Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipatia fursa hii ya kuchangia kwenye Hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya pia Naibu wake kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya lakini yote kwa yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya ya kuhakikisha ya kwamba Tanzania tunaishi kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ninachangia mambo machache sana, nianze tu kwa kusema Jeshi letu la Polisi linafanya kazi kubwa sana. Nijikite kwenye kuzungumzia watumishi, Askari wetu waliopo kwenye maeneo yetu tunayotoka katika maeneo ya vijijini. Maeneo ya vijijini Askari wetu wanaishi katika mazingira magumu sana, pia ukiangalia Mishahara yao, ukiangalia kazi zao ni kwamba Jeshi letu la Polisi katika maeneo hayo ninayoyataja mara nyingi sana yanaendeshwa na wadau. Sasa hili limekuwa ni tatizo kubwa sana juu ya utekelezaji wa majukumu yao kama Askari, weledi kwa sababu mambo mengi yanaendeshwa kwa sababu ya wadau kutokana na changamoto ya kibajeti.

Mheshimiwa Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri ili kutunza heshima ya Jeshi letu hasa Askari wetu hawa, tuone namna gani sasa Serikali inaweza ikatenga fedha nyingi na kupeleka katika maeneo yale ili Askari wetu waweze kufanya kazi kwa weledi. Wanapotaka mafuta ni kwamba wanatafuta wadau, kila kitu ni wadau, Mheshimiwa Waziri kuna changamoto imeanza kuna mfumo umeanza wa kutoa hizi loss report. Hizi loss report Mheshimiwa Waziri kwa sasa utaona kabisa kwamba IGP amekaimisha mamlaka kwa OCS na OCS ameteua mtu kwa ajili ya ku-verify zile ripoti. Hasa ripoti hizi Mheshimiwa Waziri utaona kwamba huyu Askari aliyeteuliwa na OCS hajatengewa fungu la bundle, kuweka bundle ili aweze kuingia kwenye mtandao ku-verify zile loss repot. Maana yake ni nini tunawatengenezea mazingira ya Askari wetu hawa kwenda kuanza kutafuta wadau na kushusha heshima ya Jeshi. Niwaombe sana kuhakikisha ya kwamba wanatenga fungu la bundle, huyu mtu aliyeteuliwa ku-verify kwenye mfumo atengewe fedha asitegemee wadau.

Mheshimiwa Spika, pia nikazie kwa kusema kwamba Askari wetu hawa kuna suala zima la posho ya safari imekuwa ni changamoto Mheshimiwa Waziri. Tuhakikishe ya kwamba sasa Askari wetu hawa wanapotaka kwenda safari wanafanya kazi, tunatambua kazi ngumu wanazofanya huku, wanaposafiri sasa likizo maana yake ni kwamba wanategemea ile fedha watakayolipwa kwenye likizo lakini pia na posho ya safari iweze kuwasaidia katika ku-refresh mind zao kutokana kazi kubwa walizofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii utaona kabisa kwamba hata fedha zao za likizo zimegeuzwa kuingizwa kwenye mfumo wa madeni tena. Kwa hiyo tunaendelea kuwanyonya bila kutambua Askari wetu hawa wanafanya kazi kubwa sana. Nikuombe Mheshimiwa Waziri haya nenda ukayashughulikie kuhakikisha Askari wanalipwa posho zao za safari kwa wakati, likini pia moja kwa moja fedha za likizo zisiende kuingizwa kwenye mfumo wa madeni wapewe fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kusema kwamba tuna changamoto kwenye Jimbo la Msalala la ukosefu wa Kituo cha Polisi, hapa nikwambie Mheshimiwa Waziri ninaenda kukamata Shilingi ya Mshahara wako Mheshimiwa Waziri kama hautanipa majibu sahihi ya kwamba ni lini sasa Jimbo la Msalala tunaenda kuwa na Kituo cha Polisi.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kahama ina Majimbo matatu, Ushetu, Kahama na Msalala lakini utaona kwamba tuna Ma-OCD kote kule, lakini hakuna vituo vya Polisi, hapo hapo vitendea kazi magari hakuna na nimeona Mheshimiwa Waziri umesema kuna ununuzi wa magari. Niombe kwetu kule OCD anatembea na boda boda lakini mbaya zaidi ni kwamba tuna mgodi katika maeneo yale lakini pia hata gari anayotumia aliyopewa ni ngumu kwenda kuhakikisha kwamba wanafanya patrol katika maeneo yale. Tuna Leyland moja imeletwa, kule kwetu Leyland huwa inatumika kubeba matimba kwenda machimboni. Sasa hii Leyland inatumika kufanya operesheni katika maeneo ya porini, nikuombe Mheshimiwa Waziri mnapoenda kutoa magari toeni magari kuzingatia maeneo husika ya mazingira halisi ya maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Leyland haiwezi ikapita kwenye barabara zetu kule kwenda kufanya operesheni. Mheshimiwa Waziri kwenye magari yale naomba Jimbo letu la Msalala liwe namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala jingine la NIDA. NIDA kumekuwa na changamoto kubwa sana na nimuombe Mheshimiwa Waziri akisimama hapa na nitashika Shilingi ya Mshahara wake, atueleze ni kwa nini hili suala zima la NIDA limechukua muda mrefu. Leo hili mwananchi wetu kila jambo analotaka kulifanya ni NIDA, anapotaka kwenda kusajili line NIDA, anapotaka kwenda kufanya jambo lolote inahitajika kadi ya NIDA na kama wameshindwa hivi leo hii kweli Serikali watu wa Uhamiaji tunazidiwa na Club ya Yanga, Club ya Yanga inagawa kadi. Kama wameshindwa waje walau wajifunze kwenye Club ya Yanga kuona ni namna gani hawa Club ya Yanga wanafanya kuhakikisha wanawapatia kadi wanachama wao. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, niendelee kumuomba Mheshimiwa Waziri ninakuomba baada ya hotuba yako Mheshimiwa Waziri…

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi kuna taarifa ikitokea kwa Mheshimiwa Nicholaus Ngassa.

T A A R I F A

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimpatie taarifa mchangiaji kwamba kadi zinazotengenezwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa za NIDA zile zinaitwa smart card maana yake zinazosomana na mifumo. Kwa hiyo, ndiyo maana unaona inaweza ikatumika kadi ya NIDA kusoma mfumo kwenye PSSF, NSSF au kwenye leseni tofauti na kadi zinazotolewa na wananchi - Yanga ni kadi ambazo haziwezi kusomana popote kwenye mfumo.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, umepokea taarifa hiyo?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, taarifa ya Mheshimiwa Ngassa siipokei. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuwaomba, niendelee kuwaomba hivyo hivyo Chama chetu cha Mapinduzi kinatoa kadi hizi ambazo zinaendana na mfumo anaousema huyo. Pia niwaombe waje wajifunze kwenye Chama cha Mapinduzi kuona ni namna gani tunatoa kadi zile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala zima la Magereza. Wilaya ya Kahama ina Gereza moja na Gereza lile ni dogo sana, nimeenda kufanya ziara mle na nilimwambia Waziri kwamba kuna changamoto ya ukosefu wa majengo.

Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)