Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii na mimi nikupongeze kwa kuchaguliwa kwako lakini naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja katika kumpongeza Waziri wa Elimu pamoja na Naibu wake pamoja na staff yake nzima kwa kazi nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba nijikite kwenye eneo moja lakini yatakuwa maeneo mawili. Moja ni kwenye shule mbili ambazo zimetelekezwa pale kwenye Jimbo langu ambazo ni shule za Wizara hii ya Elimu ni shule moja ya Lugufu Boys na shule moja ya Lugufu Girls. Hizi ni shule za Wizara ya Elimu, shule hizi zimetelekezwa kwa sababu hazijapata miundombinu ya maji pamoja na umeme. Naomba Mheshimiwa Waziri unisaidie kwenye jambo hili kwa sababu hizi hazipo chini ya Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi Jimbo langu lina Tarafa tatu. Nilikuwa naomba Tarafa ya Nguruka tupate high school kwa sababu tuna sekondari nyingi. Lakini pia naomba kwenye Tarafa ya Buhingu, Buhingu Sekondari ipandishwe hadhi iwe shule ya high school kwa sababu eneo langu la Jimbo ni kubwa sana. Kutoka mwanzo wa jimbo mpaka mwisho wa jimbo ni kilomita 400. Kwa hiyo unaweza ukaona kabisa kwamba kila tarafa kuna haja ya kuwa na high school. Kwa hiyo watu wa Nguruka wako tayari kupokea high school kwenye Shule yao ya Nguruka Sekondari lakini pia Buhingu wako tayari kupokea high school kwenye Shule yao ya Buhingu. Naomba Mheshimiwa jambo hili unisadie.

Mheshimiwa Naibu Spika, liko jambo ambalo mimi ninaomba nilizungumze; ni jambo la kitaifa. Kwanza naomba nipongeze Serikali kwa kukubali kuwarudisha shuleni wanafunzi waliopata ujauzito; kwamba baada ya kuwa wamejifungua basi warudi kusoma na huku wakiendelea kunyonyesha. Hili ni jambo jema sana na naomba nikuhakikishie wananchi wamelifurahia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye eneo hili mimi ninaona bado kuna hatari kubwa sana, kwa sababu kwa taarifa ya mwaka jana, mimba za shuleni zilikuwa 8,000, ni nyingi sana! Kwa hiyo, Serikali lazima iweke mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba inapunguza hizi mimba shuleni. Lakini hili ambalo Serikali imelifanya la kuona namna ya kuwarudisha waliopata mimba, baada ya kujifungua warudi shuleni huku wakinyonyesha watoto wao. Mimi naona kama hili jambo litaongeza idadi ya mimba. Kwa sababu wale 8,000 walipata mimba lakini wakiamini kwamba hawawezi kwenda shuleni kwa sababu wamepata mimba. Sasa watakapokuwa wamepata mimba na wakarudi shuleni kusoma huku wakinyonyesha mimi ninaona kabisa kuna hatari ya mimba kuongezeka shuleni.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, kwa kuwa pia hata Kamati yangu imelizungumza hili na kuona, kwamba kuwe na elimu kwenye eneo lile la mimba shuleni. Kwa maana itapunguza sasa kile kitendo cha kuongeza mimba shuleni.

Mheshimiwa Waziri hili jambo usipoliangalia litaleta shida kwa sababu pamoja na kwamba wananchi wamefurahia lakini mimba zitakapoongezeka wananchi wataandama. Kwa hiyo itakuwa kashfa kwa Serikali kuona yenyewe imechochea mimba shuleni kwa sababu imeruhusu sasa watoto waliokuwa wamepata mimba wajifungue na warudi shuleni wakiendelea kunyonyesha watoto wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kitakachotokea mle darasani yawezekana ikawa ni darasa ambalo linafundisha wazazi waliojifungua. Kwa hiyo, naomba hili nizungumze kwa msisitizo. Nakumbuka hili jambo kuna kikao cha Bunge wakati fulani niliwahi kulizungumza, nadhani lilikuwa Bunge la mwezi wa tisa. Kwa kweli naomba nirudie ili kusudi lisije kuleta taharuki baadaye kwa wananchi wetu watakapokuja kuilaumu Serikali kuona kwamba yenyewe ndiyo imesababisha mimba za shuleni kuweza kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)