Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara yetu hii ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Niende moja kwa moja katika michango yangu kutokana na uchache wa muda. La kwanza ningependa kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake kwa uwasilishaji mzuri ambao wameufanya.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana wakati nachangia bajeti kuu ya Serikali nilitoa indhari hapa kwamba kama sikuona mabadiliko katika matatizo ya wizi wa mazao ya kilimo na mifugo kule Zanzibar kama sikuona ufumbuzi wa kudumu katika bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri basi nitashika mshahara wake, sasa Mheshimiwa kwa masikitiko makubwa kwa kweli katika bajeti hii sikuona sehemu ambayo kuna mkakati maalum kwamba tunakwenda kuondoa tatizo la wizi wa mazao ya kilimo na mazao ya mifugo kule Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aje aniambie kuna mkakati gani wa kwenda kuondoa tatizo la wizi wa mazao, kwa sababu hili tatizo limekuwa ni kidonda sugu kule Zanzibar, wananchi wanalima sana, wanajitahidi kufuga, lakini wizi umekuwa mkubwa unawarudisha nyuma na hakujakuwa na suluhisho la kudumu ambalo linatia matumaini kwa wakulima wetu ambao wanajituma siku hadi siku kuweza kulima.

Mheshimiwa Spika, tukizungumzia food security tunakusudia kwamba usalama wa chakula ambao unategemea asilimia zaidi 70 ya wakulima wetu ambao wanalima. Sasa wewe unakwenda kwenye kilimo unalima, unakuta shamba lako limevunwa lote. Unakwenda kwenye mifugo unakuta mifugo yako kama ni kuku au ng’ombe wameondoka wote. Hapa juzi Mheshimiwa Mbunge wa Chambani aliuliza swali hapa na akaelezea changamoto za Chambani, kwa hiyo nazungumzia katika Jimbo langu la Donge, lakini hili tatizo ni tatizo sugu kwa Zanzibar nzima. Kwa hiyo ningependa Mheshimiwa Waziri aje anipe majibu ya kuridhisha hapa, tunakwenda kutatua vipi tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, suala lingine katika Jimbo langu la Donge ni sehemu ya machimbo ya mchanga, mchanga asilimia 90 unatoka katika Jimbo langu la Donge na Jimbo la Mheshimiwa Mbunge wa Bumbwini. Sasa kuna ajali nyingi zimekuwa zikitokea kutokana na magari ya mchanga kwenda kwa kasi na hivi juzi nimeenda kwenye hizi sherehe za sikukuu, nimezika wananchi wangu wawili kutokana na ajali za barabarani. Kwa hiyo ningeomba vile vile Mheshimiwa Waziri atakapokuja aniambie ana mpango gari wa kupunguza ajali katika eneo langu la Jimbo la Donge, lakini katika barabara ya Bububu - Mkokotoni ambayo kwa Zanzibar ndio inayoongoza kwa ajali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la tatu niongelee kuhusu Kituo changu cha Mahonda, Kituo cha Polisi Mahonda kimeanza kukarabatiwa na kuna ujenzi unaendelea hivi sasa lakini huu ujenzi unasuasua sana. Kwa hiyo, vile vile ningeomba Mheshimiwa Waziri aje aniambie kwamba je, ujenzi huu utaratibu ukoje isije ikawa unasema zile Tuzo na Tozo ambazo mpaka zipatikane ndio ujenzi uendelee, ningependa ujenzi huu uwe endelevu na umalizike kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho ni suala la ajira ambazo Mheshimiwa Simai hapa amelizungumzia. Kwa kweli ni tatizo kwa sababu imekuwa kama vile hii ajira wenzetu wa Makao Makuu wana mpango wao maalum ambao kwa kweli Majimbo, Wilaya na Mikoa hawaujui unaendaje. Nafasi za Polisi, Uhamiaji yaani utaratibu haufahamiki vema, kwa hiyo ningependa Mheshimiwa Waziri angejitahidi kuwe na uwazi katika masuala ya ajira kwa nafasi hizo za Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)