Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyoko mezani. Mimi pia nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi wanayoifanya, lakini kutuletea bajeti hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wetu wa Iringa zaidi ya asilimia 50 ni wanawake, tukianza na RC ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, lakini pia tunaye Kamanda wa Zimamoto, tunaye Kamanda wa Uhamiaji pamoja na TAKUKURU. Naomba Wizara ilete pesa nyingi sana katika Mkoa wetu wa Iringa ili wanawake hawa waweze kufanya kazi wanajituma sana pasipo kuwa na hakuna fedha za kutosha katika mkoa wetu. Kwa hiyo, naomba waletewe pesa ya kutosha ili kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo wenzangu wamesema, askari wetu wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana, hasa katika Mkoa wetu wa Iringa. Hakuna kitu kinachokatiza, wahamiaji haramu wamekuwa wakikamatwa kwa wingi sana kwenye Mkoa wetu wa Iringa. Kwa hiyo ninaomba; changamoto ya nyumba za polisi kila mkoa ipo ukiwepo Mkoa wetu wa Iringa. Askari anatoka katika lindo anarudi nyumbani anashindwa hata kufanya mambo mengine kwa sababu, kwanza anakaa chumba kimoja na watoto na isitoshe nikichukulia mfano hata katika pale FFU Kihesa, mimi nimezaliwa pale, tangu nimezaliwa zile nyumba hazijawahi kufanyiwa ukarabati, unakuta hakuna vyoo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawahurumia sana akinamama na watoto wanaoishi katika maeneo ya makazi ya askari. Kwa kweli ninaomba kabisa Serikali iwe na mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba, hizi nyumba za askari zinajengwa tena ni kwa majeshi yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukija katika Wilaya ya Kilolo unakuta miaka 20 katika makao makuu hakuna ofisi ya OCD. OCD anakaa TAZAMA Pipeline, DC yuko kwenye makao makuu. Wale mahabusu wanakaa TAZAMA Pipeline na hakuna gari la kuwapeleka yaliko makao makuu. Kwa hiyo, mimi naomba Wilaya ya Kilolo iangaliwe kwa karibu kwa sababu, kwanza kabisa wana eneo kwa ajili ya kujenga makao makuu ambalo bado halijalipiwa hata fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunayo ile Barabara ya Kitonga. Unakuta kila wakati ile barabara inakwama kwa sababu ya ajali nyingi. Kwahiyo, itatakiwa usalama, na hivyo lile eneo linatakiwa kuwa na kituo cha polisi kitakachokuwa karibu. Hii ni kwa sababu, ndani ya siku mbili ama tatu katika ile barabara kunatokea ajali. Jambo lingine kuna shortage pia ya askari polisi. Kwa hiyo, tunaomba askari polisi kwa wingi Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie kuhusu Jeshi la Magereza. Jeshi la Magereza changamoto zao kwanza ni makazi kama walivyo askari wengine, lakini pia naomba Jeshi la Magereza lichukuliwe kama jeshi la mafunzo, ni kituo cha mafunzo. Wale watu walioko pale wafundishwe, wapatiwe mikopo ili wanapotoka watoke na elimu lakini pia wapatiwe pesa ili wakaanze kuendeleza kile walichokipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile kuna tatizo la matrekta. Wanafanya kilimo kizuri sana lakini matrekta yao yote ni mabovu. Tunaomba pia waongezewe matrekta ili waweze kujikimu kwa chakula na waweze kujitunza wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tatizo jingine ni kwamba, wanatakiwa wapatiwe mablanketi na masweta. Mkoa wetu wa Iringa una tatizo kubwa sana la baridi, kwa hiyo unakuta wafungwa wanapata pneumonia na wana zahanati pale ambayo haina ruzuku kwa hiyo sasa hawana bima ya afya. Sasa tunaomba kile kituo kwanza kipewe ruzuku ili waweze kutibiwa pale katika Zahanati ya Magereza ambayo inatibu hata raia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunalo gereza letu ambalo liko pale Mgagao. Hili Gereza la Kihesa Mgagao unaona kwamba…

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Ritta Kabati kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Nusrat Hanje.

T A A R I F A

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, mzungumzaji anayezungumza nakubaliananaye na ninaomba nimpe Taarifa tu kwamba, anachokiongea ni very valid, ni cha halali kwa sababu, wafungwa hawaruhusiwi kabisa kutumia nguo yoyote ya uraiani hata ya kujifunika kujisitiri na baridi. Kwa hiyo, suala la mavazi ya kujisitiri kwenye baridi kama mablanketi na masweta na mavazi yao kwa ujumla ni muhimu sana, ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Ritta Kabati, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa sababu, ndilo tatizo kubwa lililopo hata katika Gereza letu la Iringa na magereza nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunalo Gereza la Kihesa Mgagao, Wilaya ya Kilolo. Tunaomba Serikali sasa ifanye utaratibu aidha, ilihamishe lile gereza au ibadilishe matumizi. Kwa sababu, naona lile gereza lilikuwa kama lilivyo, kuna maeneo ambayo waliishi wakimbizi wa Kusini mwa Afrika ambako maeneo yote unaona kwamba, wameweka kumbukumbu. Kwa mfano ukiangalia Mazimbu kuna campus ile ya SUA, lakini ukiangalia pia Dakawa kuna shule, kuna chuo, lakini pia ukiangalia pale Kongwa sasa hivi kuna kituo cha Ukombozi wa Afrika, kimetoka makao makuu. Sasa kwa nini Kilolo hilo gereza tusiende kujenga kwingine ili pale kuwe kuna kumbukumbu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kuna vyumba ambavyo alilala Nelson Mandela, kuna vyumba ambavyo walilala marais wengi waliokuja kupigania uhuru. Kwa hiyo, ninaomba kabisa kiwe kama kivutio na ikiwezekana sasa pale watu wawe wanakuja kuangalia iwe kama utalii kuliko ilivyo sasa hivi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana. Kengele imeshagonga.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga hoja mkono, lakini niliandika kwa maandishi. (Makofi)