapata yote. Tumepata chujio, tumepata mabomba, tumepata na pump za ku-pump, maji haya tutayapeleka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali itusaidie. Ombi letu tunaomba tupate tank la kuhifadhia haya maji ili tuweze kuyasambaza. Tumeshaleta maombi, tunaomba tank la lita milioni 100.5 ambalo litagharimu bilioni 1.1. Ombi langu, naomba mtusaidie ili tuweze kutoka kwenye asilimia hizo tulizokuwanazo, maana baada ya kutusaidia tumetoka 27 tuko 56 na tunalenga na sisi tufike huko 74 ambazo sinasemwa kwamba, ni za kitaifa. Sasa ili na sisi tufike kule tunaomba na sisi tupate tank la maji la thamani hiyo ya bilioni 1.1 ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, waswahili wanasema kushukuru sana ni kuomba tena. Niendelee kuiomba Serikali itusaidie wataalamu; mamlaka zetu hazina wataalam, hatuna technical staff pamoja na wahasibu. Ma-engineer hawa, Engineer Aidan na Almas wanakimbia sana. Mkiwaongezea hawa wataalamu basi kazi itafanyika vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niombe Serikali itusaidie miradi hii imetekelezwa kwenye maeneo ya watu ambao wanahitaji fidia. Katika Kituo kile cha Kumwai mradi huu umetekelezwa kwenye eneo la watu ambao wanadai fidia, milioni nane. Serikali haishindwi naomba mtusaidie. Familia hizi za akina Hamisi Omary na wenzake kila nikifika jimboni, mama tusaidie; na mimi nakuja leo kuiomba Serikali, naomba tuwalipe fidia wananchi hawa wa Kumwai ambao miradi hii ilitekelezwa kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niombe vitendeakazi. Jamani Jimbo la Muhambwe ni jimbo lililoko pembeni, tunaomba magari tupate japo gari moja liweze kutusaidia tuweze kutembelea hivi vijiji ili utendaji kazi wa ma-engineer hawa uweze kuboreka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imelea bajeti kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa. Na mimi nichukue nafasi hii kuiomba, tuna ahadi ya Mheshimiwa Rais, hayati Magufuli, ya kujengewa bwawa katika Kata ya Busunzu. Naona sasa ni muda muafaka madam tumetenga bajeti basi na mimi naomba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Florence Samizi kwa mchango wako.

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)