Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye Wizara hii muhimu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba nchi nyingi ambazo zimeendelea waliwekeza, Serikali ilitenga bajeti kubwa ilielekeza fedha nyingi kwenye Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ni Wizara ambayo ndiyo engine ndiyo ina uwezo wa kusisimua uchumi kwenye Wizara zingine nyingi kwa sababu wao ndiyo connection kati ya uchumi kwa maana ya uwekezaji na maendeleo ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2021 Tanzania waliingia kwenye Mkataba wa Umoja wa Afrika Mkataba unaitwa Africa Continental Free Trade Area, mwaka 2021 sisi ndiyo tulisaini. Kwenye mkataba huu katika nchi 55 ambazo ni wanachama nchi 54 zimeshasaini na lengo la huo mkataba ni kufungua biashara na huduma katika nchi za Afrika ambazo ni wanachama kutufungua ili tuweze kusafirisha biashara na kuepuka ushuru na gharama mbalimbali ambazo zinaweza kuwa ni vikwazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hivi kweli Tanzania tuko tayari kuanza kwenda kuuza kwenye hizo nchi zingine ambazo ni wanachama? Au ukiangalia kiuhalisia sisi ndiyo tutakuwa tunaletewa bidhaa kuliko kuuza huko nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma kwa mfano kwenye ripoti ya CAG ya mwaka 2022; SIDO ambao ni Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo waliomba bajeti kwa ajili ya kuboresha mazingira ya uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo. Kwenye bajeti waliyoomba ya shilingi bilioni 21 ili waweze kuendeleza maeneo hayo wamepewa shilingi bilioni 1.7 na kwa sababu hiyo asilimia 70 ya maeneo ambayo ya kimkakati walidhani watakwenda kuendeleza kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda vidogo vidogo haikuendelezwa. Tafsiri yake ni kwamba Watanzania tumeshindwa kuwekeza kwenye viwanda hata kama Rais wa nchi akiwa na nia njema kiasi gani, akizunguka duniani kiasi gani kutafuta wawekezaji unufaikaji wa Watanzania kwenye eneo la viwanda na biashara ni ndoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2018/2019 hapa Bungeni kwenye Finance Bill tulihamisha Shirika linalosimamia ubora wa chakula tulilihamisha tukalirudisha TBS. Sasa TBS inakagua ubora wa matairi, TBS inakagua ubora wa matofali, TBS inakagua ubora sijui wa magari. TBS hiyo hiyo ianze kuangalia ubora wa maparachichi, TBS hiyo hiyo ianze kuangalia ubora wa matikitiki maji, tutafika kweli Na hiyo practice dunia nzima ubora wa chakula una kitengo chake idara yake maalum ambayo inatakiwa isimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kama tukitangaza vipi Tanzania kwamba tunaweza kwenda kuwekeza na Waziri anasema sasa hivi tunaweza kwenda kuuza mazao yetu nje, huwezi kuuza mazao ambayo yamezalishwa chini ya kiwango. Waziri anaongelea habari ya uzalishaji wa parachichi, alizeti kama haijapimwa, haijasimamiwa ina afya toxin nyingi hayo mahindi ukitaka kwenda kuuza nje mwisho wa siku yatazuiwa mpakani yatarudishwa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mwisho wa siku Tanzania rasilimali tuliyonayo wala hatuhitaji kuweka incentive, wala hatuhitaji kusema tunawavutia watu, Tanzania ina madini, mtu yeyote anayetaka kufanya biashara atakuja kuchukua madini Tanzania bila kujali kwamba umempunguzia ushuru kiasi gani, mtu yeyote anayefanya biashara atakuja kuchukua mazao Tanzania kwa sababu chakula ni hitaji muhimu kwa binadamu yeyote, lakini mwisho wa siku ni lazima Wizara ya Viwanda na Biashara ikasimame kama muhimili ambao unasaidia kufungua Watanzania wawekezaji wadogo wadogo na Serikali na mataifa ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ya Viwanda na Biashara ni Wizara nyeti sana, ndio Wizara ambayo inatakiwa iwe na wachumi na watafiti wanaoweza kuishauri Serikali uwekezaji wa kimkakati ambao unaleta tija kwa Taifa na unaongeza pato la Taifa. Pale kwangu Shinyanga Mjini wamejenga inaitwa machinjio ya kisasa, five billion za Serikali zimewekezwa pale wanasema wakati wanaleta huo mpango kwa bashasha wanasema wanawekeza bilioni tano kujenga yale machinjio ya kisasa kwa maana gani, kwa siku tutaweza kuchinja ng’ombe na mbuzi wasiopungua 500.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa tatu/wa nne sasa hivi ng’ombe wanaochinjwa pale hawafiki 15; five billion imewekezwa hiyo ni kazi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuishauri Serikali uwekezaji wa kimkakati. Ukienda Kibaha kuna kiwanda pale Serikali imezika fedha billions of money kiwanda cha viuwadudu na kaka yangu ameeleza vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kile kiwanda pale Serikali imeweka fedha na viuwadudu hivyo vinavyotakiwa kuuwa malaria ni ugonjwa unaoongoza kuuwa Tanzania. Viuwadudu vinavyoweza kuuliwa na dawa ambazo zinazalishwa kwenye kiwanda kile ambacho tumeingia ubia na Cuba ni pamoja na wadudu wanaoleta malaria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekazana kununua neti, Serikali inatoa fedha nyingi kwenda kutibu watu na madawa tunajisifu kwamba tuna madawa na tumefungua hospitali kila kata, kila Kijiji, sijui kila nini, lakini kiuhalisia wale wadudu wangeweza kuteketezwa na hii ndio kazi ya Viwanda na Biashara, ndio maana hii Wizara imekuwa unpopular labda ni kwa sababu sijui haina fedha au haionekana kama ni Wizara ya muhimu, lakini sasa hivi ambapo Mheshimiwa Rais analeta uwekezaji ndani ya nchi Waheshimiwa Mawaziri mumsaidie kumshauri, ninyi ni cross cutting, ni Wizara mtambuka, mnauwezo wa kwenda kushauri kwenye kilimo, kwenye mifugo, kwenye afya, kwenye madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi Mheshimiwa Biteko wakati anajibu hotuba yangu niliyoongea kuhusu madini anasema anakwenda kuwasaidia wafanyabiashara wa madini wale wadogo wadogo kwa kuwapa mikopo na kuwaombea kwenye benki, lakini Wizara yako inatakiwa ijue Je, hiyo mikopo wanayopewa wawekezaji wadogo ina tija, wale watu wanaenda kupewa mikopo condition namba moja anatakiwa apeleke hati, sasa yule mchimbaji mdogo mdogo anayekaa kule Mwakitolyo mchimbaji mdogo mdogo wa Mwazimba sijui kule…, anatoa wapi hati ya nyumba ili aweze kupata mkopo? Uwekezaji mdogo anaambiwa riba atalipa kwa mwezi na riba ya kibiashara kama mtu aliyefungua duka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi ili niweze kupata madini lazima kwanza nianze kuchimba shimo, nifunge matimba, nivute maji nikimaliza kuvuta maji nianze kuchimba, nipeleke plant, niende nikachenjue, miezi tano, sita, saba, sasa miezi sita saba unamwambia huyu mfanyabiashara alipe riba kwa mwezi hiyo fedha anaitoa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa ya Wizara ya Viwanda na Biashara ni kuangalia uwekezaji wenye tija na mimi nishauri Wizara hii itengeneze kamati maalum au timu maalum…

(Hapa kengele ililia kushiria kwisha muda wa Mzungumzaji)