Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi lakini namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai. Naishukuru pia familia yangu na wananchi wa Urambo kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua nafasi hii kupongeza Wizara ya Elimu kwa jinsi ambavyo inafanya kazi kwa bidi, Wizara hiyo ni ngumu inahitaji kwa kweli maarifa, juhudi na kweli wanajitahidi kadri ya uwezo wao. Hongera Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote, Katibu Mkuu, Makamishina na wengineo hongereni sana kwa kazi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kwa niaba ya wananchi wa Urambo kushukuru Wizara hii kwa kutupa sisi VETA. Kwa sababu VETA kwa kweli ni ukombozi kwa vijana wengi ambao hawana kazi wanapata ujuzi kwa hiyo, tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kutupa VETA. Ombi letu ni kwamba tuongezewe majengo tuongezewe na ujuzi ili vijana wetu waendelee kunufaika na suala la ufundi. Kwa sababu, ufundi ni suala linalosaidia sana hasa vijana wasiokuwa na ajira ili na wao wapate jinsi ya kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninawaomba Wizara ya Elimu itilie mkazo sana masuala ya VETA, nchi nyingi zilizoendelea zimetiliwa mkazo sana masuala ya ufundi. Kwa hiyo, nitawaomba sana waendeleze juhudi yao ya kueneza VETA zaidi lakini pia, kuongeza aina mbalimbali za ufundi ili vijana wetu wanufaike.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya Walimu yamezungumziwa sana, nami naunga mkono Waheshimiwa Wabunge wote waliozungumzia umuhimu wa kuwajali Walimu wetu. Unapozungumzia elimu vitu viwili unaanza, wanafuzi, walimu halafu ndiyo yanakuja majengo na kadhalika na nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ametusaidia kwa upande wa majengo ya kila aina maabara, madarasa, kwa kweli tunampongeza sana hongera sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kujali elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu ni kwamba unapoongeza wanafunzi maana yake ni kwamba unaongeza Walimu zaidi. Tanzania tunahitaji kuwa na Walimu 433,992 ili iweze kukidhi mahitaji ya hapa. Kwa mfano, mimi Urambo tu nahitaji Walimu 600 kwa hiyo kwa nchi nzima mahitaji yetu ni 433,992 ndiyo mahitaji ya Walimu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu ni kuwa unapokuwa na idadi kubwa ninaamini kabisa kwa jitihada ya Serikali yetu inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi Walimu hawa watapatikana tu. Mimi ninaamini kwa jitihada ya mama yetu Samia Suluhu Hassan walimu hawa watapatikana, lakini unapokuwa na idadi kubwa ya Watendaji Kazi kama hawa 433,992 ninaamini unahitaji chombo chao maalum cha kuwahudumia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu iliunda Sheria ya kuanzisha TSC hapa nchini na ukiisoma ile Sheria inasema wazi kabisa ni kwamba Sheria ya TSC ni kuwa ndiyo chombo cha ajira na maendeleo ya walimu na taaluma yao, lakini ukiiangalia Sheria ilivyo na kilichotokea siyo sawa. Naiomba Serikali irudi ikaiangalie ile Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiisoma la kwanza inasema kuajiri TSC haiajiri, TSC haipandishi madaraja inashughulikia sana masuala ya nidhamu na kadhalika. Ombi langu kwa kifupi ni kwamba Serikali iiangalie ile Sheria iliiunda yenyewe kwa nia nzuri kwamba, kikundi kikubwa cha Walimu kilivyo kihudumiwe na chombo kimoja. Sasa hivi ndio naona walimu wengi wanaomba hiki na hiki wanashindwa kupata uhamisho, wanashindwa kwenda shule, kwa sababu wanahudumiwa na vyombo vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa heshima na taadhima TSC iundwe upya kwa kuiangalia Sheria upya haifanyi kazi iliyotakiwa, ninaamini Serikali yetu ni sikivu itasikiliza. Serikali ilikuja na Sheria inaitwa Teachers Board sijui ilikuwa ni ya nini, kwa sababu ile imeongeza tu mzigo wa Serikali, ukiunda TSC nzuri humo humo ndani wataangaliwa kwa kila kitu, kwa upande wa professionl kwa upande wa nini. Kwa hiyo, nafikiria ile Sheria ingeangaliwa upya kwa kweli ingefutwa tu badala yake kile chombo kikaingizwa ndani ya TSC. TSC inamuangalia mwalimu kwa vyote kuanzia mwanzo mpaka mwisho. kwa hiyo mimi ombi langu ni hilo kwamba TSC iangaliwe upya. Iwe One Stop Center kwa ajili ya mwalimu itakuwa ni nafuu sana kwa mwalimu watapata morale ya kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wako Waheshimiwa Wabunge wengine wameshazungumzia kwamba maslahi ya walimu yaangaliwe ni kweli, zamani kulikuwa na posho maalum kwa Walimu wanaofanya kazi vijijini, kulikuwa na posho ya Ualimu, lakini Serikali yenyewe inaweza kuangalia tunawapa motisha vipi Walimu wanaofanyakazi katika mazingira magumu na hasa ukiangalia pia Walimu wa sayansi, hisabati na lugha pia kwa ujumla ili waweze kupata motisha ya kufanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nimetaka kulizungumzia ni suala la ukaguzi. Hapa nchini tuna shule zipatazo 24,000, shule 24,000 siyo rahisi kuzikagua kwa hali ya ukaguzi ilivyo kama Idara haiwezi kuwa Idara halafu ikahudumia shule 24,000. Jawabu lake ninavyoona mimi na ninaishauri Serikali, badala ya kuwa Idara chini ya Wizara ya Elimu iwe Taasisi inayojitegemea, wapewe fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Serikali imejenga ofisi zao tumeziona, lakini bado wanahitaji kuwa Taasisi inayojitegemea, huwezi wewe kwenda kumkagua Mkurugenzi ambaye amekusaidia mafuta asubuhi, anakusaidia mafuta halafu baadae unampelekea kwamba shule yako hii mbovu na hii na hii haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukitaka shule zetu zifanye kazi vizuri walimu waangaliwe ufundishaji wao na kupewa ushauri from time-to-time lazima Ukaguzi ujitegemee. Ombi langu kwa Serikali ukaguzi sasa hivi wanasema quality assurance (udhibiti ubora) lakini mimi nafikiri iwe authority inayojitegemea ili hata wakija kumshauri Mkurugenzi kwamba shule yako hii na hii na hii na hii ifanyiwe hivi na hivi watasikiliza lakini kwa hali ilivyo sasa hivi bado Serikali inahitaji kuimarisha ukaguzi ili wafanye kazi yao na kazi yao ni muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanakwenda pia kwenye shule private hizi 24,000 ni pamoja na private wanakwenda kwenye shule za private. Private na Vyuo vya Ualimu, ukaguzi lazima uende ukaone hawa Walimu wanaofundisha kwenye vyuo binafsi kweli wanakwenda vizuri? Kwa sababu, wakati wa kuwapanga tunapanga tu tunachanganya wanaotoka kwenye Vyuo vya Serikali wanaotoka kwenye Vyuo Binafsi wote wanapangwa. Kwa hiyo, ni muhimu wakaguzi wakaenda kuona kule je, walimu wanaoandaliwa kule pia wanaandaliwa vizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo naipongeza Wizara kwa kazi kubwa na ninaunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)