Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia na mimi nichangie katika Wizara hii ya Sayansi, Teknolojia na Elimu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa kunipatia nafasi ya kusimama hapa leo na kuchangia katika Wizara hii.

Napenda pia kuchukua nafasi ya kuwapongeza Wizara ya Elimu, Waziri Profesa Mkenda pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Kipanga pamoja na timu yote ya Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli Wizara ya Elimu inafanya vizuri sana. Nami pia nichukue nafasi ya kumshukuru sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuangalia hii sekta ya elimu na kuipa kipaumbele. Kwa hivi karibuni tumeona madarasa mengi yamejengwa na haya madarasa yaliyojengwa ni dalili kwamba sasa Vyuo vyetu Vikuu vijiandae kuwapokea wanafunzi wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kila mwanafunzi anayesoma hata kuanzia shule ya msingi ukimuuliza swali unataka kuwa nani atakwambia nataka kuwa Daktari, nataka kuwa Pilot, nataka kuwa Injinia, nataka kuwa Mwalimu lakini atakuwaje Mwalimu, mwisho wake ni wapi? Mwisho wake ni Chuo Kikuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba hivyo basi nichangie katika eneo la Vyuo Vikuu. Katika nchi yetu ya Tanzania tuna takribani Vyuo Vikuu 34. Vyuo Vikuu 12 ni Vyuo Vikuu vya Umma, Vyuo 22 ni vya Sekta Binafsi na vilevile tuna Vyuo Vikuu vitatu na ambavyo ni Vyuo Vikuu Vishirikishi kikiwepo Chuo Kikuu Kishirikishi kilichopo Mbeya - MUST, kilichopo Iringa – MUSE na kilichopo Dar es Salaam – DUCE.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Vyuo Vikuu hivi vina Wahadhiri 7,647 na hao ndiyo Wahadhiri waliopo katika Vyuo vyetu Vikuu hivi 34. Na hao Wahadhiri wenye elimu ya Uzamivu yaani Shahada ya Uzamivu (PhD) ni 2,185 sawa sawa na asilimia 28.6. Wenye Shahada ya Uzamili (Masters) ni 3,875 ambao ni sawa sawa na asilimia 50.7 na wenye Degree ya Kwanza ni 1,587 sawa sawa na asilimia 20.8. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii idadi ya Wahadhiri ni ndogo, ukilinganisha na wanafunzi katika Vyuo Vikuu. Hii idadi ni ndogo, matokeo yake ni nini? Ndoto ya wanafunzi wanaofika Vyuo Vikuu inafifia hapa katika Chuo Kikuu. Wanafunzi hawa wamesoma kuanzia Elimu ya Msingi, Sekondari hadi wanafika Chuo Kikuu wanakutana na changamoto ya upungufu wa Wahadhiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aliwahi kusema Mheshimiwa mmoja sehemu kwamba hata ukiwachukua wanafunzi leo ukawaweka katika hoteli ya nyota tano halafu hao wanafunzi wakapata kila kitu lakini kama Wahadhiri wa kuwafundisha hawapo ni bure. Tutapata wanafunzi ambao hawataendelea na wataondoka katika maeneo hayo, tutapata wanafunzi ambao watachanganyikiwa na mwisho wa siku hata ndoto zao hazitafikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii changamoto imetokana na hii sera ya kusema Wahadhiri wanaajiriwa kutoka Utumishi, Wahadhiri wanatoka Utumishi. Kwa hiyo, kila wakati Vyuo Vikuu vinapokosa Walimu wanasema hili tatizo liko Utumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba kama ambavyo wengine walishashauri asubuhi, kwamba sasa Vyuo Vikuu virudushiwe ile autonomy waweze kuajiri wenyewe. Mheshimiwa Waziri Vyuo Vikuu vinawatambua wanafunzi ambao wana uwezo wa kubaki pale na kufundisha na hapo zamani ndivyo ilivyokuwa. Wanafunzi wanapokuja pale wanafanya Degree ya Kwanza, wale wanaofanya vizuri na kuwa na GPA nzuri ndiyo waliokuwa wanaajiriwa. TCU wameweka kwamba GPA ya kufundisha Chuo Kikuu japo kuwa hapo pia kuna tatizo fulani kwa sababu kwenye Vyuo Vikuu vingine wanachukua GPA 3.5 lakini Vyuo Vikuu vya Umma wamesema wachukuliwe wale wanaopata GPA ya 3.8 lakini hata hivyo siyo jambo baya.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi wanamaliza wana 3.8, wana 3.9 mpaka 4.0 mpaka 4.2 lakini mwisho wake hawajui kwa sababu Utumishi hawajawaajiri na Chuo bado kina shida lakini hawana ile autonomy ya kuajiri hawa wanafunzi au kuajiri hawa wawe Tutorial Assistant na mwishowe wajiendeleze mpaka wapate Shahada ya Uzamivu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, naishauri Serikali, naishauri kwa dhati kabisa, hapa Chuo Kikuu ndiko ambako tunawatoa Wahadhiri wenyewe, hapa ndipo watumishi wa Serikali wanakotoka, maana watumishi wa Serikali wengi ni wale ambao wameshapita Chuo Kikuu, Sekta Binafsi hata wafanyabiashara wengi wangetaka wawe na Degree ili waweze kufanya biashara zao vizuri. Kwa hiyo, hili jambo naomba Wizara iliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende sasa kwenye uwiano wa kijinsia katika Vyuo Vikuu. Kati ya hao wanafunzi 7,000 kama nilivyokwisha kusema, hawa 7,647 wanaume ni 5,766 asilimia 75.4 ni wanaume. 1,881 asilimia 24.6 ni wanawake. Hivi ni kwanini? Kwani wanawake hawawezi? Kweli asilimia hii hata nusu haijafika? asilimia 75 ndiyo wanaume? Tatizo liko wapi? Hawa wanawake kwani ina maana hawawezi kweli kusoma hata kama huko nyuma hali ilikuwa tofauti? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara iwaangalie wanawake, kwa sababu katika Sekondari kuna shule zinafanya vizuri za wasichana. Tatizo liko wapi wakifika Chuo Kikuu Wahadhiri wanakuwa asilimia 24 ya wanawake? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ifike mahali tufanye maamuzi magumu ya kuhakikisha kabisa hawa wanawake nao wanapatikana. Sasa mimi nina wazo, kuna hii project ya Higher Education Economic Transformation (HEET) ambayo imedhamiria katika mwaka 2021/2022 mpaka 2025/2026 kuwasomesha wanafunzi wa Degree ya Uzamivu 623 na Uzamili 477. Mimi nashauri Serikali angalau robo tatu wawe wanawake. Wanawake wote ambao wanaweza kusoma Chuo Kikuu na wanafikia vigezo vya kuwa Wahadhiri basi wapewe nafasi ya juu katika kuwafikiria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi zilizoendelea hata katika miradi iliyoko Chuo Kikuu ukipeleka mwanamke wanasema women are highly encouraged, kwa maana ya kwamba wanatambua na hata mradi unaolipa Chuo Kikuu wanasema ukipeleka candidate ambaye ni mwanamke unapewa asilimia 40 katika ile project.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi naiomba Serikari iangalie kuweza kuwapata Wahadhiri wengi wanawake hii pia itaondoa malalamiko. Sasa hivi tunafikiria kuweka dawati la jinsia, dawati la jinsia kwa nini? Hawa wanawake ni mama, hawa wanawake ni wanawake, wanajua matatizo ya watoto wa kike lakini sasa unakuta ni wanaume ndiyo wengi. Sasa hata tatizo likitokea kesi ya ngedere utapelekaje kwa nyani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wanaume, mwanaume kakosea, kateleza kesi inapelekwa kwa mwanaume, kwa sababu wanawake hawapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine katika Vyuo Vikuu ni katika uongozi. Vyuo Vikuu vingi ni wanaume ndiyo wanaopewa nafasi ya uongozi. Nakipongeza sana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Anangisye Mwalimu wangu yeye amefanya vizuri sana. Amewajali wanawake. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinawajali wanawake sana, na hilo nawapongeza sana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mheshimiwa Waziri naomba hii jambo liingwe na Vyuo Vikuu vyote kuwaweka wanawake katika nafasi za juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami pia naunga mkono hoja. (Makofi)