Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE: MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii. Kwanza kabisa ningependa kuchukua nafasi hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwana Masauni, pamoja na Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na timu yote ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kazi kubwa wanayoifanya. Nawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, mimi kwanza kabisa naomba nizungumzie suala la wahamiaji haramu. Nchi yetu imekumbwa na tatizo kubwa sana la wahamiaji haramu. Mpaka sasa tunavyozungumza kutokana na taarifa ambazo wamezitoa katika hotuba ya Waziri na taarifa ya Kamati, inanesha kuwa kuna wahamiaji haramu wasiopungua 4,025 ndani ya nchi kutoka katika nchi mbalimbali. Wenzetu nchi za jirani hawa wahamiaji haramu wanapokuja katika nchi zao huwa hawakai, wanawaruhusu wanaondoka lakini Tanzania tumejijengea utaratibu kwamba hawa watu wakija tunawapokea, tunawashtaki na tunawaweka katika magereza yetu. Hii inasababisha gharama kubwa sana kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi kama Ethiopia, katika sera yao ya mambo ya nje ni kwamba wanawaruhusu watu wao waende popote kule duniani wanakotaka, hawawakatazi. Kwa hiyo katika nchi nyingi sana wanapita na hawa wahamiaji haramu wa Ethiopia walio wengi hawana dhumuni la kukaa hapa nchini kwetu; nia yao kubwa wao wapite njia. Kwa sababu sisi Tanzania watu wetu wenyewe bado ajira hazijatosha. Kwa hiyo wao hawana nafasi ya kupata ajira katika nchi yetu. Kwa hiyo wanapita njia kuelekea nchi zingine. Kwa hiyo naomba Serikali sasa hivi iangalie ni jinsi ambavyo watawaruhusu hawa watu wapite waende kule wanakotaka badala ya kuwaweka magerezani na kutumia rasilimali zetu za nchi, kwa kuwalisha kwa muda wote ambao wanakuwepo magerezani na kukaa hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwangu pale Bagamoyo mpaka leo hii nina wahamiaji haramu wasiopungua 252 wako pale na wanakula tu siku zinaondoka. Kuna Waethiopia 237, kuna Wasomali 13, kuna Mburundi mmoja na kuna Mkenya mmoja, sasa wote hawa wanakaa wanaitegemea Serikali. Kile tunachokipata kuendesha mambo yetu katika nchi tunaamua kuwahudumia wao. Sasa kwa hiyo niiombe Serikali wafanye haraka iwezekanavyo kuwaondoa hawa watu, wanatutia hasara katika nchi. Kule wenzetu wanapokuwa wanatoka kwao kwa mfano Ethiopia wanawaachia wakifika mpakani wale Maafisa Uhamiaji wakiwa Mashekhe, Mapadri mpaka dua wanawaombea nendeni salama huko mnapokwenda mje kuinufaisha nchi yetu, sisi tunakuja hapa tunawazuia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili nataka kuzungumzia juu ya uzalishaji mali katika Jeshi la Magereza. Jeshi la Magereza linafanya kazi kubwa sana katika uzalishaji mali. Kwa hiyo, niiombe Serikali ili-support sana Jeshi la Magereza na nina imani kabisa kwamba watakapowa-support watu wa Magereza katika suala zima la uzalishaji, Magereza itajitosheleza kwa chakula, Serikali itaondokana na kuhudumia hawa watu. Wao wenyewe wanaweza wakajitosheleza. Wawape vifaa, wawanunulie Matrekta na vifaa vingine vyote. Mashamba wanayo ya kutosha ili waweze kuisaidia nchi katika suala zima la chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala jingine nataka kuzungumza ni suala la vitendea kazi katika Jeshi letu la Polisi. Kumekuwa na lawama kubwa zinazowapata Polisi wetu, Polisi inatokea tukio wanaweza wakachukua dakika 40, hadi dakika 50, lakini gari ileile moja imetoka imeenda katika sehemu nyingineyo. Kwa hiyo magari ni tatizo kubwa sana. Wapatie gari za kutosha ili waweze kuyawahi matukio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho, suala la hali ya usalama.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)