Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Mimi pia, kama ilivyo ada, naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wengineo. Kwa ujumla wake Mheshimiwa Waziri wewe ni mtu rahimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo mimi nitajielekeza zaidi katika suala la uendelezaji wa rasilimali za maji na utafutaji wa vyanzo vipya. Eneo kubwa nita- concentrate hapo lakini niishukuru Wizara kwa ujumla wake. Najua sisi kwa maana ya Mpanda mahitaji ni lita 11,370,000 lakini tunapata lita 6,050,000. Tuna upungufu wa lita 5,320,000. Hiyo ndiyo sura ya suala la maji pale kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema nitakuwa si muungwana nisiposhukuru. Nafahamu kwamba kwa muda wote huu tuna Miradi ya Ikorongo Namba Moja na Ikorongo Namba Mbili. Vilevile kuna Mradi wa Manga ambao takribani shilingi bilioni 7.5 tumeletewa kutoka Serikalini. Lakini pia niishukuru kwa maana ya miradi mitatu. Tuna Mradi mmoja wa Mwamkulu ambayo hiyo Mwamkulu inakwenda Mkwajuni, Mlima Kipara na St. Maria. Tulipata fedha za UVIKO ambayo ilikuwa ni takribani shilingi milioni 476. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tuna mradi wa Kakese ambao ni Mfuko wa Maji wa Taifa, tulibahatika kupata shilingi milioni 951. Tunao mradi wa Milala kwenda Kampuni, tulibahatika kupata shilingi milioni 458. Hizo zote kwa ujumla wake nimshukuru Mheshimiwa Waziri. Isipokuwa, maombi yetu mapya kwako Mheshimiwa Waziri, tunaomba shilingi milioni 572 ili kuweza kumalizia mradi wa Kakese wenye thamani ya shilingi milioni 412 na Shilingi milioni 160 Mradi wa Milala kwenda Kampuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo natamani nilete picha kwa hili jambo ambalo nilisema, ramani ya mtandao wa maji na masuala ya vyanzo vipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuzungumza hapa. Bahati nzuri Waziri wa Fedha aliwahi kuleta taarifa akielezea wenzetu wa China. Ukiiangalia China pamoja na ukubwa wake lakini wametengeneza mtandao wa maji. Mtu wa Kaskazini ana uwezo wa ku-supply maji mpaka Kusini, mtu wa Kusini ana uwezo ku-supply maji mpaka Kaskazini, likewise Magharibi, Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini; nchi hii kwa ujumla wake ikiwa kuna miradi mikubwa; leo tunatoa bomba la mafuta kutoka Uganda linakwenda mpaka Tanga. Tuna bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam linakwenda mpaka Zambia. Ipate picha hiyo Mheshimiwa Waziri, na nikuombe, unayo nafasi ya kuacha kumbukumbu. Mzee wa Toronto pale Dodoma ameacha kumbukumbu ya miti. Unaouwezo wa kuacha kumbukumbu Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii visima sikatai, mabwawa sikatai. Lakini uwezekano wa kuiunganisha nchi kwa mtandao wa maji upo, tunachotakiwa ni kuthubutu. Bomba linaweza likatoka Dar es Salaam likafika Katavi. Bomba linaweza likatoka Bukoba likafika Mtwara. Inawezekana ni kuthubutu tu; na kupanga ni kuchagua. Lakini unaweza ukapanga kufeli, ukishindwa kupanga umepanga kufeli. Kwa hiyo, mimi niombe sana, na katika hili kuna nchi nyingine hatujafika huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kusema hapa ukienda kwa nchi za wenzetu wana-treat maji ya bahari, hatujafika huko, kwamba nchi hii tufike sehemu labda kama ni Bahari ya Hindi, tuyatoe maji ya Bahari ya Hindi kuyaleta huku, hatujafika hapo, vyanzo vinatosha. Chukua Ziwa Nyasa, chukua Ziwa Tanganyika, chukua Ziwa Rukwa inatosha. Habari ya visima sijataja Victoria na mimi kwa ajili ya uzalendo sioni tabu hata kama maji ya Ziwa Victoria yatamfikia mtu wa Dodoma sawa ni mipango ya ki-nchi. (Makofi)

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Kingu Elibariki.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa mchangiaji taarifa ya kwamba mambo mazito na ya muhimu anayoyazungumza ambayo kimsingi mimi naya-reflect kwamba ni long term plan ambazo Wizara yetu inaweza ikasaidia katika kuleta maendeleo makubwa katika sekta ya maji lakini bahati mbaya sana Wizara ya Fedha nimejaribu kuangalia hapa simuoni Waziri, simuoni Naibu vitu kama hivi vingeweza kusaidia sana angalau kama mmoja anakuwa hayupo basi mmoja awepo kwa ajili ya kuchukua kumbukumbu ya kutengeneza mipango ya muda mrefu ya nchi. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapufi, unapokea taarifa?

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi niseme pamoja na kuongelea mipango ya muda mrefu lakini watu waliofanikiwa duniani ni wenye jeuri ya kuthubutu. Mimi pale kwangu Mpanda tunalo Bwawa la Milala. Bwawa lile limechimbwa miaka ya 1950. Tuna chanzo cha Mto Ugala, Mkoloni kwa ajili ya kuyapeleka maji kwenye uchimbaji wa madini ameyatoa maji Ugala kuyaleta Mpanda Mjini, amechimba Bwawa la Milala uko miaka ya 1950. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama watu wa miaka ya 1950 walikuwa na mitazamo hiyo mipana, vipi kizazi cha sasa hivi? Kwa hiyo, naendelea kuomba hilo. Nishukuru kwa maana na miji 28 na Waziri mimi Mpanda pale najua kwa maana miji 28, mji wangu umeguswa. Nikikataa hicho kidogo nitakuwa mtu wa ajabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia habari ya kuendeleza Bwala la Milala, lakini chanzo cha uhakika ni Ziwa Tanganyika. Niombe sana; na nikilisema hilo liende sambamba kwa Mji wa Mpanda. Ukitumia maji safi inakwenda bila kujiuliza, utazalisha maji taka. Hatuna mfumo wa maji taka. Niombe sana wenzetu wa mipango miji; jamani maji taka bado ni bidhaa muhimu.

Leo mahali kama Dodoma kwa kupitia maji taka, ukizalisha maji masafi mfumo wa maji taka ndio unapendezesha miji. Ukienda miji ya watu wengine hawaangaiki kumwagilia maua na vitu vingine ni kutokana na maji taka. Uki-treat maji taka unapata uwezekano kwanza hamtobanana kwenye kutumia maji safi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuendelee kujipanga huko Mheshimiwa Waziri ili kuhakikisha habari ya maji taka isiwe ni tatizo iwe ni jambo la kuwekwa kwenye mipango yako pia. Miji inakua, Mji wangu wa Mpanda kasi yake ya kukua, na wewe Mheshimiwa Waziri umeshafika pale…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: … Kasi ya kukua ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)