Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba hii kwanza kwa kumpongeza Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya kumsaidia Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nitachangia kwenye maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, usikivu wa redio Tanzania ni mdogo sana kwenye maeneo mengi ya nchi yetu ya Tanzania. Redio hii kwa jina TBC ndiyo wananchi wengi wanaitegemea kwa ajili ya taarifa za uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Jimbo langu la Kilindi kwa kweli, wananchi wa eneo hili kwa muda mrefu wamekuwa wakililia kupata haki yao ya kupata taarifa, hususan za TBC, japo zipo baadhi ya redio zinasikika. Naishauri Wizara hii na Wizara ya Mawasiliano wahakikishe mawasiliano ya uhakika ya redio yanapatikana katika Jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuchangia suala la michezo hususan mpira wa miguu. Mchezo huu muhimu ni sehemu ya ajira kwa vijana wetu. Utaratibu wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) katika kuandaa soka letu Tanzania siyo mzuri. Hatuna utaratibu wa kupata timu ya Taifa, hususan timu ya vijana, Serikali haina budi kuwekeza zaidi kwenye soka la vijana kuanzia soka la vijana chini ya miaka 14, miaka 17 na chini ya miaka 20 huko ndiko tunakoweza kuwekeza soka la uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira (TFF) ni lazima tuwekeze kwenye mpira kwa kushirikiana na makampuni mbalimbali ambayo yatatoa udhamini mkubwa ili Taifa liweze kusonga mbele. Nchi za wenzetu za Afrika kama Nigeria, Algeria, Ivory Coast na kadhalika wamefika mbali kwa nchi zao kuweza kuwekeza katika soka la vijana. Vilevile Wizara ya Elimu ihakikishe kuwa michezo shuleni inarudishwa kwa kasi kubwa kwani huko ndiko waliko vijana wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kujielekeza kwenye upatikanaji wa vifaa vya michezo kwa bei nafuu. Vifaa vingi vya michezo vipo bei ya juu sana, Serikali ilione suala hili kwa kusimamia bei za vifaa vya michezo ili wananchi wengi hususan vijana waweze kupata vifaa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni muhimu katika michezo nchini ni suala la uchaguaji wa timu ya Taifa. Timu ya Taifa imekuwa na utaratibu mbovu sana, timu hii ya Taifa imekuwa haiangalii wachezaji kutoka Wilayani na Mikoani kama ambavyo miaka ya nyuma ambapo timu ya Taifa ilitazama uwezo wa mtu na siyo timu kubwa tatu za Dar es Salaam, Simba, Yanga na Azam. Wakati umefika sasa pawepo na Kamati ya wachezaji wa zamani waliocheza timu ya Taifa kuhusishwa na utafutaji wa vipaji mikoani kuanzia ngazi ya vijiji, wilayani na mkoani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hotuba.