Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya nchi yetu na hususani kwenye Wizara hii ya Elimu. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuteuliwa na Naibu Waziri, leo sitakupongeza kwa kazi kwa sababu haya tunayokuambia leo ukiyafanya ndio nitakuja kukupongeza. Wabunge wengi wamechangia vitu vizito sana kuhusu Wizara hii, kwa hiyo ni mategemeo yangu utakapokuja kuhitimisha, utakuja na hitimisho linalofanana na wewe sisi ambao tunakufahamu kama Profesa la kuchukua hatua na michango hii ambayo tumeichangia hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaingia kwenye hoja yenyewe nitoe utangulizi kidogo kuwakumbusha yale ambayo Wizara ya Elimu wenyewe mmeyaandika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dira ya Wizara ya Elimu inasema: “Kuwa na Mtanzania aliyeelimika mwenye maarifa, mwenye stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya, ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa” hiyo ndio Dira yenu. Niende kwenye majukumu mawili tu mliyoyataja pale. Majukumu yenu ni kubaini vipaji na kuviendeleza, jukumu lingine kuendeleza utaalam wa ndani katika sayansi ya teknolojia na ubunifu. Sasa hayo mambo ndio nitakayosimama nayo kuwashauri tuende vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najaribu kupitia historia ya elimu ya nchi hii kwenye website yenu. Pale juu tu ukifungua historia fupi ya elimu inakuambia kuna elimu ya jadi wakaeleza elimu ya jadi ilivyokuwa kipindi hicho. Pili, akasema elimu wakati wa ukoloni wakaishia hapo. Kwa hiyo, historia ya elimu Tanzania kwa mujibu wa website yenu imeishia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa leo kupitia Bunge hili tuandike historia ya elimu ya Watanzania baada ya uhuru, ili tutengeneze historia ya elimu tuanzie kwenye mitaala ndio hoja yangu inapokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwamba mmeanza mchakato wa kutengeneza mitaala, lakini kabla hujafikiria kutengeneza mtaala fikiria kuwa na malengo ya Serikali. Government Objectives ziende zika-reflect hicho mnachotaka kukifanya, sisi kama watanzania kwa miaka 100 miaka 50 tunataka kwenda wapi? Ninafahamu tunayo maono lakini tuna maono ya muda mfupi, sasa tunataka tuwe na maono ya muda mrefu ili tutakapokwenda kutengeneza mitaala yetu i-reflect National Objectives.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutengeneza mitaala bila kujua sisi tunataka kwenda wapi ndio hayo mambo tutakayoambiwa hapa, sijui Zinjanthropus sijui vitu gani, na kule kwetu Mlima Kilimanjaro tunaambiwa aligundua Mzungu wakati tulikuwepo sisi pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutengeneze kwanza National Objectives Mheshimiwa Waziri kaa na Wizara zinazohusika tengenezeni malengo ya miaka 50, miaka 100 then sasa ndiyo tutaenda kutengeneza mitaala na kama tunatengeneza mitaala hii iende moja kwa moja kwenye ujuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu tunafahamu kila aliyeko hapa Mwenyezi Mungu amempa karama yake, ile talent ambayo amepewa na Mwenyezi Mungu, sisi tunatakiwa tutumie mifumo ya kidunia ya elimu kuwezesha kuboresha zile talents. Sasa mifumo ya elimu tuliyonayo inaenda kupishana na talents tulizonazo mtoto anatoka hapa huyu anatakiwa kuwa engineer, akifika chuoni kwa sababu kwenye education ndiyo ambapo mikopo inapatikana anaacha kile ambacho ni talent yake anakwenda kwenye jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunahangaika mtu amemaliza Chuo Kikuu akirudi nyumbani hana cha kukusaidia kwa nini tulimpa kitu ambacho siyo karama aliyopewa na Mwenyezi Mungu. Humu tutaumana tu humu! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anakuambia hapa nilikuwa najadiliana na mwenzangu anasema ukimchukua Mzee aliyesoma elimu ya ukoloni mpaka Darasa la Saba, kipindi kile Darasa la Nane na mtu aliyemaliza Masters sasa hivi, yule wa Darasa la Nane ana uwezo mkubwa wa kufikiria na kuamua kuliko huyu why? Majibu ni kwamba wale walienda kwenye talent. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasoma historia mliyoiandika kwenye website yenu kwamba elimu ya jadi ilikuwaje. Sasa tuangalie vipawa vya watoto wetu tuviendeleze. Ukisoma types of curriculums aina za mitaala, tunayo core-curriculum na extra-curriculum tukivitumia hivi ni mifumo sahihi inayoweza kuwafanya watoto wetu wakaboresha talent walizopewa na Mwenyezi Mungu na wakaja kutusaidia sisi, hii ni baada ya kujua tunataka kwenda wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunakwenda kwenye Serikali ya viwanda maana yake ni nini? Baada ya miaka 50 tunategemea kufikia malengo ya Serikali ya viwanda, sasa tuanze kuwaandaa watoto kuanzia Darasa la Saba huku kufikia Serikali ya viwanda. Kwa sababu, huwezi kuwa na Serikali ya viwanda kwa kutegemea wataalam kutoka nje, ni lazima uwaandae hawa wa kwako wapande wafikie pale wafanye hicho tunachokitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kama tunataka sasa mitaala hii ifanikiwe lazima tuende kwa Walimu, hawa ndiyo ambao wanaenda kutekeleza mitaala yote hii tunayoizungumza. Tuwatengenezee Walimu mazingira mazuri na namna ya kuwatengenezea mazingira mazuri tuwatoe kwenye hii mikanganyiko ya kiutawala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu kila mtu ni kiranja wake, nilishasema kwa nini tusikubali kwamba Tume ya Utumishi wa Walimu iwe ndiyo i-centralize masuala yanayohusu Walimu? Ghana wamefanya wenzetu wa Kenya wamefanya Tume hii iwe na uwezo wa ku-hire ku-fire ku- promote ku-transfer na vitu vyote vinavyohusiana na recruitment ya Walimu na stahiki zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunahangaika na uhamisho kila siku, kazi hii ifanywe kwenye Tume ili mwalimu amtazame mtu huyu mmoja. Ninajua nikizungumza hivi Maafisa Elimu watasema sisi tunakwenda wapi hapana! Wote wanakuwa covered kwenye Tume hii, kwani Tume ya Madini Tanzania inaendeshwaje kuna Wizara pale juu lakini hapa chini kuna Tume ya Madini na ina-run vizuri. Kwa hiyo tuombe sasa Serikali ije hapa na majawabu ya hili jambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijakalishwa chini, niombe Mheshimiwa Waziri sisi tunaokufahamu na tunaojua uwezo wako na uwezo wako wa kufanya maamuzi, leadership is all about decision making. Make decision brother njoo hapa tupe majawabu kwamba sasa tunataka tukaandike historia ya nchi hii na tuanzie hapa, ninajua ni ngumu na inahitaji pesa na hapa niseme ni ngumu kweli na inahitaji fedha kweli, lakini tutumie fedha zetu za ndani, hakuna mtu atakayekupa knowledge na skills brother. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiomba fedha za kunawa mikono, sijui matende utapewa lakini za kukuletea knowledge and skills usitegemee. Hakuna jirani atakayekuletea fedha wewe ukawape watu wako knowledge na skills ili ukawatawale never! Kwa hiyo, lazima sisi tuweke fedha humu tuhakikishe huu mtaala from the beginning, tutumie fedha ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hapo ndipo siri ilipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda tu pale kupiga magoti tumetoka kwenye track kwa sababu, sisi tupo kwenye ushindani ni lazima tukubaliane hivyo. Serikali hizi zinashindana kuwapa watu wake sasa kama unataka watu wako wawe smart, hakuna atakayekujengea watu smart tutaletewa hizi historia za kizamani ambazo haziwezi kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nisemee kidogo kuhusu Chuo cha SUA kile Chuo cha SUA Mheshimiwa Waziri…

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa…

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, tukubaliwe kiwe cha kilimo wakafanye stadi ambazo zitatusaidia kuleta mabadiliko ndani ya nchi yetu, waache kufanya kazi zingine ambazo ziko nje ya uasisi wake.