Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kuwapongeza Waziri Mheshimiwa Masauni, Naibu Waziri Mheshimiwa Jumanne Sagini, pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kutuletea hotuba ya bajeti ili tuweze kuijadili na kuishauri Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, nitaanza na mambo yafuatayo; kwanza ni uhusu Jeshi la Polisi; changamoto kubwa ni uchakavu mkubwa wa makazi na upungufu mkubwa. Katika Wilaya ya Kilolo hawana kabisa nyumba za askari wala ofisi ya OCD yalipo Makao Makuu ya Wilaya karibu miaka 20 sasa.

Mheshimiwa Spika, kuna ofisi za Serikali zinatumika kama kituo cha polisi. Eneo lipo lakini halijalipiwa fidia. Sasa tunaomba Serikali itoe pesa ya kutosha kwa Mkoa wa Iringa ili kazi za Jeshi la Polisi ziendelee.

Mheshimiwa Spika, kituo cha polisi Ruaha Mbuyuni ni kituo mtambuka, kinahudumia Jimbo la Mikumi na Jimbo la Kilolo, lakini hakina gari (eneo kutoka kituo kikuu ni mbali sana). Pia Kituo cha Polisi Kitonga ni muhimu sana na kinahitajika kutokana na ajali za mara kwa mara na ulinzi wa abiria na mali zao.

Mheshimiwa Spika, jeshi hili lina upungufu mkubwa wa askari kwa sababu kuna kesi nyingi za mauaji na ubakaji upelelezi unachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, kwa Jeshi la Zimamoto tunashukuru sasa hivi Kamanda ana usafiri pongezi, lakini jeshi hili halina magari ya kutosha ya kuzimia moto, yaliyopo ni machakavu sana.

Mheshimiwa Spika, katika mkoa wetu tunayo misitu ya mazao ya mbao katika Wilaya ya Mufindi na Kilolo na kumekuwa na matukio ya mioto mara kwa mara, lakini sasa hivi Serikali imejenga shule, mabweni pia tunasambaza umeme vijijini kwa hiyo magari ya uokozi ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, pia tunayo barabara ya Kitonga ambayo mara nyingi kumekuwa na ajali za mara kwa mara na kusababisha barabara kutopitika karibu siku nzima, hivyo muhimu jeshi hili kupatiwa gari la uokozi (crane).

Mheshimiwa Spika, jeshi hili lina uhitaji mkubwa wa nyumba na askari. Pia wana viwanja tayari katika Wilaya ya Kilolo na Mufindi lakini pesa ya ujenzi inahitajika.

Kwa upande wa Jeshi la Uhamiaji; Jeshi hili lina changamoto ya kutokuwa na magari katika Ofisi za Wilaya ya Kilolo na Mufindi. Nyumba za watumishi pia wana viwanja Wilaya ya Mufindi lakini hawana pesa. Wana madeni mengi na magari mabovu. Waongezewe OC na wapatiwe kwa muda unaotakiwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Jeshi la Magereza; changamoto kubwa ya Jeshi hili ni makazi ya askari, msongamano wa mahabusu unaotokana na wahamiaji haramu, wanahitaji vitendea kazi vya kilimo kama matrekta ni machakavu, Mkoa wa Iringa ni baridi kali, wafungwa wanahitaji masweta mazito na mablanketi, wanapata nimonia na hawana bima za afya na pia wana zahanati lakini hakuna ruzuku ya Serikali ya kusikia pamoja na kusaidia raia.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali ibadilishe matumizi ya Gereza la Kihesa Mgagao lililopo Wilaya ya Kilolo, Mkoa wa Iringa kwa sababu maeneo yote waliyokaa wapigania uhuru wa Kusini mwa Afrika ikiwemo nchi za Afrika ya Kusini, Msumbiji na Angola katika mikoa yote wamejenga vyuo vikuu na shule na vyuo vya kawaida na nchi hizo zikisaidia kama maeneo ya Mazimbu kipo Chuo Kikuu, Dakawa ipo shule ya wasichana na chuo, Kongwa ipo shule; kwa nini Kilolo tu ndiyo liwekwe gereza? Tunaelewa yapo makubaliano kwa nini hayafanyiwi kazi? Kama sitapata majibu nitashika shilingi ya mshahara wa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, wadau wanaosaidia Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa ni pamoja na Kampuni ya ASAS imesaidizi sana ujenzi wa vituo vya polisi na dawati la mkoa na kadhalika. Pia Kampuni ya Majembe Auction Mart imekarabati gari la polisi Kilolo ambalo litapelekwa kituo cha Ilula. Aidha Silver Land wamesaidia gari la kituo cha polisi Ifunda.

Mheshimiwa Spika, Dkt. Ritta Kabati amefanya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Semtema katika Kata ya Kihesa na kadhalika. Je, Serikali inautambua? Inahamasishaje wadau wengine waendelee kusaidia jeshi hili?

Mheshimiwa Spika, kuhusu stika za Wiki ya Nenda kwa Usalama; je, Serikali inatambua stika zinazouzwa katika Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani zinauzwa na wala mtu halipi kwa control number wala risiti?

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.