Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja hii. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa hotuba nzuri lakini vilevile kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mama yetu, kipenzi chetu ambaye anahangaika huku na kule kuhakikisha kwamba anatuletea maendeleo. Tumeona kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameifanya katika nyanja mbalimbali kama vile kwenye barabara, kwenye nishati, kwenye elimu, kwenye afya, kwenye maji kote tunaona kwamba tunaendelea kupata maendeleo. Na kwa kutumia hizi fedha alizozipata za mpango wa UVIKO basi akaweza kutujengea madarasa 15,000, tukaweza kupata ofisi za walimu 3,184, tukapata matundu ya vyoo 557 katika kipindi kifupi, madawati zaidi ya 47,000 na meza na viti zaidi ya 451,918. Kweli mama ameamua kutuletea maendeleo tunasema mama ahsante sana na nikweli mama anaupiga mwingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu upungufu wa watumishi. Kuna upungufu wa watumishi wengi na hasa katika sekta ya elimu, ambako hapa nazungumzia upungufu wa walimu. Kwa sasa mahitaji ya taifa tunahitaji walimu takribani 274,549, lakini kuna upungufu wa asilimia 37 ya walimu wapatao kama 100,958 kwenye shule za msingi, vilevile tunaupungufu wa walimu 74,743 katika shule za sekondari. Huu ni upungufu mkubwa sana, kama kweli tunataka kutoa elimu bora haiwezekani bila walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkumbuke mwaka 2012 kwamba watoto wa kidato cha pili walifeli wengi humu Bungeni palikuwa hapakaliki, Wabunge walitaka kujua kwanini wanafunzi wamefeli mpaka ikambidi Waziri Mkuu aunde tume, na tume ikaenda kufanyakazi kutafuta kwanini watoto walishindwa. Moja ya sababu waliyoiona ni kwamba, walikuta kwenye shule kuna walimu wachache sana. Kuna shule zilikuwa na walimu watatu, walimu wawili, mwalimu mmoja na hiyo ikachangia mass failure ya wanafunzi katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba mwanafunzi anayesoma sekondari anasoma vipindi saba na kuendelea. Kwa hiyo, unapokuta kwenye shule kuna walimu wanne, watatu, watano ujue kwamba huyu mwanafunzi hakusoma masomo yote. Kuna masomo ambayo hakuwahi kumuona mwalimu, kuna masomo ambayo syllabus ameigusagusa lakini hakusoma yote. Lakini ndugu zangu mtihani hauna huruma, mtihani uleule utakapotungwa atatungiwa uleule aliyekuwa na walimu wote katika masomo yote na akasoma syllabus nzima, atatungiwa huo huo na yule ambaye alikuwa hana walimu wa kutosha. At the end of story yule ambaye alikuwa hana walimu wa kutosha atafanya vibaya na tutam-label kwamba amefeli; na hii inakuwa ni hasara kwa mwanafunzi mwenyewe inakuwa ni hasara kwa mzazi, lakini vilevile ni hasara kwa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie, kwamba umuhimu wa mwalimu ni mkubwa sana. Hata ukiondoa vitabu vyote au ukawafanya wanafunzi wakakaa tu chini mkeka lakini ukawapatia mwalimu mzuri, hata kama unampa huyo mwalimu watoto ambao wanasema hawafundishiki au wale watukutu au wale slow learners lakini as long as kuna mwalimu mzuri hao watoto watajifunza na watafaulu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuongeza ubora wa elimu mimi nilikuwa na pendekeza yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza, Serikali itafute chanzo, ipate chanzo, iajiri walimu wa kutosha kwa wakati mmoja kusudi sasa tuweze kutoa elimu bora. Sasa hivi katika mashule mengi watoto wanapita tu kwa sababu wanasoma nusunusu sababu hatuna walimu wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera kuna upungufu wa walimu. Katika shule za msingi tunaupungufu wa walimu asilimia 48.8, na katika Shule za Sekondari tunaupungufu wa walimu asilimia 37.

Niombe basi, Serikali yangu wakati wanaajiri walimu katika Shule za Sekondari Mkoa wa Kagera tupatiwe angalau walimu elfu 2,108 ambao tunawakosa, na katika shule za msingi ambako tunaupungufu wa walimu 8,593 basi tupatiwe hao walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumzie kuhusu upungufu wa miundombinu. Najua Serikali imefanya juhudi nzuri sana za kuboresha kuongeza kukarabati miundombinu ya elimu lakini bado kuna upungufu wa madarasa na upungufu wa shule. Katika Mkoa wa Kagera tunamatatizo hasa katika upungufu wa High Schools. Kwa mfano, Wilaya ya Muleba ambayo inakata zaidi ya 40 tuna High Schools tatu, Misenye tatu, Kyerwa mbili, Karagwe High School moja na Bukoba Vijijini High School moja. Tunatambua kwamba hizi shule ni za kitaifa lakini unapowachagua watoto ambao niwatoka katika kaya maskini ambao wazazi wao wana uwezo mdogo unakuta wanarudi kuomba kwamba waendelee kusomea kwenye mikoa ileile kwa sababu ya zile gharama za kuwasafirisha. Kwa hiyo, ninaomba Serikali itusaidie waweze kutuongezea shule zenye High Schools waweke mkakati kuhakikisha kwamba shule zenye High Schools zinajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mrundikano mkubwa wa wanafunzi shuleni. Pamoja na juhudi kubwa za kuongeza shule lakini hasa katika Wilaya ya Biharamulo ndugu zangu ni balaa. Najua hii inatokana na mafanikio makubwa ya elimu bila malipo lakini vilevile ni kwa sababu afya zetu ni njema, tunakula vizuri na tunazaa sana, kwa hiyo, tunawanafunzi wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano; kwenye shule ya Kabindi ambayo iko kwenye Kata ya Kabindi katika shule moja ya msingi kuna watoto 2,672, Muungano kuna watoto 2,366, Nyamarangara kuna wanafunzi 2,828 hiyo yote ni Biharamulo tu. Kikomakoma - Kabindi kuna wanafunzi 3,920, Munzani ambayo ipo Nyakaura kuna wanafunzi 3,992, Shule ya Nemba ambayo ipo katika Kata ya Nemba kuna wanafunzi 5,248 katika shule moja na shule ya Nyakanazi ambayo ni Nusaunga inawanafunzi 6,063.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu imagine huyu Mwalimu Mkuu anawezaje kuongoza shule ambayo ina watoto 6,063, 5,000, 4,000? Lakini pia hao walimu wana mzigo kiasi gani ambao wanafundisha? Hawa watoto ni kweli wanafundishwa au wanakwenda pale wanashinda wakicheza? Ndugu zangu mlione hili kama dharura, tusaidieni Mkoa wa Kagera hasa katika Wilaya ya Biharamulo, tujengewe shule, hasa kwa miradi wa EP4R kabla haijaisha tusaidie. SEQUIP tusaidie kusudi tuweze kujenga shule kwenye kata moja kwa mfano yenye watoto mpaka 6,000 tunaweza kujenga shule nyingine tatu ndani ya kata ili kunusuru hao watoto wasiwe wanaenda wanashinda shuleni tu wanacheza waweze kupata elimu ile iliyotarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwisho; Mkoani Kagera mnatujengea chuo cha VETA kikubwa kizuri cha viwango. Sasa niiombe Serikali yangu tukamilishe kile kituo cha VETA ili kusudi kiweze kuanza kutoa elimu na wanafunzi waweze kupata elimu ya ufundi iliyotarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)