Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2022/2023 kwa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote kwa kuandaa bajeti hii. Sambamba na hilo, naomba niendelee kuipongeza Serikali yangu Tukufu chini ya uongozi wa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa sana katika elimu pamoja na ufinyu wa bajeti, lakini kazi inaonekana, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 76 wa hotuba hii, Wizara imebainisha kwamba ina dhamira ya dhati ya kuongeza fursa na ubora wa elimu ya awali, elimu ya msingi na elimu ya Sekondari, naipongeza sana. Ushauri wangu kwa Wizara, nilikuwa naomba Wizara ione umuhimu wa kuifanya Kurugenzi ya Elimu ya awali iwe peke yake ili kusudi kuipa nguvu ya usimamizi wa karibu na iwe na bajeti ya peke yake. Kwa sababu elimu ya awali ndio msingi ambapo mwanafunzi akitoka elimu ya awali, akienda katika elimu ya msingi atakuwa ameandaliwa vyema, hivyo tutakosa wale wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika, maana yake elimu yetu itakuwa bora sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba niishauri Serikali ione umuhimu wa kuwa na kurugenzi maalum ambayo itashughulikia elimu ya awali badala ya Kurugenzi kuwa na Elimu ya Awali, Elimu ya Sekondari, Elimu na Msingi na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nizungumzie kuhusu uhaba wa watumishi wakiwemo walimu na wakufunzi; imezungumzwa lakini pia Kamati ya kudumu ya Huduma za Jamii pia imezungumzia hili jambo. Ushauri wangu ni kwamba ili kuwapunguzia walimu mzigo, kuna baadhi ya maeneo ambapo walimu wanafundisha zaidi ya wanafunzi 100, mwalimu mmoja, lakini ratio tunajua kabisa kwamba elimu ya msingi ni wanafunzi 45 na Sekondari ni 40. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba hebu Wizara iangalie upya ile ikama, kwamba katika yale baadhi ya maeneo ambayo walimu wamezidi, basi waweze kuwa-regulate ili mwisho wa siku tuweze kupunguza hili suala la mzigo kwa baadhi ya walimu kufundisha wanafunzi wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo katika ukurasa wa 33 wa hotuba hii umezungumzia kuhusiana na udhibiti ubora wa shule pamoja na Vyuo vya Ualimu, pamoja na Serikali kuhakikisha kwamba Elimu ya Awali Msingi na Sekondari na Walimu inafuata kanuni na miongozo iliyopo. Nina ushauri kuhusiana na udhibiti ubora wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa ya Kamati imeonesha kwamba fedha kiasi cha Shilingi bilioni moja kwa ajili ya ukaguzi kwa mwaka 2021/2022 hazikutolewa. Kwa hiyo, naiomba Serikali na Wizara kwa ujumla, hebu watoe fedha hizi, kwa kweli wakaguzi tunahitaji kuwawezesha kifedha ili kusudi waweze kukagua hizi shule zetu na waweze kutoa ushauri ili mwisho wa siku ule upungufu utakaoonekana uweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naishauri Serikali itoe fedha kwa sababu kuna baadhi ya maeneo katika Halmashauri, magari yale ya ukaguzi yamelala kwa sababu hakuna fedha za kuziendeshea, lakini pia kuna baadhi ya maeneo kutoka Halmashauri ya Wilaya ni mbali na Makao Makuu, kwa hiyo, wanapokwenda kukagua, sometimes wanakuwa hawana fedha. Kwa hiyo, zile fedha zikija kwa wakati, ina maana kwamba wakaguzi hawa watatimiza malengo yao na hatimaye ufanisi wa elimu utatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kuzungumzia ni kuhusu miundombinu ambayo ni pamoja na vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, maabara, mabweni, madawati, meza za walimu pamoja na maktaba. Natambua juhudi za Serikali, lakini bado kuna upungufu. Hata hivyo, tuendelee kuwapongeza baadhi ya wadau zikiwemo benki mbalimbali ambazo zimekuwa ziki- support katika masuala mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa nilitamani nizungumzie kuhusu maktaba. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, amezungumzia kabisa kwamba katika ukurasa wa 26 amezungumzia kuhusiana na suala la Maktaba na kwamba katika shule wameweza kutenga Maktaba 171.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ushauri kuhusiana na suala zima la maktaba. Maktaba zilizokuwepo katika Shule za Msingi na Sekondari zitawasaidia hawa watoto kuweza kujifunza mambo mengi. Takwimu au taarifa mbalimbali zinaonesha kwamba miongoni mwa watu ambao ni wavivu wa kusoma, Watanzania ni miongoni mwao. Ni kwamba Watanzania wengi wanapenda waende wakaangalie gazeti, zile headings tu za pale juu na yale magazeti ya udaku, lakini vile vitabu ambavyo vinaweza vikamwongezea maarifa na taarifa ambapo vinaweza vikapatikana katika maktaba, inabidi tuwandae watoto wetu mapema ili kusudi waanze kuwa na utamaduni huo waweze kujisomea na hatimaye iweze kuwaongea maarifa na taarifa. (Makofi)

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu kumpa taarifa mchangiaji ya kwamba, mchango wa magazeti ya udaku kwa Taifa hili ni mkubwa. Magazeti ya udaku siyo tu yanaandika habari za ovyo, yana habari za elimu na afya ambazo zinaweza zikamsaidia mtoto kujifunza. Kwa hiyo, naomba asijaribu tu kushusha hadhi ya magazeti haya kwa sabau yametoa mchango mkubwa kwa Taifa letu. Ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Toufiq, taarifa.

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niendelee. Sikuwa na nia ya kuyadhalilisha magazeti haya, badala yake tunachotaka wanafunzi wajifunze kwenye vitabu mbalimbali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)