Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kunipa nafasi hii ya kuwa mmoja wa mchangiaji katika wizara hii muhimu ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake za makusudi za kwenda kutatua changamoto za maji katika nchi yetu ya Tanzania na majimbo yote ya Tanzania likiwemo Jimbo langu la Igalula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nimshukuru na nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa jitihada na kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya. Shukrani hizi zienda kwenye Wizara nzima ya Maji, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu; kiukweli mimi wamekuwa wakinipa ushirikiano mkubwa pindi ninapopata changamoto kwenye miradi yangu ambayo nitaitaja hapo baadaye. Nikiwa nawakimbilia basi wao wananipa ushirikiano na changamoto hizo kuzitatua. Mimi niwashukuru sana, endeleeni kutulea na endeleeni kutusikiliza kwa sababu sisi tumeletwa hapa kwa nia ya kuwatetea wananchi na wananchi tukileta shida zao kwenu na nyie mnazitatua kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo ngazi ya Wizara pia niwashukuru viongozi ambao wao wanawasaidia kutatua changamoto katika mikoa yetu na wilaya. Nimshukuru Meneja wa RUWASA mkoa wetu wa Tabora Ndugu Kapufi, anafanya kazi nzuri sana na ndio maana mkoa wetu umeheshimika kwa kuwa wa kwanza kitaifa kwa kutoa huduma bora ya maji.

Nimshukuru Meneja wetu wa Wilaya Mr. Shibiki, kiukweli anafanya kazi kubwa sana. Kuna kipindi Mheshimiwa Waziri nilikuwa meneja huyu amekosa usafiri lakini kwake usafiri haukuwa kigezo kutokufika site, alikuwa anatuma mpaka bodaboda ili aweze kwenda kutatua na kusikiliza kero ambazo zilikuwa zinawakabili wananchi. Nilikuja kwako na umeshanipa ahadi yakuniletea gari basi ninaami akipata gari changamoto zote za maji katika jimbo langu litakuwa limetatulika kwa asilimia kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninayo mambo machache sana nimempongeza Mheshimiwa Waziri na niendelee kukuomba tena. Tarehe 29 mwaka 2021 niliuliza hapa swali la msingi kuhusu Wizara ya Maji, niliuliza kuhusu Mradi wa Ziwa Victoria ambao unaendelea katika Jimbo la Igalula ambapo utatatua changamoto katika kata nne za Goweko, Igalula, Kigwa na Nsololo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kupitia majibu yako, na siku hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri hakuwepo, ulijibu wewe mwenyewe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Maji; uliniambia mradi huu utakwenda kukamilika kabla ya mwaka wa fedha 2022 kuisha. Leo tumebakiza siku kama arobaini na tano mwaka wa fedha uishe lakini mradi ule huko katika asilimia thelathini kwenda arobaini, na haujafika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri; lengo la huduma na limeshaonyesha dhamira kwa sababu mradi huu umeanza; na juzi hapa Mheshimiwa Mkuu wetu wa Mkoa alikuja na viongozi wa chama tukaja ofisini kwako tukafanya kikao na wataalam. Kulikuwa changamoto ya ulipaji baadhi ya certificate. Siku ileile ulitoa maelekezo na certificate zililipwa na yule mkandarasi alileta mabomba yako site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, palikuwa na changamoto ya mkandarasi wa kuchimba msingi kwa sababu ya masika. Sasa, masika imekwisha na sasa mmuagize arudi site aendelee na kazi ili kuwafikishia maji wananchi wa Jimbo la Igalula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe jambo lingine Mheshimiwa Waziri. Hii mikataba ambayo wanatuletea kule inakuwa na mkanganyiko mkubwa sana. Unakuta mtekelezaji ni RUWASA kule ngazi ya wilaya lakini anayetumika kununua mabomba ni anatoka Makao Makuu yani Wizarani sasa mnakuwa mtu wa wizara atambui umuhimu wa adha anayoipata kule Meneja wa RUWASA wa wilaya na wa mikoa. Sasa ninyi mna-relax kwa sababu ya ucheleweshaji wa kulipa certificate hasa ususani wa supply ya vifaa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri, kwenye mradi wangu aliniahidi ataenda kuongea na supplier alete mabomba yote lakini jambo lile bado halijafanyika. Nimbuombe atakapopata muda amuite supplier huyo alete, na asianze kutupa vigezo, kwamba akifikisha kilometa haleti vifaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine, Mheshimiwa Waziri tuna mradi ambao wewe ulikuwaga Naibu Waziri wakati huo waziri Professor Mbalawa mlikuja katika Kata ya Tura pale mwaka 2019 mkaahidi kwamba ku- supply katika Mji wa Tura utakamilika baada ya miezi mitatu. Tangu mwaka 2019 mpaka leo ule mradi haujakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini changamoto si mameneja wangu wa Wilaya na Mkoa, changamoto iko katika hatua ya manunuzi ngazi ya Taifa. Niombe Mheshimiwa Mheshimiwa Waziri waendeni wakatatue changamoto hii. Wananchi kila siku nikienda kule wananiuliza ni lini sasa kitendawili naomba ukakitatue ili waweze kupata maji katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la tatu ambalo nilitaka nishauri, na niombe Mheshimiwa Waziri mwaka jana aliniahidi kuwa usanifu wa bwawa la Kizengi umekamilika, lakini kwenye bajeti hii nimefungua vifungu vyote na majedwali yote sijaona amelipangia fedha. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, Jimbo la Igalula lina changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji. Nishukuru kwenye fedha za UVIKO nilipata milioni 505 ambazo zitawezesha kuchimbwa visima 15; lakini kwa takwimu mpaka sasa hivi vimechimbwa visima sita ambapo katika Vijiji vya Kalangatu, Mwisolo pamoja na Isaga wamechimba wamekosa. Ni vijiji vitatu tu ambako wamechimba maji wamepata ambavyo ni Vijiji vya Kalangale, Mwamabondo na Mwamdalaigo, wamechimba maji wamepata lakini si mengi sana. Kwa hiyo ukiangalia jiografia ya Jimbo la Igalula maji ya visima si muhimu sana. Ili kutatua changamoto hizo ni kuwepo kwa upatikanaji wa maji ya mabwawa. Nimuombe; kwenye Bwawa la Kizenji usanifu umekamilika; sasa anipelekee fedha ili zikatatue asilimia zaidi ya 80 ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Jimbo la Igalula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru juzi ameniletea wasanifu wengine waliokwenda kufanya usanifu kwa ajili ya kujenga Bwawa katika Kata ya Miswaki. Hata hivyo solution ya Jimbo la Igalula ni kuniletea mabwawa na si visima. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri pamoja na jitihada kubwa unazozifanya za kumsaidia Mheshimiwa Rais za kuweza kwenda kutatua changamoto ya maji miradi iliyoanzishwa awali naomba iende ikakamilike kwenye mwaka huu wa fedha ili, wananchi wetu waone yale maneno wanayosema Mheshimiwa Rais akiwa kwenye majukwaa na mikoa mbalimbali basi yawafikie wananchi wetu wa Jimbo la Igalula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja na niwapongeze wizara iendelee kufanya kazi nzuri. Ahsanteni sana.