Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa mwisho kwa siku hii ya leo kabla Serikali kuanza kujibu.

Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi wameongea kuhusiana na uadilifu wa Jeshi la Polisi na kweli wewe ni shahidi, malalamiko ya raia kwa askari yamekuwa ni mengi sana, lakini bado hata askari wenyewe wana malalamiko yao. Wakati mwingine unakuta raia wanalalamikia askari kwa sababu ya kubambikwa kesi na mambo mengine. Ukienda kule katika Majimbo yetu ukimkuta askari kwenye kijiji fulani labda askari Mkuu wa Kituo ni kama Mungu mtu hivi, yaani ukikorofishana na yeye ni kwamba wewe wakati wowote unaweza ukabambikiwa kesi na ukaozea ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini wakati mwingine kuna malalamiko kwa raia kuhusiana na ajira za askari, sasa hivi kila Mbunge hapa anaandikiwa ki-memo na wapiga kura wake, naomba unisaidie unifanyie mpango nipate ajira ya uaskari. Tatizo limekuwa kubwa, utaratibu wa ajira haueleweki, kuna hali fulani ya sintofahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile kuna malalamiko ya wafungwa magerezani, wafungwa na wenyewe ni binadamu wana haki zao, lakini vile vile kuna malalamiko ya maaskari wenyewe kupanda vyeo, wakati mwingine wanasema kabisa kuna kupanda vyeo kwa sababu ya upendeleo fulani. Kwa hiyo kuna sintofahamu, nimejaribu kufuatilia na kuona tatizo ni nini, kuna chombo tunatakiwa tukiunde na chombo hiki ni lazima kiwepo kwa ajili ya kusimamia kitu wanaita code of conducts kwa ajili ya askari wetu au jeshi letu la Polisi na Magereza.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri kama tungeanzisha kamisheni ambayo inaitwa Police Force and Prisons Service Commission ambayo itasimamia code of conducts ya askari, suala la kupanda cheo, kuhamishwa lisiwe suala la kufahamiana, uwe ni utaratibu ulio sahihi unaoeleweka na ulio wazi kwa Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kenya, Nigeria na nchi nyingine kama Jamaica na maeneo mengine wameunda kamisheni kama hii ambapo hata sisi tuna Tume ya Utumishi, mtumishi akiwa na malalamiko yake anapeleka kwenye Tume akiwa na kesi au tatizo anapeleka kwenye Tume, anatafutiwa haki yake, lakini Jeshi la Polisi ni kwamba, leo Rais wa nchi akitaka kutafuta IGP anatafuta wale watu ambao yupo karibu nao, wakati kumbe kungekuwa na chombo hiki, kingemsaidia Rais kupendekeza majina matatu au manne halafu Rais anasema katika haya mawili, matatu, manne mlioniletea yeye anakuwa na uhuru wa kuteua mmoja kuwa IGP.

Mheshimiwa Spika, leo IGP akiwa na tatizo na askari wa chini, hawawezi kumlalamikia IGP, lakini pangekuwa na chombo hiki, angepeleka malalamiko yake, chombo kikampa haki. Kwa hiyo naona kabisa kwamba tuna haja ya kuwa na kamisheni ya utumishi wa Jeshi la Polisi na Magereza, mfano mwingine kuna watu wanahamishwa kwa sababu tu ya ugomvi kati ya yeye na bosi wake, pangekuwa na chombo hiki kingeweza kusaidia kuondoa hayo matatizo.

Mheshimiwa Spika, chombo hiki rahisi tu kuunda, tungetunga sheria, tungepitisha hapa, tukawa na chombo hiki kinachoweza kusimamia code of conducts ya maaskari wetu. Kkuna maaskari waliostaafu Jeshi, kwa mfano ma IGP waliostaafu muda mrefu, wangekuwa wanateuliwa wanaendesha chombo hiki kama ilivyo kwenye Tume ya Utumishi, kuna majaji wastaafu, wanasimamia taratibu za utumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kulalamika askari wanaonea raia, raia wanalalamikia askari kila mmoja anamlalamikia mwenzie na msuluhishi wa hili tatizo hatumwoni, njia kubwa ni kutunga sheria ya kusimamia au ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na kamisheni hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ombi langu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Maswa ni Wilaya Kongwe, hatujawahi kuwa na kituo cha Polisi, toka tumepata uhuru mwaka 1961. Nilishawahi kuuliza swali hapa, Maswa Kituo cha Polisi cha kwanza kilichovunjwa kilikuwa ni jengo la halmashauri, sasa hivi tumepeleka kwenye jengo la misitu, Ofisi ya Misitu ndio imekuwa kituo cha Polisi. Tunaomba watujengee kituo chetu cha Polisi ambacho kitasimamia shughuli zote za Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile nyumba za Polisi za Wilaya ya Maswa ni nyumba ambazo hazijakarabatiwa miaka na miaka, ni nyumba ambazo zimechoka, askari kupelekwa Maswa kwenda kufanya kazi, ukimpa nyumba ya Askari kuishi ni kama vile umempa adhabu. Tunaomba Wizara ya Mambo ya Ndani watujengee nyumba za wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)