Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nikushukuru sana kwa kunipa fursa ili na mimi niweke mchango wangu kwenye Wizara ya Elimu ambayo ni Wizara nyeti na nichanzo kikubwa cha maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda kwenye mchango wangu naomba nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuingilia kati na kuona namna ya kupunguza makali ya bei za mafuta nchini, jambo ambalo lisababisha unafuu katika mfumuko wa bei.

Jambo alilolifanya Mheshimiwa Rais ni kubwa. Sisi Wabunge tupo tayari na tuko nyuma yake kuhakikisha kwamba tunaendelea kwenda kuyazungumza hayo mazuri ambayo ameanzisha kuyafanya katika hali hii ya taharuki ya uchumi katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Naibu Waziri kaka yangu Kipanga kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Mheshimiwa Mkenda tangu amefika pale, na mimi ni mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii yapo mambo mengi ambayo wajumbe tunamshauri na tunaona hata kwenye taarifa yake amewasilisha kuona kwamba anaithamini kamati yetu na anaona mchango mkubwa unaowasilishwa kupitia kamati na mpongeza na ninamshukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa leo nimeupa jina la quality education, ni namna gani nchi yetu tunaweza kusogelea elimu yenye viwango. Quality education inategemea vitu vingi na ukitaka kumuuliza mtu yoyote maana ya elimu atakwambia ni kuhamisha maarifa kutoka eneo moja au kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine. Lakini vitu ambavyo vinahusika katika kuhamisha maarifa haya ni mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa sana naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais na Wizara kwa ujumla kwa namna ambavyo wameimarisha mifumo na miundombinu ya elimu katika maeneo yetu. Zimetumika fedha nyingi sana, zimewekezwa katika kujenga miundombinu ya madarasa, miundominu ya vyuo na ofisi mbalimbali kwenye Idara ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jumapili nilikuwa Wilaya ya Kilindi. Nilitembelea Halmashauri ya Wilaya ile na nilikutana na akina mama wa Wilaya ya Kilindi. Moja ya eneo ambalo walinituma kuja kuzungumzia ni namna gani tunaweza tukaboresha elimu hasa katika Wilaya za Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilindi kwa mfano, wao wamefanya utafiti na wamegundua kwamba watoto wa Kilindi hawafeli tu kwa sababu hawana uwezo wa kufaulu wao kama wao, isipokuwa mazingira yao, ukosefu wa vitendea kazi na homa ya mitihani ndiyo inayowafikisha katika hali hiyo ya kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wameenda mbali, wataalam wa elimu, Afisa Elimu Msingi na Sekondari wameeleza ya kwamba wameunda Jukwaa la Wazalendo wa Elimu wa Kilindi. Lengo lao ni kutafuta photocopy machine kwa ajili ya kuziweka kwenye Tarafa zao, kwa ajili ya kuzalisha mitihani. Kwa sababu baada ya kufanya utafiti wamegundua ya kwamba watoto wengi wanafeli mitihani kwa ile homa, taharuki kwenye mitihani kwa kuwa hawana uzoefu wa kufanya mitihani iliyochapishwa. Wamezoea kunakiliwa mitihani ubaoni, wamezoea kufanya mitihani kwenye madarasa ambayo darasa moja watu 80 watu 90.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukimuweka mtoto kwenye dawati peke yake na ukampa mtihani ambao uko kwenye karatasi umechapishwa tayari anapata taharuki na pengine inaweza kumsababishia kwa kiasi kikubwa kufeli mtihani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wazo ambalo wamelianzisha Kilindi ni wazo zuri sana. Kwamba moja ya eneo ambalo tunaweza tukaisaidia Serikali kupata elimu bora kwa watoto wetu na tukapunguza failure kwa watoto wetu ni kuwapa mitihani mingi zaidi, wapate mazoezi mengi zaidi. Tunaweza kufanya hilo kama tutapeleka hizo photocopy machine walau kwenye Tarafa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajenga madarasa ni vizuri na tumefikia kwenye hatua nzuri sana lakini tupeleke hivyo vitendea kazi ambavyo sasa angalau vitaifikisha elimu hii inayotolewa na Shule za Serikali ifanane na zile Shule za Private. Watoto wanaosoma Anne Maria wanafanya mitihani hata weekly test iliyochapishwa. Mtoto anayesoma shule ya kwetu ya Serikali anakutana na mtihani uliochapishwa siku ya NECTA.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ili aweze kuzoea hali hiyo ya mitihani, aweze kuwa settled ni muhimu sana kwenda kufanyia kazi wazo hili ambalo limeanzishwa Kilindi na pengine liambukizwe kwenye nchi nzima ili tufanye vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ninatamani kulizungumza ni kuhusu Walimu bora na wanaotosheleza. Zimetolewa takwimu mbalimbali, ratio ya Mwalimu mmoja kwa Shule ya Msingi ni kufundisha watoto 45 lakini ratio ya Mwalimu mmoja kwa Elimu ya Sekondari ni kufundisha watoto 45. Kwa Mkoa wa Tanga, ratio ya Mwalimu mmoja anafundisha watoto kuanzia 80 mpaka 200 shule nyingine hii inaleta shida.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna upungufu mkubwa sana wa Walimu. Walimu ambao tunahitaji siyo chini ya 200,000 kama ambavyo takwimu zinaonesha. Pamoja na kwamba kasungura ketu ni kadogo, ajira zinatolewa kulingana na upatikanaji wa fedha kwenye Bajeti. Kuna haja ya kuweka utaratibu wa wazi kupunguza minong’ono, kupunguza Wabunge kuendelea kupigiwa simu mara kwa mara kuombwa ajira na vijana wetu. Kwa mfano, tunao watoto ambao wamehitimu vyuo tangu mwaka 2013, 2014, 2015 ni kwa nini sasa Serikali isitangaze kwamba mwaka huu itawaajiri waliohitimu 2015 peke yake au 2013 au 2014? Tukaweka nafasi ya kupunguza simu na meseji kwa Wabunge wanaombwa kusaidia watoto hao kuajiriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watoto wenye umri mkubwa na unafahamu kwamba mtanzania kwa mujibu wa Sheria ya Ajira anaeajiriwa permanent employment ni chini ya miaka 45. Kadri wanavyokaa nje ya soko umri unakwenda kwa hiyo, mwisho wa siku watakosa nafasi ya kuajiriwa. Je, kwa nini sasa tusiwaajiri hata wale wenye umri mkubwa kwanza kwa sababu tunaajiri kwa awamu ili kuweza kuwaondoa kwenye hilo wimbi la kukosa sifa ya kuajiriwa na Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitazama katika watoto ambao wanaajiriwa wapo vijana wengi ambao wanajitolea kwenye shule zetu za Serikali, lakini bado kila siku tumekuwa tukiimba humu ndani wapewe kipaumbele wale wanaojitolea. Kwa sababu tuna upungufu wa Walimu na wao tayari walishaamua kujitolea kutusaidia kuziba hizo nafasi za upungufu. Kwa nini zinapotoka ajira wasiangaliwe wakaanza kuajiriwa hao kabla hawajatazamwa watu wengine? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukitaka elimu bora, tukitaka quality education tunahitaji pia kuwa na Quality Insurers wazuri, bora, wanaowajibika na sisi kuwajengea mazingira ya wao kuwajibika. Katika nchi yoyote elimu hailindwi au haisimamiwi na mtutu wa bunduki. Hutamkuta Polisi anamsimamia Mwalimu afundishe, hutamkuta Afisa wa TAKUKURU wala Afisa wa Usalama wa Taifa wala wa Magereza akimsimamia Mwalimu afundishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, chombo cha usalama kinachosimamia elimu nchini ni Uthibiti Ubora (Quality Insurers) wao ndiyo wanaangalia namna gani elimu inatolewa, wana- assure elimu itolewe ambayo inahitajika yenye viwango. Lakini kitu cha kusikitisha hatujawawezesha Wathibiti Ubora, tumewaacha katika mazingira ambayo pengine tumeshindwa kutambua uwezo wao au nafasi yao katika kutekeleza majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma majukumu ya Quality Insurers jukumu lao la pili linasema carrying out periodic school and center physical conditions survey, anapaswa kutembelea shule moja au kituo cha kutolea elimu kimoja baada ya kingine lakini hawana magari. Wanaokwenda kumkagua ni Mkurugenzi mwenye shule zake, Mthibiti Ubora anaenda kuomba mafuta, anaenda kuomba gari kwa Mkurugenzi ili aende amkague shule zake. Tutapata vipi hapo elimu bora? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango wako mzuri.

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba dakika mbili niweze kumalizia. Tafadhali.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Kengele ya pili hiyo.

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)