Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kuniona na kunipa nafasi hii adimu na mimi niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze sana Wizara kuanzia Waziri na timu kwa ujumla na kwa kweli kuja na hotuba ambayo inaonesha mabadiliko mengi ambayo yanakwenda kufanyika na yale mambo saba ambayo umeyasema kwamba mnakwenda kuyatekeleza basi sisi tupo tayari tunayasubiri utekelezaji na tunaamini yataweza kuisaidia nchi hii ikaweza kwenda mbali. Kwa hiyo, Mheshimiwa Profesa tupo pamoja na wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Kamati kwa uchambuzi walioufanya wamefanya vizuri, kwa kweli wamezungumza mambo ya msingi na mimi naamini Wizara itakuwa imeyachukua kwenda kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya Japan ni moja ya nchi zilizoendelea sana, lakini ilifika mahali kuna kipindi nchi ile uchumi wake ulisimama, kila kitu kilisimama. Sasa Waziri wa Elimu wa nchi ile alichokifanya alitayarisha questionnaire akawaandikia Maprofesa 14 duniani wa vyuo vikubwa, akawaambia nataka mniambie hivi hasa nini roho ya elimu katika: akaweka kila eneo kama ni kwenye kilimo, ufugaji, uvuvi, viashara, viwanda na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale Maprofesa walipomjibu ndiyo waliyoisaidia kuikwamua Japan na uchumi wake ukaanza tena kupiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo na sisi hapa leo Profesa umebeba hiyo dhamana, tunaelewa kwamba elimu ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, elimu ndiyo inatupatia maarifa ya namna ya kufanya mambo yetu. Elimu inatupatia ujuzi lakini elimu inasaidia kubadilisha tabia tulizokuwa nazo halafu ziwe katika hali tunayoitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wale Maprofesa walisema, elimu hata ukisoma iwe ni Tanzania, iwe ni nje ya nchi yale maarifa unayoyapata, ukija nayo nyumbani kwako yakusaidie kuboresha mazingira uliyonayo na vitu ulivyonavyo ili viweze kuwa katika hali nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kule Songwe, Mkoa wetu wa Songwe ni mchanga ni mkoa wa kilimo, sisi tunashika nafasi ya tatu kwa uzalishaji wa chakula hapa Tanzania lakini pia tuna mazao ya biashara. Katika Mkoa ule ambao tunazalisha kwa kilimo, tunazalisha sana lakini tuna Shule za Msingi 193, Sekondari 64 katika vyote hivyo, shule zote hizo hakuna shule inayomuandaa kijana kwenda kuendeleza kilimo ambacho ndiyo wamekulia, ndiyo muhimili wa nchi yetu, uti wa mgongo. Sasa ina maana ile elimu wanayoipata, wanayosoma wote wale, inakwenda kusaidiaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu elimu haijagusa kwenye kilimo, ufugaji, uvuvi, haijagusa mambo yaliyopo katika ile jamii. Kwa hiyo, tunataka elimu tunayoipata iende kujibu maswali yale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nimefurahi kusikia kwamba mnakwenda kuanzisha Vyuo vya Ufundi, na mimi nasema Mkoa wa Songwe tunahitaji Chuo cha Ufundi ili kiweze kusaidia sasa katika kuwapa ujuzi na maarifa ili iwasaidie katika kuendeleza katika mazingira yale ambayo tunayo. Kwa hiyo, naamini hilo mtalifanyia kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji vifaa vya kufundishia vya kisasa. Sasa hivi shule zetu zote ili ziweze kutoa elimu nzuri, zinahitaji kuwa na kompyuta TEHAMA, ziwe na vifaa vya kufundishia, ziwe na photocopy, hizi shule za kusema kwamba eti bila ya kuwaandalia mazoezi ya kutosha hatutaweza kufanya vizuri. Lakini mimi nataka kusema haya mambo mengine yote yamesemwa vizuri na waliotangulia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ninalotaka kulizungumzia ni udahili katika vyuo vya elimu ya juu. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongenza sana Mheshimiwa Rais kwa mambo mbalimbali anayoyafanya lakini ikiwemo ya kuanzisha ile filamu ya Royal Tour. Hii itatuletea watalii wengi. Baada ya watalii hao watakaokuja hapa nchini wengine watakuja kwa ajili ya kusoma. Tutakuwa na utalii wa shule, utalii wa kuja kusoma. Sasa kwetu hapa Tanzania tuna bahati ya pekee, Serikali mmejitahidi, Serikali lazima tuipongeze imejitahidi. Tuna Vyuo vya Elimu ya Juu zaidi ya 50, zaidi ya 50 Vyuo vya Elimu ya Juu viko hapa katika nchi yetu, nchi nyingi hazina hivyo vyuo. Tunayo mitaala mingi na mitaala yetu ambayo tunaitengeneza sasa hivi na nafurahi Mheshimiwa Profesa mnaipitia upya ile mitaala naamini mitaala mtakayokuja nayo itajibu mahitaji ya nchi yetu lakini lazima pia tuangalie mahitaji Afrika Mashariki, SADC, Afrika na tuangalie ulimwengu kwa ujumla kwamba wanahitaji nini hasa maana yake sisi ni sehemu ya ulimwengu, ni sehemu ya globalization. Kwa hiyo, lazima elimu tunayoitoa ikidhi mahitaji haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa basi ninachotaka kusema ni nini. Katika hivi vyuo vyote tulivyonavyo ambavyo vipo, sasa hivi mkakati Profesa uwe katika kudahili wanafunzi wengi wa hapa ndani lakini na wa nje. Tuchukue kutoka Kenya, Uganda, South Sudan, Ethiopia, Ulaya, wote mnaelewa Waheshimiwa Wabunge, UK ukiangalia pato lake la Taifa sehemu kubwa mchango wake wa Pato la Taifa unatokana na shule na watu mbalimbali wanapeleka kwenda kusomesha watoto kule na sisi tunataka sasa tufike mahali watoto waje kusoma hapa kwetu, nchi ya Tanzania tupo strategically located! Tutumie amani na utulivu kama tunu tuliyonayo hii ituletee sasa watalii wa elimu waje kusoma hapa na vyuo vyetu vipate wanafunzi wengi. Tukifanya hivyo, mitaala tukiiboresha, tukaondokana na haya mambo ya zamani!

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Profesa zamani kulikuwa na mature age entry kwenye Vyuo Vikuu, tuliifuta tukaondoa. Sielewi kwa nini tuliondoa? Lazima tuiangalie hiyo kwa nini tuliindoa hivyo vitu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii watu wanasema mtu akitoka Kenya hana sifa ya kusoma kwenye Vyuo Vikuu vya kwetu, hivyo tunataka kusema sisi ndiyo tuna elimu nzuri kuliko hata ya Kenya? Hiyo siyo kweli, lazima hayo tuyaangalie! Kama kuna mahali tumefanya makosa ni kwenye eneo hilo. Tukaangalie udahili wetu tuanzishe mambo haya. Kama tunaona kwamba hawajakidhi vile vigezo vya kwetu anzisheni kozi ya foundation kwenye vyuo vyote, isiwe kwenye Open University tu, kwenye vyuo vyote, wapeni udahili wafanye foundation mwaka mmoja, wapate zile minimum qualification wasome hapa, walete dola nyingi, hizo dola zitatusaidia kwenda kulipa hata hii mikopo ambayo tunaikopa kwa ajili ya elimu yetu, tunakwenda kulipa. Sasa Tanzania tunasema tupo pazuri, pazuri bila kutumia hii nafasi tutashindwa. Kwa hiyo mimi nafikiri Mheshimiwa Profesa mtafanya mabadiliko makubwa na nimeona kwenye hotuba, nimeona kwenye mambo mengi na hatua ambazo mnachukua tunataka ziende zika-address haya zitusaidie kama nchi kuleta mambo tunayoyahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ina changamoto nyingi, watoto wengi wanakwenda kusoma wanakosa mikopo. Nafikiri ni wakati muafaka Profesa, hebu angaliaeni ni namna gani wadau mbalimbali wanaweza kuchangia kwenye hii Bodi ya Mikopo. Tupate fedha kutoka kwenye maeneo mengine tupanue wigo halafu watoto wetu wote wapate elimu, waweze kupata mikopo hiyo, wapate iwe ni kama vile vyuo vya elimu ya kati, Vyuo Vikuu wale wote wenye sifa wapate mkopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni mkopo watakwenda kulipa sasa kwa nini tuwanyime. Kwa hiyo, mimi nafikiri kwamba ni suala la msingi tuangalie hilo litatusaidia sana tukipanua wigo wadau wakachangia, tukawa na fedha za kutosha na tukaweza kufanya vizuri. Mimi naamini katika hatua hizo itachangia sana katika uchumi wa Taifa letu na nchi itaweza kupiga hatua vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo ninataka kusema ni ajira kwa wanataaluma. Wanataaluma kuna sifa zao, kuna vigezo na sisi kwenye ajira ndiyo tunataka huko tupanue ndiyo maana mimi nasisitiza sana hivi vyuo vyote tulivyonavyo tuajiri watu. Kwahiyo kwenye taaluma naomba Profesa aangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)