Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sanakwa kunipa fursa hii, kwamba leo nimekuwa mchangiaji wa kwanza katika bajeti hii ya Wizara ya Maji, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla yayote naomba kumpongeza Waziri wa Maji pamoja timu yake kwa kazi kubwa anayoifanya ya kujenga miradi mikubwa na kusimamia kwa weledi mkubwa, nampongeza sana Waziri kazi yake inaonekana na akijua wazi kabisa kwamba maji ni uhai na kwamba amekwishasema maji hayana mbadala na kwakweli anatendea haki, nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba hilo niseme tu, tumshukuru Mungu kwa Tanzania bado tunarasilimali ya maji ya kutosha. Kwa mfano maji yanayoweza kupatikana kwa mwaka ni lita za ujazo bilioni 126, na kati ya hizo bilioni 105 zipo juu ya usawa wa ardhi na bilioni 26 zipo chini ya ardhi; ni maji ambayo yanaweza kupatikana kwa mwaka. Hii inafanya Mtanzania kuweza kutumia maji wastani wa lita 2,250 kwa mwaka, ambapo kiwango cha kimataifa ingekuwa ni lita 1700, na chini ya hapo tungeingia kwenye water stress. Kwa hiyo, tunaona kwamba tunabahati pengine kazi kubwa ni namna gani tunaweza kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili hiyo nitoe wito, nimuombe na Waziri kabisa kwamba tunapaswa kuhifadhi vyanzo vya maji ili kwamba kiwango hiki kiendelee kuwepo. Kwa sababu kwa kuharibu vyanzo vya maji pengine kiwango hiki kinachoweza kupatikana kikapungua. Kwa hiyo, akishirikiana na mabonde ya maji nitoe rai kabisa kwamba hifadhi ya vyanzo vya maji ifanyike ili maji yaweze kupatikana kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo Mkoa wa Manyara una changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji. Wakati tukiongelea kwamba Taifa tunaenda kwenye asilimia 72 pengine na kuendelea, ya coverage ya upatikanaji wa maji lakini Mkoa wa Manyara bado tuna asilimia 58 pengine na chini. Hali hii ni mbaya zaidi kwa maeneo ya pembezoni, maeneo ya kanda za chini na maeneo ya wafugaji maji ni machache na ukizingatia vyanzo vya kudumu za maji tiririka hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba tu-focus sasa ya Waziri iende kwenye maeneo hayo kwa sababu kuna mama zangu kule bado wanatembea kilometa nyingi kutafuta maji. Kwa mfano tu kwenye Wilaya ya Mbulu, ukienda kwenye ukanda wa chini wa Yaeda Chini, Endamilay, Eshkeshi, Masieda hali ya maji kule ni mbaya. Nampongeza kwamba huko pia ameweka bajeti ya kuchimba visima. Mimi nimuombe tu kabisa kwamba fedha hizi azitoe na visima hivi vichimbwe ili mama zangu waliopo kule waki-Wabarbeig, Wakiiraki wapunguze huu mwendo, kwa sababu kule bado kuna kuamshana wakati wa jogoo la kwanza ili kwenda kukinga maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile nimpongeze tu kwa sababu hata Hanang’ ana mpango wa kuchimba visima tisa kwenye maeneo magumu kama hayo. Maeneo ya Endagau, Wareta, Dumbeta pamoja na mengine. Maeneo haya ni korofi kwa upatikanaji wa maji na kwamba hakuna vyanzo vya maji tiririka. Vilevile anampango wa kuchimba visima 13 katika Wilaya ya Simanjiro pamoja na kufanya extension na mradi mkubwa kabisa ule wa Orkesument ambao alizindua Makamu wa Rais kwamba sasa anapeleka maji Ruremo kutoka mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu kabisa kwamba, katika Wilaya ya Kiteto kuna changamoto kubwa ya maji kwa binadamu hata kwa mifugo na ndiyo maana tunapata vifo vingi vya mifugo. Watu wa Kiteto wameomba kuchimbiwa Bwawa kubwa la Dongo. Bwawa hili lipo kwenye mpango wako na ninaona kwamba miongoni mwa mabwawa ambayo umeyatambua kwamba yanaweza yakachimbwa ni pamoja na Bwawa la Dongo. Mimi nikuombe sana, Bwawa hili la Dongo ni suluhisho kwa watu wa Kiteto wameomba zaidi ya miaka minne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na bwawa hili faida yake kwanza ni kunusuru mafuriko yanayotokea kule Dumila. Can you imagine mvua inanyesha Manyara lakini mafuriko yanaenda mpaka Morogoro, ikiharibu mazao ya watu wa Dumila, miundombinu pamoja na watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bwawa hili litakapokamilika lina uwezo wa kusaidia maji katika Wilaya ya Kongwa pamoja na Wilaya ya Gairo; na inakuwa na kazi kubwa, tutapata maji ya binadamu na maji ya mifugo. Mimi unasikia kila siku nikilia na mifugo ya Kiteto inavyokufa wakati wa ukame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile itatumika katika kilimo cha umwagiliaji tukawa na uhakika wa chakula; na tukijua kwamba Kiteto ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula lakini ndiyo yenye idadi kubwa pia ya mifugo. Vilevile itasaidia katika ufugaji wa samani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba hili uliweke katika mpango mkakati kama unavyofanya mikakati ya Farkwa na Kidunda. Hili Bwawa la Dongo ninakuomba sana; litakuwa suluhisho kubwa kwa watu wa Kiteto wote changamoto ya maji itakuwa imeisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ninahamasisha uvunaji wa maji. Nimeona Wizara wamejitahidi wametengeneza mwongozo wa uvunaji wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taasisi zetu maji ni ya shida, na lakini ukiona maji ya mvua ni rasilimali muhimu. Kama tungekuwa na tabia ya kuvuna maji ya mvua tungekuwa na uwezo wa kupata maji ya kutosha na kuongeza kiwango cha maji kinachopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule hizi tunakutana na wanafunzi, unaona wanavyobeba maji wakipeleka shuleni, hatujui wamepata wapi vyanzo hivyo vya maji. Lakini uvunaji wa maji ni project rahisi wana, miundombinu ya kutosha ya paa, kinachotakiwa pale pengine ni kuweka ma- tank ya kuvuna maji na ikawasidia wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye taasisi za afya, ukienda katika zahanati zilizopo pembezoni bado changamoto ya maji ni kubwa na maji ni muhimu sana kwenye taasisi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana, kwa mwongozo huo utaratibu wa uvunaji wa maji katika taasisi uwe kipaumbele na uendelee; lakini utaratibu wa uvunaji wa maji pia kwa wananchi wa kawaida uendelee kuhamasishwa kupitia kwenye halmashauri zao. Maji ya mvua yakivunwa inaweza kuwa suluhisho kwa maji ya mifugo pamoja na matumizi ya binadamu. Sisi tunaona kabisa pengine miradi ya TARURA na TANROADS ikipita wakichimba udongo wao wakaacha yale mashimo kipindi cha kiangazi kinasaidia mifugo, ndiyo maji ambayo yanapatikana.

Sasa kumbe na sisi ukihamasisha wafugaji hata na wakulima wanauwezo mkubwa kabisa wa kuchimba vilambo vidogo vidogo wakaweza kuifadhi maji na kwa hiyo, ikawasaidia kipindi cha kiangazi. Naomba sana, mwongozo huo ukipita kwenye taasisi, lakini vilevile mwongozo huo ufike halmashauri ili wananachi kwa pamoja waweze kuhamasishwa kuvuna maji ya mvua yaweze kutumika kipindi cha kiangazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga hoja mkono kwa mchango wangu. Ahsante sana.