Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Twaha Ally Mpembenwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia. Kwa ufinyu wa muda nianze tu kwa kumshukuru kwanza Mheshimiwa Rais kama amiri jeshi mkuu kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya ndani ya nchi ili kuweza kuhakikisha kwamba vyombo vyetu vyote vya usalama vipo shwari na raia tupo salama vilevile. Pili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kuifanya katika jeshi la polisi. Nitakuwa mchoyo wa fadhila; nimpongeze sana Afande IGP Sirro kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya katika kuweza kuhakikisha kwamba anaboresha huduma za kipolisi; na tumeona mara nyingi sana anafanya reshuffle za hapa na pale ili kuweza kuhakikisha kwamba ufanisi unaweza kupatikana katika jeshi la polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naomba nichangie jambo moja la kitaifa zaidi, na hili ni jambo linalohusiana na mambo ya miundombinu ya Askari Polisi hasa katika vile vituo vya polisi vipo katika hali mbaya sana. Inasikitisha baadhi ya vituo vya polisi katika wilaya vinatia huruma. Kwa hiyo mimi nilikuwa naiomba tu Serikali na kuishauri Serikali tuweze kuhakikisha kwa namna moja ama nyingine tunakwenda kuboresha maeneo haya ili askari wetu waweze kufanya kazi katika mazingira yaliyokuwa salama zaidi.

Mheshimiwa Spika, la pili nilikuwa naomba nichangie katika eneo la kimkoa hasa katika mkoa wetu wa Pwani. Mkoa wetu wa Pwani ni Mkoa wa kimkakati tuna viwanda vingi sana, na kwatafsiri hiyo wawekezaji wapo wengi sana, lakini huduma za Jeshi la Polisi zinazopatikana hazikidhi haja, hasa katika suala zima la vifaa kama vile gari, gari za zimamotona hivyo kufanya askari wetu kupata tabu sana. Kwa hiyo ni vema Serikali waweze kuangalia katika eneo hili ili kuweza kuhakikisha Mkoa wa Pwani unapewa kipaumbele cha aina yake. Najua ni Tanzania kwa ujumla lakini Mkoa wa Pwani ni Mkoa wa Kimkakati kwa sababu kuna viwanda vingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho naomba nichangie kuhusiana na pale katika jimbo langu la Kibiti. Tunashida ya msingi sana pale katika Jimbo la Kibiti. Katika mwaka 2016 mpaka 2017 kulikuwa na hali mbaya sana ya mambo ya mauaji, na kwatafsiri hiyo Serikali iliweza kutoa tamko ikazungumza kwamba pale Kibiti itakuwa ni Mkoa Maalum wa Kipolisi. Kwa maana hiyo tunakwenda kujenga kituo cha kanda maalum ya kipolisi. Lakini mpaka hivi leo ninavyozungumza miaka takribani sita. Juzi wakati nikiwa nipo jimboni wazee wangu maarufu walinifuata, akiwemo mzee wangu maarufu sana anaitwa Mzee Saidi Lwambo, yeye aliniambia kuna ekari 25 zipo tayari tulizitenga miaka mitano iliyopita lakini mpaka leo Mbunge hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba tu niishauri Serikali; Kibiti tunahitaji tuwe na kituo cha Kanda Maalum ya Polisi kama tamko la Serikali lilivyokuwa linasema. Na huu ni ukweli ulio wazi kwa kuwa Afande Sirro akiwa anakuja kufanya mikutano katika Mkoa wa Pwani anakuja Kibiti na wanakuja askari wote wale, Ma-OCD wanakuja kutoka Kisarawe, kutoka Mkuranga, Kutoka Rufiji wengine kutoka Mafia wanakuja kukutana na Afande Sirro na mikutano inaendelea; na si mara moja wala mara mbili. Kwa tafsiri hiyohiyo Kibiti pale tupo katikati. Serikali ilivyoweza kutoa tamko kusema kwamba hapa ni kwenye kanda maalum ilikuwa ni maana halisi kwamba ni kanda maalum kwelikweli ukizingatia kwamba tumepoteza ndugu zetu wengi sana. Pale tupo katikati ya mkoa, kwa hiyo ni vema Serikali mzingatie suala la kujenga kituo hiki cha polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi nilikuwa naomba tu niseme, kwamba, katika majumuisho ya Mheshimiwa Waziri, na nipo serious katika jambo hili, nitashika Shilingi kama nisipoweza kupata tamko la Serikali kuhusiana na ujenzi wa kituo cha polisi cha Kanda Maalum katika Wilaya ya Kibiti; kwa sababu tumesubiri kwa muda mrefu sana na wananchi wa Kibiti wanahitaji huduma hizi.

Mheshimiwa Spika, Miundombinu iliyopo pale; tunazo eka 25 wananchi wameshazisafisha, zimekaa, kila miezi kila miaka wanasafisha maeneo yale lakini inashangaza Serikali tunashindwa basi hata kutenga cha kuanzia tu; japo milioni 300 au 400; kwamba hiki tunakitoa tunaenda kutengeneza kanda maalum. Kwa kufanya hivyo ni kwamba tunasuburi fedha nyingine zinakuja, lakini jitihada hizo hazijafanyika hata kidogo. Kwa hiyo nilikuwa naomba sana Serikali wahakikishe kuwa wanakuja na majibu ya msingi kuhusiana na suala zima la kanda maalum katika Wilaya ya Kibiti.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya kwa heshima na taadhima naunga mkono hoja. (Makofi)