Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii nami naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Omari Kigua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuipongeza sana Serikali kwa jitihada za haraka ambazo imeshachukua, lakini naomba nasema kwamba jitihada hizi hazitaondoa taharuki iliyopo kwa sasa wala kupunguza mtikisiko wa kiuchumi ambao upo. Hivyo, ninapenda kuishauri Serikali mambo mawili yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ningependa tutambue kuna utofauti wa zile gharama ambazo zinachangia kupanda kwa mafuta kwa maana kwamba zipo kodi za Serikali na zipo kodi za kitaasisi. Kwa hiyo, mimi ningependa kujielekeza katika tozo za kitaasisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo napenda kuishauri Serikali ni kwamba tukiangalia tozo hizi za kitaasisi gharama yake inafikia karibu Shilingi 500. Kwa hiyo, nipendekeza kwa Serikali ione naomna gani ya kuondoa tozo hizi za kitaasisi na tozo hizi za kitaasisi haziathiri moja kwa moja mapato ya Serikali kwa maana ya kodi za Serikali, vilevile hazitagusa zile tozo ambazo zipo ringfenced kama maji pamoja na REA kwa maana ya umeme vijijini. Jambo hili linawezekana na hata hivi karibuni tutakumbuka kwamba Serikali iliondoa Shilingi 100 katika tozo hizi za mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo huo napenda kuishauri Serikali kwa msisitizo mkubwa ione namna gani ambavyo itaondoa tozo za kitaasisi ambazo zinakaribia gharama ya Shilingi 500. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, natambua kwa kuokoa...

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Saashisha.

T A A R I F A

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninampa Msemaji Dada yangu Mheshimiwa Neema taarifa kwamba, pamoja na tozo hizi za kitaasisi, lakini kuna fedha ambazo zipo kwenye madini. Madini ambayo yamekuwa yakikamatwa kama faini sasa hivi ni wakati sahihi Serikali iuze, iweze kuingiza huku kama sehemu yakusaidia uchumi wetu ikiwa ni pamoja na zile dhamana zinazowekwa mahakamani, sasa hivi ziletwe ziingie huku. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Saashisha anayepewa taarifa yupo nyuma yako hapo.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, aahaa!

SPIKA: Haimaanisha uongee naye, ongea na mimi. (Kicheko)

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho, fedha zile za CSR ambazo zinatolewa na Taasisi tunaweza tukaamua mwaka mmoja zote tuzichukue ziingie humu ziweze kutusaidia, ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Neema Lugangira, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana naipokea taarifa hiyo.

Mheshimiwa Spika, naendelea kusisitiza na kurudi palepale kujielekeza kwamba Serikali ione namna gani ya kuondoa tozo hizi za kitaasisi ambazo zinakaribia Shilingi 500 na jambo hili linawezekana na linaweza kufanyika kwa uharaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa pili kwa Serikali ni kwamba natambua baada ya tozo hizi za kitaasisi kuondolewa taasisi hizi zitakuwa na mapato mapungufu. Hivyo, Serikali itafute fedha za kuweza kutoa ruzuku au subsidy kwa hizi taasisi. Moja ya njia ambayo Serikali inaweza ikafanya ni kwa kuitisha vikao vya dharura na mashirika ya fedha yanayotudai yaani creditors wetu ili kujadiliana nao namna gani ambavyo tutaweza kupata kipindi maalum cha kutolipa yale makato ya mwezi. Tuweze kufanya loan repayment re-scheduling jambo ambalo linakubalika na katika majadiliano hayo Serikali iweze pia kuhakikisha ya kwamba kutakuwa hakuna penalty za aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo, endapo tutafanikiwa katika jambo hilo basi ile fedha ambayo kila mwezi Serikali hivi sasa inatumia kulipa makato ya hii mikopo tuliyonayo ambayo ni takriban Bilioni 600 mpaka Bilioni 800 kila mwezi, fedha hiyo Serikali itaweza kutumia kuleta kwenye uchumi kama subsidy ili kupunguza makali ya kiuchumi na wananchi wote kwa ujumla tuweze kupata ahueni kutokana na janga hili la kiuchumi tulilo nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naamini kabisa Serikali sikivu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, itachukua ushauri wa Wabunge kwa uzito mkubwa na itaweza moja, kutoa tozo hizi za kitaasisi ili kupunguza gharama za mafuta. Pili, kuitisha mikutano ya dharura na mashirika ya kifedha yanayotudai ili kuona namna gani ambavyo tutaweza kufanya loan repayment scheduling. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa fursa hii, naunga mkono hoja. (Makofi)