Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niwe mchangiaji wa kwanza katika hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Kigua kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa letu lakini pia ya wananchi wetu ambao tunawawakilisha humu Bungeni. Nikupongeze pia wewe kwa kukubali kutusikiliza.

Mheshimiwa Spika, sisi tunaotoka kijijini leo bei ya dizeli ambao kwenye Majimbo yetu wengi tunatumia mafuta ya vidumu leo tunauziwa mafuta shilingi 5,000; hii ni hali mbaya sana na ndiyo maana busara yako imeona namna nzuri ya kuweza kutusikiliza.

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati; nilikuwa nataka kuomba Serikali itueleze tu ukweli, kwamba mafuta haya ambayo yamepanda bei juzi ni mafuta yamenunuliwa mwezi wa pili, sasa yamepanda yakiwa kwenye meli. Pamoja na kwamba bei zina-reflect Ulaya, lakini yakiwa tayari yameshanunuliwa kwenye meli bei imeongezeka. Sasa lazima Serikali ione namna.

Mheshimiwa Spika, ni mimi ni mmoja wa wafanyabiashara. Sisi tunacheza na namba tu, ukilegea kwenye namba sisi tunapita hapo hapo. Kwa hiyo, ni vizuri na ni lazima Serikali ione namna.

Mheshimiwa Spika, wewe ulikuwa humu Bunge lililopita, iliwahi kushuka bei ya korosho hapa Serikali ilipeleka Jeshi kwenda ku-rescue ile situation ya korosho; na baada ya hapo mpaka leo hakuna mtu anachezea bei ya korosho kwa sababu wanajua kabisa kwamba kuna tahadhari tukileta mchezo Serikali itaingia kwenda kuchukua hii biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe, Serikali kwenye hili hakuna namna, yaani kazi ya Serikali ni lazima kutuangalia sisi wananchi wake. Kama hali inatokea ya dharura kwa nini Serikali isiwe na dharura? Tuna dola kwenye benki, BoT tuna dola, hili jukumu kama linakuwa ni la kibiashara kwa nini Serikali isichukue dharura ya yenyewe kuagiza mafuta angalau ikakubali kula hasara hata kwa kitu kidogo? Lakini kama hamna, tuone namna kabisa kama Bunge, hii hali siyo nzuri na bado mafuta mwezi ujao yatapanda tena kwa takriban shilingi 3,800. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala halikubaliki, sisi Wabunge, kama kuna kodi tuliziweka kwenye mafuta, kuna vitu tuliweka tuone namna ya kuondoa hizo kwa dharura hii ya miezi mitatu ili mafuta yarudi kuwa chini na wananchi waweze kufaidi Serikali yao.

Mheshimiwa Spika, na nipongeze pia Serikali, nimeona hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri mliokaa jana; hii ndiyo Serikali ambayo tunaitaka, siyo mkae kimya. Sisi tulalamike na Serikali ilalamike hapa, tokeni na jibu. Nimeona mmesema tuwape muda, sisi kama wawakilishi wa wananchi tunasema tumekubaliana na hilo; lakini sasa mtoke na kitu ambacho hata kama ni dharura Bunge tukae tena kutengua hata kitu chochote kwenye bajeti ili tuone namna ya kupunguza bei. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu inakubalika kukopa Kimataifa na tunakopa, tukopeni tufidie hizi gharama ili mafuta yaweze kushuka kwasababu kwa sasa hakuna Mtanzania atakayeweza ku-afford mafuta. Halafu hili Waheshimiwa Wabunge hata sisi wenyewe linatupiga; kwa sababu tunalipwa mileage za kwenda vijijini, leo mimi mileage yangu ya kwenda Geita inaishia Shinyanga, sasa kutoka Shinyanga kwenda kule na kurudi ninarudije, na mimi ni Mbunge bado kuna watu wa chini.

Mheshimiwa Spika, mimi ni msafirishaji yaani kwa sababu tu watanzania tuna nidhamu ya kuiheshimu Serikali na kuwapa muda. Hebu jiulize msafirishaji aliyekuwa anapeleka abiria kwa shilingi 30,000 leo Mwanza. Leo mafuta yamefika shilingi 3,400 bado nauli shilingi 30,000, hili haliwezekani lazima sisi kama Bunge tukubaliane tuishauri Serikali na Serikali ije na kauli nzuri. Hatua mliyoianza ni nzuri, hatutaki tena kusikia tunalalamika, mkae mtoke na kauli moja ili wananchi waweze kufaidi na Serikali yao ya Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)