Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Kwanza nimpongeze Waziri na Naibu wake kwa namna walivyoanza kwenye Wizara hii wameanza kwa utulivu na usikivu mkubwa, wakienda kwa spirit hii tutakwenda mahali pazuri.

Mheshimiwa Spika, leo nina mambo mawili; moja ni la jimboni kwangu; Nimekufuata Mheshimiwa Waziri mara nyingi. Mwaka 2019 aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, alipotembelea jimboni kwangu katika Mji Mdogo wa Laela akiwepo na Waziri wake wa Mambo ya Ndani wakati huo Kangi Lugola, walitoa ahadi ya kuwarejeshea wananchi ekari 495 ambao ni mgogoro na Gereza la Moro kule Sumbawanga.

Mheshimiwa Spika, agizo hilo ni mwaka wa tatu na nimeuliza swali hapa Bungeni utekelezaji wake umekuwa ni sifuri, nimemfuata na wakati huo mtangulizi wake kaka yangu Simbachawene, nilimwambia jambo lile lina shida kubwa kwa sababu gereza mipaka yake imeingilia mipaka ya kijiji, ndiyo maana viongozi waliotangulia walitumia busara angalau kuwapa wananchi wale wa Msanda Muungano ekari 495. Nashindwa kujua tatizo liko wapi na kwa nini wanapata kigugumizi kufanya jambo hilo. Nmwombe kwa usikivu huo huo niliousema na namna ambavyo anafanya mambo yake kwa wakati mfupi huu, naomba jambo hilo tukali-close ili tuachane na mgogoro na wale wananchi.

Mheshimiwa Spika, Wizara wana mpango wa kwenda kuwekeza kwenye gereza lile, kama hawata-solve mgogoro na wale wananchi, impact yake itakuwa mbaya sana. Namwomba sana na nilikusudia kushika shilingi kwa jambo hili ila amenihakikishia kwamba baada ya Bunge tutakwenda kule ku-address lile tatizo.

Mheshimiwa Spika, jambo langu la pili ni suala la Jeshi la Polisi. Mfuko wa Tozo na Tuzo. Huu Mfuko na mara nyingi Naibu Waziri amekua ukijibu swali ambapo Waheshimiwa Wabunge wanaomba Vituo vya Polisi anasema tutajenga kwa kupitia Mfuko wa Tozo na Tuzo. Kinyume kabisa na Sheria ya Fedha Public Finance Act. Mfuko ulivyo, una takribani miaka 10 sasa; kwa jinsi ulivyotengenezwa hata kwenye Fungu Na. 28 la Jeshi la Polisi leo hakuna fedha hiyo ilivyooneshwa kwamba itapatikana, lakini three years consecutive Jeshi la Polisi limeweza kukusanya zaidi ya bilioni 32 toka kwenye Mfuko huo na mwaka jana tu wametumia zaidi ya bilioni sita bila ya kupitishwa na kuidhinishwa na Bunge. Hatuwezi tukapata tija ile tunayoitaka kwa sababu gani? Haya maendeleo ujenzi sijui wa Vituo vya Polisi, nyumba za polisi, hautakwenda kwa usawa kwa sababu itategemea na nani aliyepo kwenye menejimenti ya Jeshi la Polisi na ana utashi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, tungeweza kuivuruga hii bajeti, lakini italeta shida. Naomba CAG akakague huo Mfuko miaka 10 haujawahi kukaguliwa, haujawahi kufanyiwa reconciliation na fedha zinaingia na kutoka; ukienda kule Hazina wanasema hizi fedha ni za Jeshi la Polisi. Ukija Jeshi la Polisi wanakwambia zipo Hazina, kwa hiyo CAG ameshindwa kufanya hata auditing miaka yote hii. Mbaya zaidi huu Mfuko ni fedha zinazokusanywa kutokana na huduma za ulinzi, Benki na kwenye migodi. Kumekuwa malipo ambayo client anafanya moja kwa moja kwa Polisi yaani anawalipa anakwenda kulinda Polisi Benki analipwa Sh.10,000 wanakuja ku-deduct kwenye mkataba, jambo ambalo halipo kabisa kwenye finance. Public Finance Act inaeleza, ilibidi zile fedha wazikusanye, ziingie kwenye hiyo account, baadaye sasa Jeshi la Polisi ndiyo wawalipe wale askari kama ni risk allowance kuliko inavyofanyika sasa hivi ambayo client mwenyewe anasema haya nakupa shilingi 10,000 saini hapa, tutakatana kwenye mkataba; mambo ambayo ni yanafanyika locally, haitakiwi na nashangaa huko Jeshi kuna Wataalam wa finance? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwanza tukafanye hii audit; na kuna miradi mingi imekwama, mfano, tumetembelea juzi Ikungi, tumekuta jengo la Jeshi la Polisi la zaidi ya bilioni tu lilijengwa miaka saba iliyopita kutokana na Mfuko huo wa Tozo na Tuzo. Badaye viongozi wa wakati ule wameondoka, wamekuja wapya, wakatelekeza fedha za wananchi.

Mheshimiwa Spika, Jimboni kwangu, sijawahi pata hata senti moja hii fedha inayotokana na Tozo na Tuzo. Vituo vyangu vya Polisi karibu 11, tumejenga kwa nguvu za wananchi ndani ya Jimbo la Kwela kwenye Kata 28. Sasa tukileta hapa Bungeni tutakuwa na Mandate ya kui-discuss hii fedha, tuone kwanza upatikanaji wake na mgawanyo wake ukoje ili kila Mbunge aliyekuwepo hapa ajue huu Mfuko wa Tozo na Tuzo huu unamgusa vipi kwenye jimbo lake. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)