Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba pia nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii.

Lakini kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na wizara nzima kwa kazi nzuri wanayoifanya, nawapongeza sana; sisi ambao tumekuwa tukiomba maji kwa miaka mingi tangu Bunge lililokwisha mpaka sasa tunaona kazi kubwa ambayo Serikali inafanya kwa sababu kuna sehemu maji yamefika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Geita Mjini inaaminika kwamba ni miongoni mwa miji inayokua kwa kasi zaidi Kusini mwa Jangwa la Sahara. Sababu za kukua kwa Mji wa Geita ni uwepo wa shughuli nyingi zinazohamasisha watu kuja, za kiuchumi, ikiwemo madini. Ongezeko la watu linaongeza sana uwekezaji; na kwa bahati nzuri sana ni kwamba Mji wa Geita Mjini maji yako km 8 kutoka katikati ya mji kwenda Ziwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nianze kuishukuru sana Serikali. Kwanza katika ukurasa wa 53 Serikali inasema mchakato mzima wa miji 24 umekamilika na kwamba sasa utekelezaji utaanza tunakushukuru sana. tunamshukuru Mheshimiwa Rais tulimsikia siku ya wiki ya maji; na tunaamini kwamba kabla Bunge hili halijaisha Mheshimiwa Waziri tunaamini Mheshimiwa Rais atatuzindulia mradi huo uweze kuanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali pia tumepata fedha kwa ajili ya kupanua chanzo cha maji; na naomba nitumie nafasi hii kuwapongeza sana GEUWASA wanafanya kazi yao vizuri, wanafanya kazi yao vizuri katika Mji wa Geita na kwa kweli wanastahili pongezi.

Sasa tunapanua chanzo cha maji umetupa bilioni moja, tunashukuru sana. Lakini yale maji yanatoka Nungwe; yakitoka Nungwe yanapita Manga, Nyakabale na kwenye Kata ya Mgusu. Kule yanapotoka maji, maji wanayopata ni yale ambayo hayajasafishwa; yanayovuja kwenye bomba ambalo linatoa maji ziwani; kwa hiyo, ili wapate maji safi inabidi maji yafike Geita Mjini halafu yarudi km 8 kule yanakosafishwa, kule hakuna usambazaji wa maji. kwa hiyo Mheshimiwa Waziri pamoja na sifa hizi za GEUWASA nadhani GEUWASA wanastahili kuongezewa fedha ili wapeleke mtandao wa maji na salama kule yanapotoka maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya Mji wa Geita ni takribani lita milioni 18 mpaka milioni 20. Sasa hivi tunapata lita milioni tano. Kitakapotanuliwa hiki chanzo cha maji tunaamini kitatusogeza karibu lita milioni 8, bado tutakuwa na gape ya takriban lita milioni 12. Jambo pekee ambalo linanipa faraja ni kwamba utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji unaanza. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana kwa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri naomba kuishukuru Serikali, mwaka huu wa fedha unaokwisha tulipata fedha na tumepeleka maji katika mitaa takriban 12; na tumejenga matenki mapya takriban matatu. Sasa nimeona kwenye bajeti yako ya sasa unatupatia fedha kwa ajili ya kuongeza usambazaji wa maji kwenye Kata za Shiloleli na Bulela.

Mheshimiwa Waziri zipo kata zingine ambazo tumetafiti maji ya visima yamekosekana; pamoja na kusubiri maji ya bomba Kata za Nyanguku na za Ihanamilo kila walipochimba visima RUWASA walikosa maji. Sasa niombe, wakati tunasubiri mradi huo ambao utachukua takriban miaka mitatu, wananchi hawa, kama unavyosema mwenyewe Kwamba hakuna mbadala wa maji, waweze kutafutiwa njia nyingine ya kupata maji salama na safi kwa ajili ya maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo, ni kwa sababu kila inapofika kiangazi, wananchi wa Kata za Nyanguku na Ihanamilo wanaanza kusafiri kutafuta maji kama vile wanavyosafiri watu wa Mikoa ya nchi kavu kama Shinyanga na wapi huko na matela ya ng’ombe kwenda kutafuta maji kwenye mabwawa; lakini sisi tupo kilomita nane kutoka ziwani. Kwa hiyo naamini kwamba, jambo hili linaweza kutafutiwa ufumbuzi katika kipindi hiki ambacho Serikali bado haijasaini na hatujaanza mkataba huo mkubwa wa kupeleka maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri juzi niliuliza swali hapa na ulisema kwamba Serikali itaanza mchakato kwa ajili ya ukarabati wa bwawa la Kasamwa, nashukuru sana nimeona kwamba mchakato huo utaanza. Mji wa Kasamwa ni Mji wa pili kwa ukubwa katika Jimbo la Geita Mjini; tuna watu takribani 25,000 mpaka 30,000. Vilevile ni mji ambao unashughuli nyingi za kiuchumi. Tuna maji ya visima, maji ya bomba ya kutoka Ziwa Victoria hayajafika. Tunashukuru kwenye mpango maji yatafika kwenye Mji wa Kasamwa. Kwa hiyo, ombi langu hapa ni kwamba katika fedha hizi chache ambazo tutapata mtuongezee fedha ili huu Mji wa Kaswamwa mtandao wa maji haya ya visima pamoja na kwamba kuna kisima Kanyala na kuna tenki limejengwa pale maji yawafikie wananchi takriban 30,000 ya huu Mji Mdogo wa Kaswamwa. Kwa sababu huu mji ni mkubwa na kama visima hivi viwili vilivyopo vitaendelea kuwepo, uwezekano wa kiangazi maji yanapopungua kupata shida ya maji ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, naamni kwamba kama ambavyo watu wote wamekupongeza; wananchi wa Geita Mjini wana matumaini makubwa na wizara yako na kazi nzuri unayoifanya wewe na Naibu wako. Tunaomba tu Mheshimiwa Rais aturahishie mradi wa Miji 24 ili tuweze kupata maji safi na salama. Nashukuru sana.(Makofi)