Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii adhimu na adimu kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa kibali cha kusimama mchana huu wa leo mbele ya Bunge lako Tukufu nami niwe miongoni mwa watu wa kuchangia hoja hii ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Spika, kipekee naomba nichukue fursa hii vilevile kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akihutubia Bunge tarehe 22 mwezi wa Nne mwaka 2021 alielekeza mambo mbalimbali ambayo sisi Wizara ya Elimu tunapaswa kuyafanyia kazi; kipekee mwezi wa 10 alipopata fedha zile za UVIKO -19 zaidi ya Shilingi bilioni 304 ambazo aliweza kuzielekeza kwenye sekta ya elimu. Kwa hiyo, katika maono hayo na ndoto hizo hatuna budi kumpongeza kwa karibu sana Mheshimiwa Rais kwa juhudi kubwa.

Mheshimiwa Spika, kipekee naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini, kuweza kumsaidia kuhudumu katika Wizara hii ya Elimu nikishirikiana kwa karibu na Mheshimiwa Prof. Mkenda. Vile vile napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Prof. Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Katibu Mkuu, Prof. Sedoyeka, Manaibu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi na Watumishi wote wa Wizara ya Elimu kwa ushirikiano wa karibu wanaonipa katika kutimiza majukumu yangu ya kila siku.

Mheshimiwa Spika, kipekee nichukue fursa hii vilevile kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Mafia kwa imani yao kubwa na ushirikiano wanaonipa katika kuleta maendeleo katika Jimbo letu la Mafia na kuendelea kushirikiana na kunivumilia katika kipindi hiki chote wakati natekeleza majukumu haya. Mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, familia yangu niweze kuishukuru kwa upendo pamoja na ushirikiano na uvumilivu walionionesha katika kipindi hiki chote.

Mheshimiwa Spika, kipekee naomba nikushukuru wewe Spika pamoja na Naibu Spika na Wabunge wote kwa ushirikiano mnaotupa Wizara ya Elimu wakati tunaendelea kutekeleza majukumu haya muhimu ya Taifa. Baada ya shukrani hizo, sasa naomba nijikite kwenye maeneo machache ambayo ni ya kutoa ufafanuzi kwenye baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wameendelea kutoa tokea jana mpaka siku ya leo mchana.

Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, maoni yenu yote pamoja na mawazo mliyotupa pamoja na mapendekezo, tumeyabeba, tunayachukua, tunaenda kuyafanyia kazi. Vilevile kutokana na muktadha wa muda, tusingeweza kujibu hoja zote hapa leo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie tu kwamba hoja hizi tutazileta kwako kwa maandishi ili ziweze kuwa rejea na kumbukumbu sahihi ya kikao hiki pamoja na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ambalo ningependa kutolea ufafanuzi ni eneo la lishe mashuleni. Imezungumzwa hapa kwamba bila lishe na chakula shuleni inawezekana tendo la kujifunza shuleni likawa gumu. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu, Waraka wa Elimu Na. 3 wa Mwaka 2016 unafafanua vizuri jambo hili la ushirikishwaji wa jamii kwenye eneo la elimu na utoaji wa lishe pamoja na chakula shuleni. Vilevile mwaka huu 2022 sisi kama Wizara tumeweza kutoa mwongozo wa namna gani jamii pamoja na wadau mbalimbali tunaweza tukashirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba tunakwenda kutoa chakula shuleni.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa Wizara yetu ipo kwenye mchakato wa kuhakikisha kwamba tunaenda kutengeneza mpango mkakati namna gani tunatekeleza mwongozo huu. Vilevile tayari tumeshaingia makubaliano na wenzetu wa World Food Program kuhakikisha kwamba kuna maeneo ambayo tunakwenda kuyafanyia kazi na kuona ni namna gani tunaweza tukatekeleza mpango huu wa kuweza kuweka chakula shuleni.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge tunakoelekea ni kuzuri, lakini hili litakuwa na matokeo chanya ikiwa tu tutaweza kushirikiana kwa pamoja kwa sababu, ushirikishwaji wa jamii kwenye jambo hili la utoaji wa chakula shuleni ni jambo la msingi sana kwa sababu, tumeweza kufanya kama pilot kwenye Mikoa ya Njombe pamoja na Kilimanjaro na Mara na imeonesha matokeo chanya. Sasa matokeo yale tuliyoyapata kwenye pilot hiyo yatatusaidia sasa kuenea mpango huu kwenye mikoa yote nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe wito wa ushirikiano, na vilevile tumepanga kuweka kikao kikubwa sana na wadau wote wa elimu kuhakikisha tunakwenda kujadili namna gani mpango huu tunaweza tukautekeleza kwa vitendo kwa manufaa mapana ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo ni eneo la kwanza nikasema angalao tunaweza tukalitolea ufafanuzi wa kina.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo ningependa kulitolea ufafanuzi ni la udhibiti ubora wa shule. Katika eneo hili, ni kweli tunafahamu umuhimu wa udhibiti wa ubora ili kuweza kulinda ubora wa elimu yetu nchini. Kwa kuzingatia azma hiyo, Serikali imejielekeza na kuweka mifumo sahihi, nguvu kazi pamoja na vitendea kazi ili kuhakikisha kwamba eneo hili la udhibiti ubora tunakwenda kulifanyia kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki Serikali imeweza kufanya majukumu kadhaa kuhakikisha eneo hili la wadhibiti ubora linakwenda kukaa sawasawa. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 mpaka 2021/2022 Serikali imeweza kununua magari zaidi ya 84 na kuyasambaza kwenye ofisi zetu za kanda pamoja na zile za Halmashauri ikiwa ni eneo la vitendea kazi kama nilivyozungumza pale mwanzo. Vilevile tumeweza kujenga ofisi kwenye maeneo au Halmashauri ambazo zilikuwa hazina ofisi kabisa, zaidi ya ofisi 155 zimeweza kujengwa kwenye Halmashauri mbalimbali nchini ili kuweza sasa kutengeneza mazingira mazuri ya wadhibiti ubora kuweza kufanya kazi zao vizuri na katika mazingira mazuri na salama.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Serikali imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya kufanya M and E kwa maana ya Monitoring and Evaluation, na kuwafundisha wadhibiti ubora namna bora ya kuweza kwenda kufanya kaguzi mbalimbali kwa ajili ya kudhibiti taratibu za ufundishaji na kujifunza kwenye maeneo ya shule zetu. Pia tumeweza vilevile kufanya ukarabati wa ofisi zaidi ya 31 kwenye maeneo mbalimbali nchini. Tumeweza vilevile kuongeza watumishi kwenye eneo hilo la wadhibiti ubora ambapo zaidi ya watumishi wapya 619 wameweza kupelekwa kwenye ofisi mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha ofisi zinapata rasilimali watu wa kuweza kufanya majukumu hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vitendea kazi, tumenunua vishikwambi au kompyuta mpakato 867, kwa sababu tunajua sasa hivi taratibu na mifumo ndiyo ambayo inafanya kazi zaidi kuliko taratibu za zamani zile za makaratasi. Kwa hiyo, tumeweza kujikita kwenye upande wa mazingira pamoja na vitendea kazi na tunaendelea kufanya maboresho makubwa kwenye eneo hili pamoja na utoaji wa mafunzo kwa wadhibiti ubora ili kuhakikisha kwamba kazi zao wanakwenda kuzifanya sawasawa.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo napenda kutolea ufafanuzi au hoja nyingine ni ya miundombinu. Imezungumzwa sana hapa kuhusiana na suala la miundombinu hasa kwa watoto wetu wenye mahitaji maalum. Naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba katika kuhakikisha taasisi za elimu zinakuwa na miundombinu rafiki kwa makundi yote, Wizara imeandaa mkakati wa ujenzi na utunzaji wa shule unaoitwa School Construction and Maintenance Strategy. Mkakati huu ni wa miaka 10 wa 2019 mpaka 2028 ambao unabainisha viwango vya kuzingatia wakati wa ujenzi na utunzaji wa majengo ya shule pamoja na vyuo mbalimbali ikiwemo kuweka miundombinu ya kuzingatia wenzetu wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, eneo hili hata ukienda sasa hivi kwenye madarasa yetu tunayojenga kwamba, ni lazima zile ramp nazo ziweze kuonekana kwenye maeneo hayo ili kurahisisha wenzetu au watoto wetu wenye mahitaji maalum waweze kufanya mizunguko pamoja na kuingia na kutoka darasani bila changamoto yoyote.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ililetwa mezani hapa nadhani ni muhimu kuitolea ufafanuzi, ni suala la uanzishwaji wa madawati ya jinsia katika ngazi zote za elimu. Jambo hili tayari Wizara tumeshalifanyia kazi, lipo na ilikuwa ni suala tu la utekelezaji. Kwa mujibu wa Waraka wa Elimu Na. 11 wa Mwaka 2002, ulikuwa unaeleza wazi kwamba katika kila shule zetu za msingi na sekondari, kulikuwa kunahitajika au inapaswa kuwa na walimu wanasihi angalao wawili, yaani wa kike mmoja na mwanaume mmoja ambao wataunda Kitengo cha Malezi, Ushauri, pamoja na unasihi shuleni. Kwa hiyo, tunakwenda kusimamia vizuri mwongozo huu, lakini kazi za walimu hawa sasa zimebainishwa waziwazi katika waraka huo.

Mheshimiwa Spika, kazi za walimu hawa wa malezi ni kutoa huduma ya malezi pamoja na unasihi kwa wanafunzi, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha zinazoweza kuathiri kisaikolojia na kiafya ambazo hatimaye huathiri namna ya kujifunza. Kwa hiyo, tunakwenda kusimamia vizuri mwongozo pamoja na waraka huo kuhakikisha kwamba, eneo hili nalo linakaa sawasawa.

Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, imeandaa mwongozo wa uandaaji wa madawati haya ya ulinzi na usalama wa watoto ndani na nje ya shule ambapo waraka huu ni wa mwaka huu 2022. Madawati hayo yatafanya kazi chini ya walimu walezi ili kudhibiti matukio ya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto ndani na nje ya shule. Kwa hiyo, tunakwenda kusimamia vizuri waraka huu kuhakikisha vitendo hivi vya unyanyasaji kwa namna yoyote ile tunakwenda kuvikomesha kwenye maeneo yetu ya kujifunzia.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine lililozungumzwa sana hapa ni eneo la ujenzi wa Vyuo vya VETA nchini ambalo ndilo tunaloendeleanalo hivi sasa. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu, kazi hii inakwenda kwa speed kubwa. Naomba nitoe takwimu hapa kwamba mpaka kufika mwezi Juni, mwaka huu 2022 jumla ya Halmashauri au jumla ya Wilaya 77 zitakuwa zimepata vyuo hivi vya VETA. Kwa hiyo, safari yetu itakuwa imebaki kidogo tu kwenye Halmashauri zile nyingine ambazo zitakuwa zimebaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaondoe wasiwasi ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Sita imejizatiti kuhakikisha kwamba eneo hili tunakwenda kulifanyia kazi sawasawa. Kwa hiyo, niwaondoe wasiwasi na sisi tutakwenda kusimamia eneo hili kwa umahiri mkubwa sana kuhakikisha kwamba mambo haya yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, imezungumzwa kidogo kuhusiana na ujenzi wa Chuo cha Mkoa cha Geita. Nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, ujenzi unaoendelea pale ni ujenzi ambao ni sahihi zaidi kwa sababu tumekwenda kuongeza hata miundombinu mingine ambayo ilikuwa haipo. Ujenzi ule wa mwanzo wakati unajengwa na mkandarasi mfano vitu kama mabweni yalikuwa mawili tu, bweni moja kwa wasichana na bweni moja kwa wavulana, lakini ujenzi wa sasa hivi tunaofanya tumeongeza mabweni mengine mawili kwa maana yatakuwa mawili ya wasichana na mengine ya wavulana.

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, amezungumza kwamba, ujenzi wakati unafanywa na mkandarasi ilikuwa ni zaidi ya Shilingi bilioni 14 zingetumika kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi ule, lakini kwa kutumia Force Account tunakwenda kutumia Shilingi bilioni tano na itakamilisha ujenzi ule, lakini kwa kuongeza miundombinu mingine rafiki. Kwa hiyo, siyo tu kwamba tumepunguza gharama za ujenzi, bali vilevile tumeboresha mazingira yale. Nimwondoe wasiwasi kwamba chuo kile kitakuwa ni miongoni mwa vyuo vizuri vya mikoa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, pia alisema kuna zile structure ambazo zinanyanyuliwa sasa hivi ambazo ni steel structure. Kwenye frame structure tuna namna mbili ya kujenga; tunaweza tukatumia concrete structure au tukatumia steel structure, lakini zinafanya kazi hiyo hiyo. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba ubora wa chuo kile unakwenda kuwa vizuri kabisa na gharama yake inakuwa ni ya chini.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumza hayo, naomba niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri. Naomba tu Waheshimiwa Wabunge muweze kutupitishia bajeti yetu hii ili tuweze kuunga mkono juhudi za dhati za Mheshimiwa Rais za kuhakikisha kwamba tunakwenda kufanya restructuring katika mfumo wetu wa elimu ili hiyo Tanzania anayoihitaji Mheshimiwa Rais tuweze kuifikia.

Mheshimiwa Spika, ahsanteni sana, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)