Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono na ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa utaratibu mzuri alionao wa kuwa msikivu, mtu mnyenyekevu na mwenye mahusiano mazuri sana hasa kwa vyombo vya habari wakiwemo wamiliki na waandishi wa habari. Nakuomba PR hiyo uiendeleze ili tasnia ya habari iweze kuwa nguzo kuu katika ustawi wa Taifa letu. Nakuomba uendelee kuvishauri vyombo vya habari na waandishi wa habari kwamba kalamu zao ziangalie na kuzingatia uzalendo kwa nchi yao Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Michezo Malya kina upungufu mkubwa, lakini kubwa ni kukiboresha chuo hiki ili kiweze kutoa degree ya michezo. Chuo cha Malya ni kiwanda cha kuzalisha walimu wa kufundisha michezo mbalimbali katika shule za msingi, sekondari na vyuo. Michezo ikifundishwa vizuri shuleni, vijana wetu wajipe ajira hasa katika sanaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TFF haisimamii vyema uendelezaji wa mpira wa miguu badala yake imekuwa ni chama cha kukuza vurugu badala ya mchezo wenyewe. TFF imekuwa chanzo cha migogoro kati ya vilabu na vilabu, tofauti na matarajio ya wengi. Ikumbukwe mpira wa miguu ni mchezo unaopendwa na watu wengi lakini Watanzania hawafurahishwi na uongozi wa TFF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, programu ya timu ya under 15, 17, 21 haionekani kusimamiwa vizuri. Michezo ni furaha, ajira, utalii, afya na kadhalika, tofauti na kwetu hasa TFF imekuwa ikilalamikiwa kuhusu matumizi mabaya ya fedha.
Naomba Mheshimiwa Waziri akihitimisha majumuisho aniambie fedha zinatolewa na FIFA kwa miaka mitatu ya nyuma yaani mwaka 2013 - 2015 zililetwa na zilitumikaje? Tujue fedha za wafadhili mbalimbali walioichangia timu yetu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanaume na wanawake, tujue pesa za ligi kuu (VPL) mkataba ukoje hasa upande wa timu shiriki? Yapo malalamiko mengi kwa washiriki wa ligi ya VPL.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ligi daraja la kwanza iliyomalizika hivi karibuni imemalizika kwa migogoro ndiyo maana nimesema kuwa TFF badala ya kuendeleza soka inaendeleza migogoro na upendeleo wa dhati kwa baadhi ya timu. Naomba Mheshimiwa Waziri atueleze ni namna gani atakiendeleza Chuo hicho cha Malya? Pamoja na kutopatiwa pesa zake za OC, ni vyema wazabuni wakalipwa madai yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Michezo Tanzania (BMT) hivi kazi yake ni nini? Sioni wanachokifanya, wapo wapo tu. Sioni maendeleo katika michezo mbalimbali iliyo chini ya Baraza. Kila chama ni vurugu, siyo kwenye riadha, ngumi, wavu na kadhalika. Je, ni busara kuendelea na hilo Baraza hilo? Kama ni jipu, litumbuliwe. Naunga mkono hoja.