Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kiafya kuwepo hapa mchana huu kujadili wasilisho la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Pia nimshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake Makamu wa Rais, Waziri Mkuu kwa imani yao na hata wakaona nastahili kuteuliwa kuwa Naibu Waziri, kusaidia kwenye Wizara hii. Ahadi yangu ni kwamba nitamsaidia ipasavyo Waziri wangu kutekeleza majukumu kwa bidii uaminifu na uadilifu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, shukrani kwa wananchi wa Butiama na Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Butiama kwa imani yao kwangu na leo ipo Kamati ya Siasa hapa, nawaahidi tu sitawaangusha. Maendeleo ya Butiama yanabaki kuwa kipaumbele changu cha juu katika utekelezaji wa majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, naungana na Wabunge wote waliozungumza, kwa kutambua mchango wa kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tunawashukuru sana na tutaendelea kuthamini mchango na mawazo yao ili kuboresha zaidi utendaji wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umetolewa ushauri na Kamati na wasemaji mbalimbali walipata nafasi ya kuzungumza. Kwa uchache wa muda sitawataja, lakini itoshe tu kwamba majibu yetu bila shaka tutayaandaa kwa maandishi na kuwatambua wote waliochangia. Kamati imezungumza na nitajikita kwenye maeneo mawili ya NIDA pamoja na Uhamiaji. Imetajwa kwamba Wizara na Serikali ifanye juhudi za kupata shilingi bilioni 5.3 ambazo hazijatolewa ili NIDA itekeleze majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, naomba nikueleze pamoja na Bunge lako Tukufu kwamba, baada ya ushauri huo katika robo ya tatu zaidi ya Sh.2,382,000,000 zimetolewa na kupelekwa NIDA ili kutekeleza majukumu yao na Wizara imewasilisha maombi Hazina ili Sh.2,712,000,000 zilizobaki pia ziweze kutolewa katika robo ya nne kuwezesha NIDA kutekeleza mpango wao wa bajeti.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuwafikia wananchi wenye vigezo vya kutambuliwa na kusajiliwa ili wapewe vitambulisho vya Taifa, hili linaendelea kufanyika. Tunafahamu NIDA imeanza kwenye Wilaya zote 139 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wilaya za Zanzibar. Hata hivyo juhudi za kuboresha zile ofisi zinaendelea na kama tulivyosema katika bajeti ya mwaka ujao, uboreshaji wa bajeti umekuwa mkubwa kabisa, zaidi ya Shilingi Bilioni 56.4 zimetengwa kwa ajili ya shughuli za NIDA na humo ndani kuna zaidi ya Sh.42,000,000,000 zinazokusudiwa kwenye vitambulisho vya uraia, matarajio yetu ni kwamba fedha hizi zitatoka hasa baada ya changamoto ya kimkataba iliyokuwepo kati ya NIDA pamoja na Mzabuni shughuli hizo sasa zinaweza zikaendelea kutekelezwa ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo vipo vitambulisho zaidi ya 750,000 na Waziri amesema hapa asubuhi kuwahimiza wananchi ambao hawajachukua vitambulisho hivyo wakavichukue, ni matarajio yetu kwamba vitambulisho hivi vinatolewa kwa sababu vinahitajika hakuna sababu yoyote vitambulisho kubaki kwenye ofisi zetu za Wilaya.

Mheshimiwa Spika, kuhusu wahamiaji haramu imezungumzwa hapa kwa uchungu sana na sisi linatugusa, lakini wakati mwingine nchi inabanwa na Sheria za Kimataifa na mikataba ambayo nchi imeingia duniani huko, kwamba ukishamkamata huwezi ukawezesha kama Mheshimiwa Muharami ameshauri pale. Hata hivyo, tunatafakari hayo, kama nchi nyingine zinawasafirisha, zinawapitisha, kwa nini sisi ndio tuchukue mzigo wa kuwachukua na kuwahifadhi kwenye majela yetu, tuwalishe halafu kuondoka bado tuwagharamie.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, sasa hivi hawa wafungwa wa Kiethiopia zaidi ya 4,025 waliopo kwa usafiri wa anga ndio unasema kwenye hii mikataba wanastahili kulipiwa nauli shilingi Bilioni 6.35 na tukiwapeleka kwa barabara si chini ya Shilingi Bilioni 3.2 sasa zote hizi zingeweza kufanya mambo mengine kwa ajili ya Watanzania. Hata hivyo tunaendelea kuwasiliana na Serikali ya Ethiopia ili waje wachukue raia wao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu vitendea kazi kwenye Uhamiaji tunaendelea kuboresha mambo haya, mwaka huu pekee magari sita yamenunuliwa na mwaka ujao tumepanga kununua magari 30 na ujenzi wa makazi na Ofisi za Uhamiaji ngazi wa Wilaya na Mikoa kama tulivyosema kwenye bajeti yetu vitaendelea.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nashukuru sana kwa nafasi uliyonipa. (Makofi)