Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa hizi dakika chache za kuchangia katika hoja ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda pamoja na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anafanya kazi kwa bidii kuwapigania Watanzania na kulipigania Taifa letu, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwashukuru ndugu zangu Mawaziri kwa namna wanavyofanya kazi kwa bidii kumsaidia Mheshimiwa Rais ili kutimiza ndogo ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuchangia kwenye hoja iliyo mbele yetu ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara. Nataka nijikite sana kwenye suala la Liganga na Mchuchuma. Liganga na Mchuchuma imekuwa hoja ya muda mrefu sana pengine watu hawajui Liganga ni nini? Unaposema Liganga ni mlima wa chuma, ni mlima wa iron ore, si chuma ya kuingia chini kuchimba ni mlima wa chuma na uposema Mchuchuma ni mlima mwingine wa makaa ya mawe ambavyo hivi viwili mlima wa chuma pamoja na mlima wa makaa ya mawe ya kuiyeyushia hiyo chuma yamewekwa na Mwenyezi Mungu kwenye eneo moja ili kazi iwe rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sana, ni vizuri pia kugundua kwamba, uzinduzi wa Liganga umefanyika 1860 karne ya 18, hiki chuma cha Liganga kikagunduliwa hapa Tanzania na uvumbuzi wa hii Mchuchuma kwa maana ya makaa ya mawe ni 1898. Ina maana Mwalimu Nyerere akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa anajua, Mzee Mwinyi alikuwa anajua, Mzee Mkapa alikuwa anajua, Mzee Jakaya Kikwete alikuwa anajua, Mzee Magufuli alikuwa anajua na Mama yetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan pia anajua kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kujiuliza ni kwa nini pamoja na hiki chuma kugunduliwa muda mrefu karne ya 18, lakini hatujachimba na mahitaji ya chuma ni makubwa hapa Tanzania, ni kwa nini hasa? Kwenye kuzungumza kwangu kwa dakika chache nitawagusa baadhi ya watu siyo kwa ubaya bali kwa lengo la kusaidia nchi yetu. Nipo hapa Bungeni kwa lengo la kusaidia nchi na si vinginevyo. Kwa hiyo katika kuzungumza nikimgusa mtu nisifahamike nimemgusa kwa ubaya bali nimemgusa kwa maslahi mapana ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nitoe takwimu kidogo ya uingizaji wa chuma Tanzania. Kwa mfano, mwaka 2018 tumeingiza chuma cha thamani ya dola milioni 401.2 hapa Tanzania, tumenunua sisi. Mwaka 2019 tumeingiza chuma ya thamani ya dola milioni 491.9 hapa Tanzania. Mwaka 2020 tumeingiza vyuma vya thamani ya dola ya milioni 423.4 hapa kwetu Tanzania. Mwaka 2021tumeingiza chuma ya dola ya thamani ya milioni 7.8. Mwaka 2022 tumeingiza chuma ya thamani ya dola milioni 235.7 hapa kwetu. Kwa hiyo kwa miaka hii mitano tumelipa fedha ya kigeni kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi kwa ajili ya chuma, dola bilioni 2.2 kutokea hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtu yeyote mwenye akili na anayejua kuzitumia, jambo hili haliwezi kuruhusu kufanyika kama chuma ipo hapa Tanzania. Sasa unihurusu niongee machache kidogo, ni kwa nini sasa hili jambo halijafanyika? Hebu nikupe mawazo, kwamba, tumeanza na reli, ujenzi wa reli standard gauge a good idea very good idea na si kinyume na hapo. Kwenye ujenzi wa reli, component kubwa inayotumika ni chuma, sasa ilikuwaje tukaanza kujenga reli kwa kuagiza chuma kutoka nje ya nchi badala ya kutengeneza chuma chetu kwa kuchimba ndiyo tukaanza na reli, ilikuwaje? Ni kitu gani kinatokea mpaka priority ya kwanza inakuwa ya mwisho na ya mwisho inakuwa ya kwanza. Kinachosumbua ni kukosa Maono ya Taifa, Mipango ya Taifa na Dira ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, simlaumu mtu yoyote. Nataka sasa unisikilize vizuri, kwa mfano, kama kungekuwa na maono ya Taifa juu ya viwanda maana yake kungekuwepo maono ya muda mrefu yanayoelezea juu ya chuma kilichopo Tanzania. Kwa hiyo, tusingekuwa tumeanza na reli, tungekuwa tulianza na fedha ya kuchimba chuma ili chuma chetu kije kitengeneze reli zetu, tungeokoa mabilioni ya shilingi tunayoyasema hapa. Nchi yetu inahitaji maono au agenda ya Taifa ya pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikiliza, jambo hili linaonekana kwamba its nonsense, its chasing wind lakini sikiliza niwaambie nchi nyingi zilizoendelea zina maono ya nchi zao ya muda mrefu. Hakuna nchi duniani iliyoendelea kwa muda wa miaka mitano au kwa muda wa miaka kumi. Nchi huwa zinaendelea kwa kuweka maono ya miaka mingi, unaiona nchi kwa mbali, wanafunzi wataiona nchi kwa mbali, wasomi wataiona nchi yao kwa mbali. Tukifanikiwa kuiona nchi kwa mbali tunaweza kuisukuma Tanzania kuipelekea mahala ambapo inatakiwa kuwa.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Kingu.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa msemaji kaka yangu Askofu Gwajima, kuonesha kwamba pia kuna mahali tuliteleza, sisi tumefuta hata tume hiyo ya kutengeneza mipango ya muda mrefu wa nchi. Leo tunapozungumza kwenye Taifa letu hatuna kitu kinaitwa Tume ya Mipango ambayo ndiyo wanatengeneza plans za nchi za miaka hamsini na kwenda mbele, we don’t have Tume ya Mipango.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gwajima, taarifa hiyo.

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Kingu ana taarifa nyingine za namna hiyo aendelee kunipa, naendelea kuzikubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kinachosumbua sana ni mipango ya muda mrefu. Tungekuwa na mpango wa muda mrefu wa hii Mchuchuma ni aibu. Nikupe mfano; kuna Paris Agreement on the use of coal ambayo imeweka ukomo wa kutumia makaa ya mawe na ukomo huo ni 2030. Hebu jaribu kuwaza tangu makaa ya mawe ya kwetu yamevumbuliwa karne ya 18 mpaka yanataka kufikia ukomo hatujayatumia bado, what can you call this, hiki kitu unaweza kukiitaje? Kwamba Mungu amewawekea mlima wa chuma, halafu amewawekea moto wa kuyeyusha hiyo chuma palepale, hamwezi kuitumia mpaka unafika wakati umefika ukomo wa kutumia 2030, hatujaitumia, jambo hili hatutakiwi kuliruhusu hata kwa dakika moja, hata kwa sekunde moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kinatuleta mpaka hapa, kukosa maono. Naomba viongozi wetu waliopo Mawaziri, Naibu Mawaziri waliopo Serikalini pamoja na mama yetu mwema, mama anayewapigania Watanzania, mama Samia Suluhu Hassan, zawadi peke yake tunayoweza kuipa nchi hii kwa sasa hivi ni maono ya nchi ili watu waweze kuiona nchi kwa mbali nawaweze kupanga mipango yao sawasawa na maono ya nchi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gwajima subiri kidogo, Mheshimiwa Waziri.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitambue mchango mzuri anaoutoa Mheshimiwa Mbunge na Mtumishi wa Mungu Askofu Gwajima; lakini nilitaka niweke tu kumbukumbu sawa kwamba Taifa letu mara zote limekuwa na mipango ya muda mrefu na mara zote tangu uhuru limeongozwa na viongozi wenye maono. Kumbukumbu mbili hizo; moja, tumekuwa na mipango ya muda mrefu na ndiyo maana tulikuwa na Dira ya 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dira ya 2025 ilitungwa wakati wa Mkapa na miaka yote hii ikamegwa kwa miaka mitano mitano; na utekelezaji wake ukianza na dira ya kwanza, na ya pili na hata tunayoenda kumalizia, ilikuwa na mtiririko ambayo ukienda kwenye headings zake zimeongelea mpaka na hizi habari za viwanda, habari hizi zote ambazo tunaongelea za kukuza uchumi na hata sasa tunapomaliza 2025 tayari tumeshaanza kuandika dira nyingine ambayo kimsingi kwenye mijadala tunaangalia ama tuandike kwa utaratibu wa miaka 20, 20 au tuandikie tuoanishe na Dira ya Afrika iende 2063. Kwa hiyo, mipango ya muda mrefu ipo kwenye nchi yetu na hii ndiyo inayozaa utekelezaji huu wote ambao tunaoufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa maono, nchi yetu isingeongozwa kwa maono tusingekuwa hivi tulivyo leo, imeongozwa kwa maono ndiyo maana tumefika hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambieni ndugu zangu Watanzania, tusipende kujidharau, nchi zote majirani; SADC na Afrika Mashariki wanapenda maono ya Tanzania. Actually, wao wanaiona Tanzania ndiyo mfano. Kwa hiyo, tusijidharau. Ila tunapopeana fursa za kujirekebisha zaidi, turekebishe ili twende kwa kasi zaidi, lakini siyo kwamba nchi haijawahi kuwa na viongozi wenye maono na kwamba nchi haijawahi kuwa na mipango. Nchi nyingi tu hata mipango wanayotekeleza mingine wame-copy kutoka Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niliona tu niyaseme hayo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Waziri naamini umeeleweka. Mheshimiwa Askofu Gwajima, taarifa ya Mheshimiwa Waziri hiyo.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimalizia, kwa mfano sasa hivi, Mheshimiwa Rais tayari ameshaweka kwenye pipe line utekelezaji wa hii miradi mikubwa, yote hii tunaenda kuitekeleza. Tunatekeleza Liganga, tunatekeleza LNG; hivi tunavyoongea, inaenda kutekelezwa siku siyo nyingi. Yote hayo ni maono na ni utekelezaji wa mipango…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, nafikiri umeeleweka, taarifa hiyo Mheshimiwa Gwajima.

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu kaka yangu Waziri wa Fedha na Mipango kwa staha kubwa kwa sababu yeye ni mwakilishi wa Serikali. Amethibitisha tu kwamba Mpango uliyopo ni mpaka 2025 na wanajiandaa kuandika Mpango mwingine. Amenithibitishia kwamba hatuna mpango wa miaka 50, hatuna mpango wa miaka 100. Kwa hiyo, namshukuru sana kwa kunisaidia kwa hilo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikae kwenye hoja yangu. Ninachosema mimi, sidharau kilichofanyika na Serikali. Ninachosema, tukiwa na mipango ya miaka 50 au miaka 100, wanafunzi wakaiona nchi yetu kwa mbali; kwa mfano tukiwa na mipango ya muda mrefu...

MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia, muda ulikuwa umeenda, lakini malizia dakika moja.

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona nikichangia muda unapungua, itabidi niombe Kanuni muda unapopungua inakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tu kwamba kwa ufupi tukiwa na mipango ya muda mrefu juu ya viwanda, wanafunzi wanaosoma shule wataiona nchi yao kwa mbali na watajua wasome nini kwa sababu wanaweza kuyasoma maono ya Taifa. Hicho ndicho ninachosema. I am not attacking anybody, I am trying to improve kwamba mahali tulipo ni pazuri, lakini tukiwa na mipango. Tungekuwa na mipango juu ya hili, tungekuwa tumeanza na kuchimba chuma chetu ili chuma chetu kitumike kwenye reli, hii fedha 2.2 billion dollars iliyoenda nje kununua chuma ingekuwa imebaki hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)