Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya wapiga kura wangu wa Jimbo la Kahama Mjini, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutusaidia sana kwenye ujenzi wa shule na kutupunguzia michango mingi ambayo imekuwa mizigo mikubwa sana kwa wananchi wetu namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili la elimu naona ni vizuri kwa kuwa tunaliongea kwa mapana Mheshimiwa Waziri, ingekuwa dini tungeweza kuhama, lakini kwenye elimu utahamia wapi. Kwa hiyo ingekuwa dini mtu anaweza kuamua hii bwana imenishinda unahamia dini nyingine, lakini kwa mazingira yalivyo kwenye elimu huwezi kuhama. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wa Elimu ajaribu kutuelewa sisi Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, hali ya wananchi kwenye suala hili la elimu ilivyo kule vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Serikali ikubali, ikanunue mawazo na maarifa mepesi ili wanafunzi kuanzia darasa la kwanza, baada ya kuwa wamejua kusoma na kuandika wafundishwe elimu mbadala. Kuwe na elimu hii tuliyoachiwa na mkoloni, lakini tuwe na elimu mbadala. Maana yangu ni kwamba sisi tunaotembea sana nchi mbalimbali, leo hapa mimi nakwenda shuleni nafundishwa panzi ana miguu saba, senene ana miguu minane. Hivi elimu inakataza kweli kuniambia bei ya senene ambayo leo ni Sh.50,000 naishia tu hapo kwa kilo moja, ni kosa?

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunafahamu kabisa kwamba panzi wana protein na wanaliwa na kuku, je ni kosa kufundishwa darasani kwamba kuku anakulaga panzi na kilo moja ya panzi ina panzi 17 na ukimpa utakuwa umesevu kununua chakula cha kuku. Je ni kosa kielimu, kwa nini isiwe kwenye elimu mbadala?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu leo hapa Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, watu wanaomba kibali zah kuagiza kibali cha kuagiza chakula cha samaki India, lakini wote tunafahamu kwamba samaki anakula minyoo au chambo na kutengeneza minyoo mtu akifundishwa darasa la kwanza inachukuwa masaa 16 kupata minyoo, ni kosa?

Mheshimiwa Naibu Spika, je, unataka mtu mpaka asome, amalize form four, six, akawe fundi seremala atengeneze makochi yasiyonunuliwa, ni kweli tunaenda kuwaambia wananchi wauze ng’ombe, waje wasome waende VETA, waje watengeneze makochi, ni sawa? Wakati elimu yetu inaletwa, dunia haikuwa hii, dunia ilikuwa ni nyingine kabisa, je turudi kwa Waingereza hawa wanaoangalia mpira wa Chelsea na watoto wao, wanaweza wakatukumbuka watubadilishie elimu? Kweli sisi tunashindwa kabisa kufundisha watoto wetu darasa la kwanza wakatengeneza minyoo, wakawapa kuku, samaki badala ya sisi ku-share mahindi na kuku ni kosa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajaribu kuonyesha namna ambayo ni rahisi mtu kuishi. Zamani mtoto wako wa kwanza akimaliza shule, anawachukua wale wadogo zake anakwenda kuwa nao anakuondolea mzigo. Sasa hivi anamaliza degree, anarudi nyumbani, je, wewe utakuwa na moyo wa kuwasomesha hao wengine una moyo gani huo?

Mheshimiwa Naibu Spika na Mheshimiwa Waziri utakuwa na moyo huo wakati huyu kwanza hajapata ajira, ng’ombe wamebaki nusu, utakubali uuze ng’ombe waliobaki umsomeshe na huyu abaki nyumbani? Haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima viongozi wakati huu wa shida ya mabadiliko duniani ndipo ambapo viongozi strong huonesha mabadiliko makubwa sana ya kwenda mbele, kuliko tukisema na sisi tuwa-damp wananchi na sisi wote tunao watoto kwenye masofa, wamejaa wameweka masikioni wanasikiliza na wanacheza na WhatsApp. Je, tuendelee kuwa- damp hivyo? Je, wale panya road au panyabuku tutawaweza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani! Wenzetu Wizara ya Elimu wanayo maabara mle ndani. Kweli maabara inashindwa? Leo Mheshimiwa Bashe analia mbolea, kweli shule ishindwe kufundisha mtoto kutengeneza mbolea ya kienyeji ambapo ni kuchukua nyasi na udongo na kumwangia maji na kuuza barabarani, hata kama kilo moja shilingi 300, mtoto huku anasoma, lakini Serikali na sisi tunapata mbolea. Hili pia linahitaji kweli mpaka tujue tu Kiingereza, TEHAMA; je, ng’ombe pia tutachunga kwa TEHAMA kweli? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, je, kama tunavyotaka ni hivi, ni kweli wote tutasoma tumalize wote tuwe na degree, tutoke na ng’ombe kule Kijiji tuzilete mjini tena, tuje nazo huku tumesoma, tunaongea Kiingereza. Itawezekana kweli! Kwa hiyo, tunamwomba Waziri wa Elimu ajaribu na Kamati yake kuona kwamba hawa tunaowaongoza ni raia wa kawaida kabisa wenye maisha ya chini, wanahitaji elimu ndogo ya kujishikiza huku wanaishi ili Serikali inunue mawazo mepesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli suala hili linatupa wakati mgumu sana kiasi ambacho unapokwenda kule vijijini, wazee wanatuuliza: “Hivi kweli hakuna njia yoyote ya nyie kufikiri?” Nasi tukirudi kwa wenzetu huku wanapiga tu stop kwamba haiwezekani. Kama leo inapatikana teknolojia duniani, Waziri wa Elimu si aingize tu kule kwenye simu awaeleze kule walimu kwamba jamani, sasa hivi ukichukua lita moja ya maziwa ukatikisa saa moja, kinachopatikana ni mafuta ya kula. Hata hiyo nayo ni kosa kufundisha shuleni? Sasa nani tumwite aje atukomboe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunalia mafuta, watoto wetu hawajui kama kwenye maziwa kuna mafuta, itawezekana kweli tusomeshe watu; ukimwona mtoto aliye na degree, ukimweka mahala, ni kama umemweka kuku wa kizungu. Unamwona kweli huyu mwanangu sijui nitamkuta, sijui atagongwa, sijui atanyang’anywa hili begi alilonalo! Ni kazi ngumu kweli! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, kweli teknolojia inakataza kitu chenye faida? Inakataza kabisa, haiwezekani! Yaani teknolojia ni lazima iwe kutengeneza magari na ndege tu; na TEHAMA? itawezekana kweli! Yaani Tanzania nzima, watu milioni 60 wataenda kwenye TEHAMA? Wataziunga wapi hizo computer? (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata shule ya msingi, mmesema hapo wenyewe, kuna wanafunzi 400 mle ndani: Je, wangekuta asubuhi wanafundishwa kutengeneza minyoo, si wangekuwa wanauza pale nje wakati wanamsubiri mwalimu? Wafugaji wa kuku wangenunua. Si ndiyo sawa tu, tutafanyaje? Dunia imebadilika, population imeongezeka, watu wanahitaji vyakula: Je, tuendelee na procedure ya mbao? Mheshimiwa wa Maliasili naye anataka miti yake, watu wasome wawe mafundi seremala na mafundi rangi. Tanzania nzima tutakuwa mafundi rangi! Haitawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunamwomba sana mwenzetu Mheshimiwa Waziri wa Elimu ya Juu, ajaribu hata yale mawazo ya local. Mpaka wafugaji wanatuuliza kwamba ah, usiniletee maneno ya shule hapa, ng’ombe zangu zilizobaki hizi, mpaka nife mwenyewe, siwezi. Sasa tukatae ukweli, kwani nani hajui?

Mheshimiwa Naibu Spika, wote si tunafahamu kabisa kwamba sasa hivi mtu aliyesomesha kule kijijini ndio anayechekwa. Kwa sababu watoto hawawezi kulima, hawezi kufanya kazi yoyote na ng’ombe zimeisha, naye amezeeka, anaandikisha TASAF, itawezekana kweli? Sasa mbona kuna elimu ndogo na nyepesi ambayo inaweza kutusaidia kwenye huu muda ambao tunao kuliko kung’ang’ana tu kama Waingereza. Maana yake tukiongea wote kama Waingereza, kweli wale Waingereza wa Liverpool watakuja kutusaidia kweli! Itawezekana kweli watuletee mawazo mengine ya kutukomboa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango huo, namwomba tu Mheshimiwa Waziri asipuuzie, maana yake mtoto kwenda shule ni kwenda kuanza mawazo na maisha mapya. Akitusaidia kutufundishia watoto wetu hizi kazi ndogo ndogo za kawaida, atakuwa ametusaidia sana wakati wanajiandaa kwenda kule mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango huo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)